Kufuli zavunjwa, risasi zarindima CUF

RISASI za moto zimerindima katika Ofisi Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF) Buguruni, jijini Dar es Salaam leo mchana, wakati Prof. Ibrahim Lipumba alipowasili ili kuanza rasmi kazi baada ya kupokea barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayomtambua kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, 

Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, katika barua yake iliyoandikwa 23 Septemba mwaka huu, ameeleza kumtambua Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF na kwamba, viongozi wa CUF walioteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho 28 Agosti mwaka huu si halali.


Katika mapokezi yake, wafuasi wa Prof. Lipumba walijipanga kuanzia Barabara ya Buguruni (Rozana) inayoingia Ofisi Kuu za chama hicho na kuimba huku wakipuliza matarumbeta. Ilikuwa saa 7:00 mchana ambapo dakika ishirini na mbili baadaye kiongozi huyo alifika katika barabara hiyo akiwa katika gari aina ya Rav 4 yenye Na. T 639 AZK.

Baada ya wafuasi wake kumlaki, Prof. Lipumba alishuka na kuanza kutembea kwa mguu sambamba na wafuasi wake hadi ofisi za chama hicho zilizopo umbali wa takribani mita 300 kutoka barabarani hapo.

Wafausi hao walimsindikiza wakiimba nyimbo mbalimbali za chama hicho ikiwemo nyimbo yao maarufu, “Ooooh chamaaa… chama gani? Chama cha Wananchi CUF, Oooh chamaaa… chama gani? Chama cha Wananchi CUF.”

Walikutana na kundi lingine kubwa katika ofisi hiyo, hata hivyo geti la lango kuu lilikuwa limefungwa hivyo Prof. Lipumba alishindwa kuingia.

Baada ya kupita dakika tano tangu kuwasili Prof. Lipumba katika eneo hilo, zaidi ya wafuasi wake 20 waliparamia ukuta na kuingia ndani ya ofisi hiyo kisha kuwakabili walinzi waliokuwa wamefunga geti hilo na kisha walilivunja.

Baada ya walinzi kuzidiwa nguvu, walikimbia kwa kuruka ukuta na kudondokea nyumba za jirani na kutokomea, mmoja wa walinzi hao alinyang’anywa bunduki na wafuasi hao. Baada ya kuvunjwa kufuli la geti la lango kuu, Prof. Lipumba na kundi kubwa la wafuasi wake waliingia ndani huku wakishangilia.

Wakati hayo yakitendeka, polisi walikuwa nje ya ukuta wa ofisi hiyo ndani ya gari lao lenye namba PT 3699 wakiwa na silaha za moto. walikuwa watulivu ndani ya gari hiyo bila kuchukua hatua zozote. Baada ya muda mchache gari nyingine ya polisi yenye Na. T 709 ASF iliwasili ili kuongeza ulinzi.

Mara baada ya Prof. Lipumba kuingia ndani, polisi nao waliingia ndani kwa lengo la kuichukua bunduki iliyokuwa mikononi mwa wafuasi wa Lipumba. Wakati huo risasi za moto zilipigwa hewani kutokana na sintofahamu iliyokuwepo eneo hilo.

Hata hivyo, Prof. Lipumba hakuweza kuingia ndani ya ofisi kutokana na mlango wa kuingia ndani kufungwa, wafuasi waliamua kuvunja kufuli kwa nguvu chini ya usimamizi wa polisi na hatimaye aliingia ndani.

Mkuu wa askari hao aliokuwa amevaa kiraia sambamba na mwingine mwenye jina MADALI S.B walishuhudia tukio hilo, katika hali ya kushangaza askari aliyevalia kirai aliyeonekana kuwa kiongozi w polisi hao, alitishia kuvunja kamera za wandishi wa habari watakaompiga picha.

Prof. Lipumba aliingia ndani ya ofisi yake na kuzungumza na waandishi wa habari akisema, “nimerejea kazini na nawasihi wana CUF wawe wamoja, wasahau yaliyopita tukijenge chama chetu.”

Lipumba aliongea kwa muda mfupi na waaandishi hao kabla ya kutoka nje kuzungumza na wafuasi wake, ambapo amewatahadharisha viongozi wa muda waliowekwa na kikao cha baraza kuu la chama hicho 28 Agosti mwaka huu kukaa mbali na shughuli za chama hicho.

Lipumba amesema, “Nataka kujenga chama kitakachoenea kila mahali si chama cha upande mmoja tu, sina tatizo na viongozi wa CUF waliochaguliwa na wanachama katika uchaguzi mkuu.”

Pof. Lipumba aliwaaga wanachama wake na kuwasihi kumpa ushirikiano ili aweze kukijenga chama hicho. Hata hivyo katika hali ya kushangaza gari yake aliyokuja nayo Na. T 639 AZK iligoma kuwaka nay eye kushindwa kuondoka katika eneo hilo.

Tukio hilo lilitokea saa nane na dakika arobaini mchana (8:40) na ilimlazimu Prof. Lipumba kukaa kwa zaidi ya dakika 10 gari hilo liweze kuwashwa, lakini halikuweza kuwaka na hivyo kulazimika kupanda gari linguine Na. T 581 CJU ambalo lilikuwepo katika eneo hilo.

Haikujulikana mara moja gari hiyo ni mali ya nani, Prof. Lipumba aliondoka katika eneo hilo huku ndani ya gari hiyo akiwa ameambatana na watu wengine wanne na magari matatu yenye askari polisi yakimsindikiza nyumba.

Magari yaliyomsindikiza nyuma wakati Prof. Lipumba akiondoka katika eneo la ofisi kuu za  CUF, Buguruni  majira ya saa nane na dakika hamsini (8:50) ni pamoja na lile lenye namba za usajili PT 3891, PT 3699 na T 709 ASF.

Hata hivyo taarifa ambazo MwanaHALISI online imezipata, zinaeleza kwamba gari hizo za polisi zilienda kumzuia Prof. Lipumba katika eneo la barabara kuu na kumtaka afike Kituo cha Polisi Buguruni kwa mahojiano ambapo alitii na kuhojiwa kabla ya kuachiwa.

Hivi punde tutakuletea kwa kirefu kile alichoongea Prof. Lipumba mbele ya wafuasi wake.

No comments:

Powered by Blogger.