YANGA NA SIMBA ZIENDE MANUNGU NA MABATINI ILI KUENDELEZA DHANA YA MPIRA NI MCHEZO WA KIUNGWANA!

Bolivia ni nchi iliyopo zaidi ya mita 3000 juu ya usawa bahari. Uwanja wao wa taifa, Estadio Hernando Siles, upo mita 3,637 juu ya usawa wa bahari.

Kisayansi, kadri unavyozidi kwenda juu ya usawa wa bahari, uwezo wa kupumua unapungua sana kutokana na mgandamizo (pressure) wa damu kuwa mdogo kwa sababu ya upungufu wa hewa safi ya oksijeni (the higher the altitude the lower the pressure).

Suala hili liliibua malalamiko makali kutoka kwa timu zilizokuwa zikienda kucheza nchini Bolivia na mwaka 2007, FIFA ikapiga marufuku mechi zake kufanyika kwenye viwanja vilivyopo katika maeneo ya zaidi ya mita 2500 juu ya usawa wa bahari (mfano ukiwa uwanja wa Hernando Siles).

Marufuku hii ikaamsha upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wakiongozwa na Rais wa nchi hiyo Evo Morales na gwiji wa Argentina, Diego Maradona, ambao walicheza mechi maalumu kwenye uwanja huo kuonesha kupinga kwao wakisema kila timu ina haki ya kufurahia ‘mchezo mzuri’ katika uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wao.

FIFA wakasikia kilio hicho na kuondoa marufuku hiyo na mpaka sasa uwanja huo unatumika. FIFA ilikubali kupingana na sayansi ya afya ili kuendeleza dhana ya ‘mpira ni mchezo wa kiungwana’ na kila timu inayo haki ya kuufurahia mchezo mzuri nyumbani kwake mbele ya mashabiki wake.

Hapa Tanzania, TFF na Bodi ya Ligi, wanatakiwa kupata somo kutoka FIFA na Bolivia. Kwenye ligi yetu, kuna baadhi ya timu haziruhusiwi kupata haki ya kufurahia ‘mchezo mzuri’ katika viwanja vyao vya nyumbani mbele ya mashabiki wao kwa sababu tu TFF na Bodi ya Ligi hazitaki kuwapatia haki hiyo.

Mwadui FC, Azam FC, Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting & JKT Ruvu na African Lyon (ambayo itatumia uwanja wa Karume) hazitopata haki hiyo zitakapokutana na Yanga na Simba.

Mamlaka za soka zinasema wakongwe hawa hawachezi kwenye viwanja hivyo kwa sababu za kiusalama. Eti timu hizi zina mashabiki wengi kiasi kwamba zikienda kwenye viwanja hivyo, kudhibiti usalama itakuwa ngumu.

Sababu hii ni nyepesi mno kwa kulinganisha na tishio la uhai wa watu kucheza kwenye viwanja vilivyopo sehemu za miinuko mikubwa. Itakumbukwa kikichomtokea Lionel Messi nchini Bolivia, alipotapika uwanjani baada ya kuzidiwa na uzito wa hewa.

Lakini FIFA kwa kupigania kulinda ile dhana ya mpira ni mchezo wa kiungwana, inaendelea kusisitiza kwamba lazima timu ziende La Paz, Bolivia.

Ni rahisi kudhibiti usalama kuliko kudhibiti uwezo wa kupumua. Kudhibiti usalama ni kuuza tiketi kulingana na uwezo uwanja husika. Kwa mfano, Azam Complex Chamazi ina uwezo wa kubeba watazamaji 7000, na ziuzwe tiketi hizo tu….watakaokosa tiketi wakae majumbani kwao wasubiri Azam TV.

Yanga na Simba hawaendi Mwadui. Yanga na Simba hawaendi Manungu. Yanga na Simba hawaendi Chamazi. Yanga na Simba hawaendi Mabatini. Yanga na Simba hawaendi Karume.

Hizi ni mechi tano ambazo hawakutani na mpinzani wao akiwa kwenye ngome yake halisi. Katika mizunguko miwili ya ligi maana yake ni mechi 10. Kati ya hizo, mechi sita zinafanyika kwenye ngome zao, uwanja wa taifa.

Mechi zote mbili dhidi ya Azam FC, Yanga na Simba wanacheza uwanja wa nyumbani, taifa.

Mechi zote nne dhidi ya Ruvu Shooting na JKT Ruvu, Yanga na Simba zinacheza katika uwanja wa nyumbani, taifa.

Pia mechi zote mbili dhidi ya African Lyon, Yanga na Simba zitacheza katika uwanja wao wa nyumbani, taifa.

Mpaka wanatangazwa mabingwa msimu uliopita, Yanga walitoka sare mechi mbili pekee kwenye uwanja wao wa nyumbani, taifa, nazo ni dhidi ya Azam FC ambazo kiufundi, mchezo mmoja ulikuwa wa ugenini. Lakini walitoka sare tatu ugenini; 0-0 vs Mgambo Tanga. 2-2 vs TZ Prisons Mbeya na 2-2 vs Mwadui Shinyanga. Pia walifungwa mechi moja dhidi ya Coastal Union Tanga.

Unaweza ukaona, Yanga walivyofaidika na uwanja wa nyumbani. Japo Simba kutokana na matatizo yao walipoteza mechi nyingi za nyumbani kuliko ugenini, lakini kiujumla, hakuna timu ambayo ingependa kucheza mechi zake igenini na kuacha nyumbani.

Kinachoshangaza ni kwamba miaka ya nyuma, Yanga na Simba zilienda kwenye viwanja vidogo na hakuna taarifa ya kukosekana kwa usalama iliyoripotiwa.

Mwaka 1998, wakati Yanga ikijiandaa kurudiana na Rayon Sport ya Rwanda kwenye mchezo wa raundi ya kwanza ya klabu bingwa Afrika, ilienda Manungu na kuifunga Mtibwa 4-0. Walicheza na hakuna kilichoharibika. Siku hizi tunakwama wapi?

Ili tumpate bingwa wa kweli, ni lazima kuwe na mazingira sawa ya ushindani. Timu zote zipitie mazingira ya aina moja katika safari ya kuutwaa ubingwa. Kama kutakuwa na utofauti, basi usiletwe na mazingira yaliyotengenezwa na mamlaka bali timu zenyewe

No comments:

Powered by Blogger.