Maalim Seif ahojiwa juu ya tuhuma za ufisadi


MAMLAKA ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imemhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuwahusisha baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tuhuma za ufisadi.

Ofisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma cha ZAECA, Abubakari Mohamed Lunda, alisema jana kuwa Maalim Seif alihojiwa na Mkurugenzi wa ZAEC, Mussa Haji Ali, ili athibitishe tuhuma hizo.

Lunda alisema tuhuma zilizotolewa dhidi ya watendaji na viongozi ni nzito ndiyo maana mamlaka hiyo imeamua kuchunguza ukweli wake kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

Lunda alisema kazi kubwa ya mamlaka hiyo ni kuchunguza jambo lolote ambalo linahusu maslahi ya Zanzibar katika kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi.

“Tayari mamlaka imemhoji Maalim Seif ili kutafuta ukweli juu ya tuhuma alizotoa za kuwapo viongozi wanaomiliki fedha chafu na mali nje ya nchi,” alieleza Lunda.

Alisema nia ya kumhoji Maalim Seif ilikuwa kupata ukweli wa tuhuma alizotoa dhidi ya viongozi na watendaji aliowatuhumu kwa kumiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.

Hata hivyo, Lunda alisema mpaka sasa hafahamu mkurugenzi amegundua kitu gani baada ya kufanyika kwa mahojiano hayo huku akisisitiza kuwa ZAECA imetimiza wajibu wake wa kupokea na kuchunguza taarifa mbalimbali wanazopata kupitia wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi.

Lunda pia alisema kuna majalada 20 yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Alisema majalada hayo yanahusisha kesi mbalimbali zikiwamo za rushwa ya uchaguzi zilizotokea wakati wa kura ya maoni ya kuwapata wagombea wa ubunge na uwakilishi kupitia CCM mwaka jana.

Alisema kitendo cha majalada kukaa muda mrefu kwa DPP bila ya kufunguliwa mashtaka mahakamani si jukumu la ZAECA kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

"Ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar (DPP),"alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari, Aprili 10 mwaka huu mjini Zanzibar, Maalim Seif, ambaye ni Makamu wa kwanza wa Rais wa zamani wa Zanzibar alituhumu kuna viongozi na watendaji wa visiwani humo wanamiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.

Alisema kuwa fedha hizo zilipatikana kwa njia za ufisadi na kutaka jumuiya ya kimataifa kufuatilia akaunti za vigogo hao na watendaji nje ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

Maalim Seif alidai kuwa haihitajiki tochi kuwamulika viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi na kutaka mamlaka za dola kufanya uchunguzi dhidi ya vigogo hao na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Powered by Blogger.