Mali za CUF zatoweka

BAADHI ya mali za Chama cha Wananchi (CUF) hazijulikani zilipo na tayari Prof. Ibrahim Lipumba ameanza kuzisaka, 

Taarifa kutoka kwa chanzo chetu ndani ya CUF zinaeleza kuwa, miongoni mwa mali hizo ni magari matano ya chama hicho.


Taarifa zaidi zinaeleza, kabla ya Prof. Lipumba kuingia Ofisi Kuu ya chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam jana mchana, magari hayo yalikuwa tayari yameondolewa.

Na kwamba, juhudi za kutaka kujua magari hayo mahala yalipo zimeanza kuchukuliwa kwa Prof. Lipumba kuwasiliana na baadhi ya viongozi waliokuwa na dhamana na ofisi hiyo kabla ya jana.

“Magari kama sita hayapo ndani ya ofisi hizo, Prof. Lipumba ameanza kuuliza magari hayo yapo wapi?,” kimeeleza chanzo hicho na kuongeza;

“Alimpigia Mtatiro (Julius Mtatiro-Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF) lakini alisema hajui, akampigia Paku (Abdalla Paku-Ofisa Utawala wa CUF) alikata simu na alimpigia Bashange (Joram Bashange Mkurugenzi wa Fedha wa CUF) alimjibu kuwa yupo mkoani.”

Hata hivyo, mtandao huu umemtafuta Abdul Kambaya anayetajwa kuwa mtu wa karibu na Prof. Lipumba ambaye amethibitisha taarifa hizo.

“Ni kweli magari hayapo na Profesa amekuwa akifanya juhudi za kutaka kujua magari hayo yalipo.

“Bado hatujaangalia mambo mengine zaidi lakini kuna baadhi ya vitu havipo na tutaendelea kuangalia mali ipi ya chama na nani anayo,” amesema Kambaya na kuongeza;

“Mali za CUF ni za wanachama wote na hakuna shaka tutajua zilipo. Hatuamini kama zimetoka nje kwa njia za hovyo ila naamini mwenyekiti anataka kujua tu mali hizo zipo wapi kwa kuwa anawajibuka kujua.”

Kambaya amebainishwa kwamba, Prof. Lipumba amekuwa akiwasiliana na baadhi ya viongozi ili kutaka kujua yalipo magari hayo.

“Sijui kwa watu wengine lakini najua kuwa amewasiliana na Bashange ambaye alijibu kwamba yupo nje ya Dar es Salaam,” amesema Kambaya.

Jana kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho kulikuwa na hekaheka kutokana na Prof. Lipumba kurejea ofisini hapo akisindikizwa na wafuasi wake.

Hatua hiyo iliyokana na taarifa ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliyotolewa jana ikieleza kumtambua Prof. Lipumba kwamba ni mwenyekiti halali wa chama hicho kwa mujibu wa taratibu.

“Baada ya upembuzi wangu ni kuwa, Lipumba bado mwenyekiti halali wa CUF na waliofukuzwa, kusimamishwa ni wanachama halali.

“Viongozi ambao uamuzi wao uliathirika na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa bado ni viongozi halali wa CUF,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Prof. Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na ujio wa Edward Lowassa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hata hivyo, Agosti mwaka huu CUF ilimsimamishwa uanachama Prof. Lipumba kwa tuhuma za kuwa kinara wa vurugu zilizosababisha mkutano mkuu maalum wa chama hicho kuvunjika.

Mkutano huo ulifanyika katika Hotel ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba na wafuasi wake waliuvamia na kusababisha kuvunjika.

Wengine ni Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kaliua; Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini na Kambaya.

Uamuzi huo ulitangazwa rasmi Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, wakati akitoa taarifa ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT), kilichofanyika mjini Zanzibar mwezi uliopita.

No comments:

Powered by Blogger.