Mahadh ataja kinachomnyima namba kikosi cha kwanza Yanga

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Juma Mahadh anayelalamikiwa kushuka kiwango, amevunja ukimya na kutaja kinachomfanya kukosa namba ndani ya kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Wakati mchezaji huyo akipasua jipu, Mzambia George Lwandamina, amewaaga wachezaji wake wa timu ya Zesco ya nchi hiyo, tayari kuanza kuinoa Yanga inayotajwa kumalizana naye.

Mahadh ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Yanga waliotua katika kikosi cha Mholanzi, Hans van der Pluijm kwa kishindo akitokea Coastal Union iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika siku zake za mwanzoni ndani ya kikosi hicho cha Jangwani, Mahadh alionyesha kiwango cha juu mno kiasi cha kutabiriwa kung’ara mno msimu huu.

Na kati ya mechi iliyofanikiwa kulitangaza vilivyo jina la Mahadh, ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu kati ya Yanga na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyopigwa Juni 28, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ulioishia kwa Yanga kufungwa bao 1-0, mchezaji huyo alicheza vizuri mno kiasi cha kufikiriwa kuwa na uwezekano wa kutua katika kikosi cha miamba hiyo ya soka Afrika.

Lakini kadiri siku zinavyokwenda, mchezaji huyo alianza kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga, ikiwamo kuenguliwa timu ya Taifa, Taifa Stars.

Wakati mashabiki wengi wa Yanga wakijiuliza kulikoni, Mahadh hatimaye amevunja ukimya na kuanika kila kitu, huku akiapa kukabiliana na changamoto inayomkabili ili aweze kurejea katika kiwango chake kilichomwezesha kutoka Coastal na kutua Jangwani.

Akizungumza na BINGWA, Mahadh alisema kinachomkwaza ni benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Pluijm kumpa muda mfupi wa kuwapo uwanjani.

Alisema tangu alipoboronga dhidi ya Simba Oktoba mosi mwaka huu, amekuwa hapewi nafasi ya kutosha ya kumwezesha kufanya vitu vyake.

“Kwa kweli nimekosa kujiamini na kucheza nilivyokuwa nikicheza Coastal Union msimu uliopita kwani kwa sasa napewa dakika 10 hadi 20, kitu ambacho kimekuwa kikiniangusha sana,” alisema Mahadh.

Mahadh alisema ili mchezaji acheze vizuri katika mechi, ni lazima apewe muda mrefu wa kucheza mechi nyingi awe na uwezo wa kujiamini na kuzoea mazingira ya mchezo kwa ujumla.

“Ukiangalia dakika10 hadi 20 ninazocheza, siwezi kufanya lolote. Ni kweli kuna mechi nilikuwa nikiboronga, hicho ni kitu cha kawaida kwa mchezaji, hata Ulaya wachezaji nyota huwa kuna siku wanacheza chini ya kiwango na bado wanaendelea kupangwa…mfano mzuri ni Wayne Rooney wa Manchester United,” alisema kinda huyo.

Alisema kitendo cha kupewa muda mfupi, kinamfanya kucheza kwa presha kubwa na kutojiamini ukijiona kama umeingizwa tu ilimradi.

Mahadh alisema ligi itakaposimama kuanzia Alhamisi ya wiki hii, atahakikisha anajifua hasa ili aweze kuwa fiti zaidi, ikiwamo kujiandaa kisaikolojia tayari kukabiliana na changamoto hiyo inayomkabili.

“Ninachopenda kuwaambia watu wa Yanga, wasiwe na wasiwasi juu yangu, ligi itakaposimama, nitahakikisha ninajipanga upya ili mzunguko wa pili ukianza, nirejee nikiwa Mahadh mpya,” alitamba kinda huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, chenga na kufunga mabao pia.

Juu ya Lwandamina, habari kutoka Zambia zinasema kuwa kocha huyo juzi aliwaaga wachezaji wake wa Zesco baada ya mchezo dhidi ya Nkana Reds ambao walilala kwa mabao 3-2.

Na tayari uongozi wa Zesco umekiri juu ya kuondoka kwa kocha huyo katika taarifa iliyotolewa mapema jana asubuhi.

Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Zesco, Justin Mumba na Ofisa Habari, Katebe Chengo, walisema klabu hiyo imekubali uamuzi huo na kumshukuru Lwandamina kwa kazi na mchango mkubwa kwa wakati wote waliokuwa naye.

Lwandamina alijiunga na klabu hiyo mwaka 2014 na ameshinda mataji mawili ya ligi, moja la Kombe la Barclay, Ngao ya Jamii na kuiongoza timu hiyo kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016.

“Klabu inapenda kutangaza kwamba kocha msaidizi, Tenant Chembo, ameteuliwa kuwa kaimu kocha mkuu hadi mwishoni mwa msimu. Tunamtakia kila la kheri Lwandamina katika safari yake mpya,” ilisomeka taarifa hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa kocha huyo anatarajiwa kutua nchini kesho akiwa ameambatana na watu wawili, lakini haijajulikana kama watakuwa ni wachezaji au wasaidizi wake.

No comments:

Powered by Blogger.