Tumbua Tumbua ya John Pombe Magufuli, Vigogo Hawa Wingu Jeusi

Ni wingu jeusi kwao! Mpaka sasa, Rais Dk. John
Pombe
Magufuli ‘JPM’ ameshawatumbua majipu karibu nusu ya vigogo wa taasisi za
serikali lakini habari mpya ni kwamba, maafisa wa usalama wa taifa ‘makachero’
wamekuwa wakishinda kwenye taasisi kubwa za serikali na kupekua nyaraka
mbalimbali ili kubaini utendaji uliotukuka au mbovu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, makachero hao wamekuwa
wakiingia kwa kushtukiza kisha kujitambulisha wao ni akina nani na kuomba
nyaraka zinazohusu kitu ambacho wamekwenda kukichunguza.
MSIKIE MTOA HABARI
“Kinachofanyika sasa ni kwamba, usalama wa taifa wanakwenda
kwenye taasisi waliyoilenga, wanaomba nyaraka kutoka kwa wahusika, wanafuatilia
utendaji wa taasisi hiyo kisha wanaondoka na majibu mkononi.”
HABARI KWA MAWAZIRI, WAZIRI MKUU
“Kama taasisi ikikutwa na madudu, habari zinapelekwa kwa waziri
mwenye dhamana na taasisi hiyo au moja kwa moja kwa Waziri Mkuu, Kasimu
Majaliwa.
ZILITEM-BELEWA
“Taasisi zote ambazo watendaji wake wakuu wametumbuliwa majipu
walishatembelewa na watu wa usalama wa taifa. Unajua serikali hii inafanya sana
kazi na hawa jamaa. Ndiyo maana kama utafuatilia sana, utabaini kuwa, kila
waziri na waziri mkuu akifika mahali penye figisufigisu anasema mambo ambayo
kwa akili za kawaida unajua alishaambiwa kabla hajafika.”
Kaimu M James Anditile – TPDC
Chanzo hicho
kilizitaja taasisi ambazo zinafuatiliwa na makachero kuwa ni Tanesco (Shirika
la Ugavi wa Umeme Tanzania, linaongozwa na Felchesmi Mramba), Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC, linaloongozwa na Nehemia Mchechu), Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL, inayoongozwa na Kazaura Kamugisha na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC, linaloongozwa na James Anditile).
Kazaura Kamugisha – TCCL
Taasisi nyingine ni
Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa, inayoongozwa na Allan Kijazi), Shirika la
Madini Tanzania (Stamico, linaloongozwa na Edwin Ngonyani) na Shirika la
Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido, linaloongozwa na Omar Bakar).
Pia alizitaja taasisi
za Benki Kuu ya Tanzania (BoT inayoongozwa na Ben Ndulu), Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura inayoongozwa na Felix Ngamlagosi) na
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra inayoongozwa na
Gilliard Gewe).
Edwin Ngonyani – STAMICO
Hata hivyo, chanzo
chetu kilisema kuwa, si kwamba kufuatiliwa kwa taasisi hizo ina maana
wakurugenzi wake wana madudu.
“Hizi taasisi kama
nilivyosema awali, zinafuatiliwa kwa sababu serikali ya Magufuli inataka
kujiridhisha katika kila idara. Kama viongozi wake wako sawa watapona na
wataendelea na kazi, hakutakuwa na uonevu. Kwa hiyo si kwamba wamebainika kuwa
na utendaji mbovu, hapana,” kilisema chanzo hicho.
TANESCO, NHC HAKUKALIKI
Juzi gazeti hili
lilipiga hodi Tanesco Makao Makuu jijini Dar kwa lengo la kuzungumza na Afisa
Habari, Adrian Sevelin lakini hata hivyo hakuwepo ofisini.
Mfanyakazi mmoja
ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema hali ya Tanesco kwa sasa ni kazi kwa
kwenda mbele kwani bosi wao mkuu, Mramba amekuwa mkali na kufuatilia utendaji
wa kazi wa kila mtu.
Ndulu – BoT
“Nyie kama waandishi
hapa Tanesco sasa si kama miaka ile. Huyu Mramba, japokuwa hata kabla ya
Magufuli alikuwa mkali, lakini da! Sasa hivi mfanyakazi akitoa mguu na yeye
kaweka. Anafuatilia utendaji wa kazi wa kila mmoja mpaka pamekuwa pachungu,”
alisema mfanyakazi huyo maelezo ambayo yanafanana na ya mfanyakazi mmoja wa
NHC.
Gilliard Gewe – Sumatra
Mpaka sasa, taasisi
ambazo wakurugenzi au watendaji wake wakuu wameshakumbwa na tumbuatumbua ya
Magufuli ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ambapo
mkurugenzi wake, Edward Hosea alitenguliwa uteuzi wake na rais na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA ambapo mtendaji wake mkuu alikuwa Rished Bade).
Felichesmi Mramba – Tanecso
Taasisi nyingine ni
Hospitali ya Taifa Muhimbili (mkurugenzi alikuwa Dk. Hussein Kidanto), Kampuni
ya Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco, mkurugenzi wake alikuwa
Mhandisi Benhadard Tito), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA, mkurugenzi wake
alikuwa Awadhi Massawe), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA, mkurugenzi wake
alikuwa Charles Chacha).
Nyingine ni Idara ya
Uhamiaji Tanzania (mkurugenzi wake alikuwa Sylvester Ambokile), Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida, mkurugenzi wake alikuwa Dickson Maimu) na wengine
wengi, wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya.
No comments: