Jonas Mkude aanika siri nzito Simba
SIKU moja baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya African Lyon, nahodha wa Simba, Jonas Mkude, amepasua kilichowaponza juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, akiwataka wenzake kukwepa mtego huo iwapo wanahitaji kumaliza ukame wa mataji Msimbazi.
Simba juzi ilipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa African Lyon, kikiwa ni kipigo chao cha kwanza msimu huu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkude alisema licha ya kutengeneza nafasi nyingi juzi, walishindwa kufunga kutokana na wapinzani wao hao kucheza kwa kukamia na kupaki basi.
“Tumecheza vizuri na tumetengeneza nafasi ila nilichokiona wenzetu walikuwa wamepanga kuja kulinda zaidi ili kutuzuia na ndio sababu ilitufanya kupoteza mchezo wetu,” alisema.
Hata hivyo, alisema wanashukuru kwa kila kilichotokea kwa sababu ni hali ya mchezo wa soka kuna kupoteza na mashabiki wao wameendelea kuwaunga mkono na wanachoangalia ni mchezo uliobaki wa kumaliza mzunguko wa kwanza.
“Tumefungwa, lakini tunashukuru pia kwa matokeo haya kwa sababu sio tusubiri tumeshinda ndio tufanye hivyo. Napenda kuwashukuru mashabiki na wadau wote wa Simba na waendelee kutusapoti kwa kila jambo,” alisema Mkude.
Simba inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 14, ikishinda 11, sare mbili na kupoteza mmoja.
Wekundu wa Msimbazi hao wanatarajiwa kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa kupepetana na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine kesho.
No comments: