Kampeni za Ukawa sasa anga kwa anga




Mwenyekiti wa Chadema ,Freeman Mbowe akihutubia
By Fidelis Butahe

Rukwa. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Katibu Mkuu
wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa aliyetangaza kujiondoa ni sawa na abiria
wa treni ya kati aliyeshukia njiani kabla ya mwisho wa safari, huku mgombea urais wa chama hicho chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa akisema: “Tanzania ya CCM sasa basi, ni wakati wa mabadiliko.”
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nduwa, Sumbawanga, Mbowe akiwa sambamba na Lowassa alisema hakuna kiongozi wa Chadema ambaye ni mkubwa kuliko chama hicho.
“Mtu yeyote anaweza kuondoka katika chama lakini kikabaki salama na kuendelea na safari yake ya mabadiliko,” alisema na kushangiliwa na maelfu ya wananchi wa mji huo waliojitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga kuwapokea viongozi hao wakitokea Ruvuma.
Juzi, Dk Slaa alitangaza kuachana na siasa za vyama kutokana na kutofautiana na viongozi wa Chadema juu ya masharti ya kumpokea Lowassa.
Mbowe ambaye alipokewa na mabango ya kumtaka atoe kauli kuhusu Dk Slaa alisema: “Watu wengi waliniambia nikifika hapa nizungumze habari ya Dk Slaa sasa ngoja niwaambie kwa kifupi sana.”
Alisema mwaka 1992, Chadema kilipoundwa kilianza safari yake, akiifananisha na ile ya treni ya Reli ya Kati inayoanzia Dar es Salaam hadi Kigoma, kwamba katika safari hiyo wapo wanachama walioshukia njiani, akimaanisha walioamua kuachana na chama hicho... “Tukafika Pugu wapo walioshuka na wengine wakapanda, tulipofika Morogoro wapo walioshuka na wapo waliopanda. Oktoba mwaka huu treni itafika Kigoma mwisho wa reli na tutaingia Ikulu,” alisema.
Alisema vikao vya Baraza Kuu, Kamati Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho vilikubali Lowassa kuwa mgombea urais wa Chadema na Ukawa... “Hiyo ndiyo habari ya mjini, sasa kama kuna mtu na mke wake wana mawazo tofauti watatukuta mbele ya safari. Hatuna muda wa kupoteza tunahitaji mabadiliko.”
Mbowe aliwataka askari kuwalinda wananchi kwa maelezo kuwa Oktoba 25 wataamua hatima ya nchi yao kwa kukichagua Chadema kuingia Ikulu na kusisitiza kuwa uamuzi ya Watanzania hausababishwi na mapenzi kwa Chadema, bali maumivu, tabu, umaskini, ujinga, kukosa maji, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi na ukosefu wa pembejeo.
“Tusijenge uadui na askari polisi kwa sababu ni ndugu zetu, wadogo zetu, baba zetu na tunawahitaji kama wao wanavyotuhitaji, nao wanahitaji mabadiliko kwani wapo hoi,” alisema.
Mbowe aliwataka wanaCCM kuiga mfano wa Lowassa kwa kujiunga na mabadiliko na kuwataka wanachama wa Chadema kuwashawishi wanachama wa chama hicho tawala kujiunga na safari ya mabadiliko.
Lowassa apunguziwa safari
Alisema Chadema kimeunda timu nne zitakazoundwa na wabunge wake kwa ajili ya kuzunguka mikoa mbalimbali kufanya kampeni kwa maelezo kuwa Lowassa hawezi kumaliza majimbo yote ya uchaguzi ndani ya siku 60 za kampeni zilizopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema wabunge hao watatumia helikopta (chopa) nne kuzunguka katika majimbo mbalimbali.
Wabunge hao waliomaliza muda wao na majimbo wanayogombea katika mabano ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), David Silinde (Momba), Ezekia Wenje (Nyamagana), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Halima Mdee (Kawe), John Mnyika (Kibamba) na yeye mwenyewe.
Alisema kuna majimbo ya uchaguzi 265 na Lowassa akifanya kampeni katika majimbo manne kwa siku, atamaliza majimbo 240 ndani ya siku 60, kwamba yapo ambayo atashindwa kuyafikia.
Lowassa
Akizungumza katika mkutano huo, Lowassa alisema licha ya kutawala kwa miaka zaidi ya 50, CCM imeshindwa kumaliza matatizo yanayowakabili wananchi. “Nipeni dhamana ya kuibadilisha nchi yetu kwani chama hiki (CCM), kipo miaka 50 lakini hakuna kilichofanya. Nipigieni kura na kulinda kura yako.”
Lowassa alisema akiwa rais wa awamu ya tano, elimu itakuwa bure na atafuta kodi na ushuru kwa wakulima, kusisitiza kuwa anataka kuwaonyesha Watanzania kuwa anaweza kuwaletea mabadiliko na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo makubwa.
Aanza kutumia chopa
Jana, Lowassa alianza kutumia chopa katika mikutano yake ya kampeni ili kurahisisha kuwafikia wapiga kura wengi zaidi. Mbali na chopa, mgombea huyo ambaye ameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma pia atatumia ndege.
Jana aliruka na chopa kutoka Songea Mjini na kufanya mikutano Mbinga na Namtumbo na baadaye Sumbawanga.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema: “Tutakuwa na chopa nyingi si moja lakini hawezi kuitumia kila siku na kuna maeneo atatumia ndege. Suala la matumizi ya chopa pia linahitaji vibali.”
Kwa mujibu wa ratiba ya NEC leo Lowassa atafanya mkutano wa kampeni Mlele na Mpanda mkoani Katavi na kesho atakuwa mkoani Kigoma ambako atafanya mikutano Uvinza, Kigoma Vijijini na Kigoma Mjini.
Keshokutwa atakuwa Tabora ambako atatumia siku mbili kufanya mikutano wilaya za Sikonge, Urambo, Tabora Mjini, Nzega na Igunga.
Septemba 7, atafanya mkutano jijini Dar es Salaam katika jimbo la Kibamba na Bunju na kuendelea katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera na Mtwara.
-chanzo:mwananchi

No comments:

Powered by Blogger.