JK: Tutafunga CCTV kukabiliana na uhalifu



Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
By Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya
Kikwete amesema ili kuwaweka salama wananchi kamera maalum za CCTV
zitafungwa katika miji mikuu kukabiliana na wahalifu nchini.
Rais Kikwete alisema hayo juzi katika hafla ya kuagana na wapiganaji na walinzi wa usalama iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Alisema ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, Serikali inakamilisha mpango wa kufunga kamera hizo.
“Tutakomesha huu wizi wa kupora mali za watu kwa kutumia pikipiki kwa sababu kamera hizo zitakuwa zinaona sehemu zote za mji,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Tanzania lazima iendelee kuwekeza ipasavyo katika ujenzi na uimara wa majeshi yake kila wakati. “Hata katika mambo ya kiraia, msipowekeza katika usalama wa raia, wezi watawasumbua kila siku kwa kuvamia benki na kuiba pesa za wananchi.
“Kadri uchumi wa Tanzania unavyozidi kukua ni lazima majeshi ya ulinzi nayo yaboreshwe kwa sababu uchumi imara ni lazima ulindwe na jeshi imara,” alisema.
Rais Kikwete pia alisifia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuiletea nchi sifa na heshima kubwa katika kipindi cha uongozi wake.
Alisema anaondoka madarakani akiwa na furaha kwa sababu ya mchango wake katika ujenzi mkubwa wa majeshi kwa miaka 10.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na maofisa wa JWTZ, polisi, magereza, idara ya usalama wa Taifa na uhamiaji alisema: “Tumelinda amani na utulivu, katika mipaka ya nchi yetu. Pia tumegundua gesi asili, hivyo ni lazima ilindwe vingivevyo nchi itakuwa na watu wa ajabu.
“Watu wanaiba samaki wetu katika bahari kuu na ndiyo maana tulizindua meli mbili mpya kubwa za MV Butiama na MV Msoga kwa ajili ya Kamandi yetu ya Maji.”
Rais Kikwete alimkariri Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchill ambaye alikuwa askari na alisema:
“Uimara wa uchumi lazima ulindwe na uimara wa jeshi la nchi. Uchumi wa nchi lazima ulindwe kwa upanga.”
Rais Kikwete alisema: “Mwaka 2005, hatukuwa na ndege ya kijeshi iliyokuwa inaruka. Sasa tuna Jeshi la Anga lililo kamili.
“Tumejenga kikosi cha mizinga na vifaru...pia tuna uwezo wa kuaminika.”
Hata hivyo alisema ujenzi wa nyumba 6,000 kati ya 10,000 za wanajeshi umekamilika.
-chanzo: mwananch

No comments:

Powered by Blogger.