Lipumba arejeshwa uenyekiti CUF
PROFESA Ibrahim Lipumba, aliyetangazwa kusimamishwa uanachama na Chama cha Wananchi (CUF), ametangazwa kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho,
Taarifa ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliyotolewa jana na kusambazwa leo imeeleza kuwa, Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti wa chama hicho kwa mujibu wa taratibu.
“Baada ya upembuzi wangu ni kuwa, Lipumba bado mwenyekiti halali wa CUF na waliofukuzwa, kusimamishwa ni wanachama halali.
“Viongozi ambao uamuzi wao uliathirika na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa bado ni viongozi halali wa CUF,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa Jaji Francies Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Prof. Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho Agosti mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na ujio wa Edward Lowassa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katika Ofisi Kuu ya chama hicho iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, wafuasi wa Prof. Lipumba mchana huu wamefurika wakimsubiri na kwamba, yupo njiani kwenda ‘ofisini kwake.’
Agosti mwaka huu CUF ilimsimamishwa uanachama Prof. Lipumba kwa tuhuma za kuwa kinara wa vurugu zilizosababisha mkutano mkuu maalum wa chama hicho kuvunjika.
Mkutano huo ulifanyika katika Hotel ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumbana wafuasi wake waliuvamia na kusababisha kuvunjika.
Pamoja naye katika adhabu hiyo ni viongozi waandamizi wengine 10 akiwemo Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kaliua; Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini na Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.
Uamuzi huo ulitangazwa rasmi Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, wakati akitoa taarifa ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT), kilichofanyika mjini Zanzibar mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wengine waliochukuliwa hatua hiyo hadi watakapojieleza mbele ya Baraza Kuu hilo, ni Ashura Mustafa, Omar Mhina Masoud, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Wakati Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na mwanamama aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama, Mnyaa na Kombo ni viongozi wazoefu waliokuwa wabunge kipindi cha 2010/2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.
No comments: