Mufti Zubeiry aunda tume kuchunguza Bakwata
MUFTI wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar bin Zubeiry Ally ameunda tume ya watu wanane ya kuchunguza na kutoa taarifa kamili juu ya misamaha ya kodi na mikataba mbalimbali iliyoingiwa baina ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na watu mbalimbali nchi nzima.
Alitangaza kuunda tume hiyo jana na kuipa siku 90 na Shehe Abuubakar Khalid atakuwa Mwenyekiti wa tume hiyo inayojulikana kama ‘Tume ya Mufti wa Tanzania’ akisaidiwa na Shehe Issa Othman Issa.
Mufti amemteua Mwalimu Salim Ahmed Abeid kuwa Katibu wa Tume hiyo ambayo alisema ameiunda kwa mujibu wa Katiba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kipengele 82 (3) b.
Taarifa ya Mufti kwa vyombo vya habari jana iliwataja wajumbe wengine wanaounda tume hiyo ni pamoja na Shehe Khamisi Mataka, Ustaadh Tabu Kawambwa, Mwalimu Ally Abdallah Ally, Alhaji Omar Igge na Shehe Mohamed Khamis.
Alisema katika taarifa yake kuwa, tume hiyo itafanya kazi kwa kufuata hadidu za rejea saba ambazo ni pamoja na kufuatilia suala la misamaha ya kodi mbalimbali zilizoombwa na Bakwata na taasisi zake nchi nzima.
Aidha, Mufti ameitaka tume hiyo kufuatilia mikataba yote ya uuzwaji wa viwanja na mali mbalimbali za Bakwata na taasisi zake nchi nzima na kuona uhalali wa umiliki huo na kufuatilia mikataba ambayo Bakwata imeingia na wawekezaji na kuona kama ina maslahi na baraza au kinyume cha hivyo.
Pia tume hiyo imetakiwa kufuatilia mali zote za baraza na kuona hali ya usajili wa mali hizo, kufuatilia mapato na matumizi ya baraza na taasisi zake kisha ameitaka kupeleka taarifa na mapendekezo yake kwa mufti ndani ya siku 90 kuanzia jana.
Desemba mwaka jana, Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Zubery alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Utawala wa Bakwata, Karim Majaliwa ili kupisha uchunguzi juu ya kashfa ya magari 82 yaliyoombewa msamaha wa kodi pamoja na matumizi mabaya ya ofisi.
No comments: