Rais Magufuli aitumbua Tanesco

magufuli_aapa
ais wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli anayesifika kwa utumbuaji wa majipu, safari hii ameifanya kazi hiyo kimyakimya, baada ya kuivunja Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Mighanda Manyahi, Risasi Mchanganyiko linathibitisha.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, bodi hiyo iliyokuwa na wajumbe wanane, ilivunjwa Machi 3, mwaka huu katika barua zilizosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Mhandishi Mussa Ibrahim Iyombe na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya bodi za mashirika mbalimbali ya serikali zilizovunjwa.
Bodi hiyo ya wakurugenzi iliyovunjwa, licha ya mwenyekiti wake Dk.  Manyahi ilikuwa na wajumbe ambao ni Dk. Haji Semboja (Makamu Mwenyekiti), Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Shaaban Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Nyamajeje Weggoro.
Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema ni kweli wamepewa barua za kutenguliwa kwa uteuzi wao, lakini anaamini Rais Magufuli hakupewa taarifa sahihi zilizosababisha kuchukua uamuzi huo.
“Rais anafanya kazi kwa kupewa information (maelezo), lakini nina wasiwasi baadhi ya wanaomsaidia huwa hawampi taarifa sahihi, bodi yetu haikuwa na sababu zozote za kuvunjwa, lakini hatuna cha kusema kwa sababu ameshachukua uamuzi na hakuna wa kuutengua,” alisema mjumbe huyo.
Gazeti hili liliwasiliana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ili kujua sababu za kuvunjwa kwa bodi hiyo na endapo yapo maagizo ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi dhidi ya wajumbe wa bodi hiyo.
Grayson Msigwa ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, alikiri kuchukuliwa kwa hatua hiyo, lakini akalitaka gazeti hili kuwasiliana na Tanesco kwa maelezo mengine yoyote ya ziada.
Risasi Mchanganyiko liliwasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba kuhusu suala hilo, ambaye alikiri kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo.
“Ni kweli bodi imevunjwa na jambo hili mbona limezungumzwa hata na Waziri (wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo), limetokea siku kadhaa zilizopita,” alijibu kwa kifupi mtendaji huyo.
Baadhi ya mashirika ya umma ambayo bodi zake zimevunjwa na rais wa awamu ya tano tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana ni Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Chanzo: GPL

No comments:

Powered by Blogger.