Profesa Ibrahim Lipumba Aibuka....Amtaka Rais Magufuli Atangaze Mshahara Na Marupurupu Yake

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
amemtaka Rais
John Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake, kwa kuwa amejivisha joho la
kuwa Rais wa wanyonge.
Profesa Lipumba amelieleza gazeti la Mwananchi kuwa Rais Magufuli
amejipambanua kuwa kiongozi anayeguswa na matatizo ya wanyonge, hapendi makuu,
anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha za umma,
lakini watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani
Profesa huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi, alirejea
mijadala mbalimbali iliyowahi kuibuliwa kuhusu mshahara wa Rais, ikiwamo ule
uliyowahi kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, wakati huo akiwa Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema kuwa Rais analipwa Sh32 milioni kwa mwezi.
Pia alirejea taarifa iliyochapishwa na Mwananchi, Julai 27, 2015,
iliyoandikwa kutoka katika mtandao wa African Review kuwa Rais mstaafu Jakaya
Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika kwa kupata mshahara mkubwa wa
dola za Marekani 192,000 kwa mwaka sawa na dola 16,000 kwa mwezi, ambayo ni
sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Hadi jana jioni, dola moja ya Marekani ilikuwa
sawa na Sh2,187.
“Taarifa ya Ikulu ilikanusha vikali habari zilizochapishwa na
Mwananchi. Ikulu ilieleza kuwa habari hizo siyo za kweli. Hata hivyo,
haikueleza mshahara wa Rais na marupurupu yake ni kiasi gani?
Pia, katika mjadala wa mshahara wa Rais, Naibu Spika wa Bunge
lililopita ambaye ndiye Spika wa sasa, Job Ndugai alinukuliwa akieleza kuwa
mshahara wa mtu ni siri yake.
Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa
Umma wa wakati huo, Celina Kombani (kwa sasa ni marehemu) alisema kuwa ni kosa
kutangaza mshahara wa Rais.
“…Kwa hivi sasa Rais Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake
na kama mapato yake ni Sh32 milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya
mapato hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua hii itaimarisha taswira
inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” amesema
Lipumba.
Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais
Magufuli aliwataka mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu wachangie Sh1
milioni katika mishahara yao kuchangia elimu.
Pia Rais alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wake na waziri mkuu
watachangia Sh6 milioni kila mmoja, ili zifike Sh100 milioni kusaidia
changamoto za elimu bure Mkoa wa Dar es Salaam.
Kutokana na tangazo hilo, Profesa Lipumba alisema, “Ikiwa Sh6
milioni zitakatwa katika mshahara wake wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na
ule wa makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya Sh6 milioni kwa mwezi.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania hayako wazi.
Watanzania hawajui kila mwezi Rais, Makamu wa Rais na viongozi wakuu wa
Serikali wanalipwa kiasi gani? Malipo ya wabunge pia hayako wazi?” alihoji.
Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Rais katika
masuala ya uchumi kati ya mwaka 1991 na 1993, alisema kwa kuwa Rais Magufuli
amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge, anawajibika kuwaeleza Watanzania
mshahara na marupurupu yake.
“Ikiwa mshahara ni mkubwa sana achukue hatua za kuupunguza kama
alivyofanya Mwalimu Nyerere mwaka 1965.”
Hata hivyo, alisema kifungu cha Katiba cha 43 (2) kinaeleza kuwa
mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais
atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli akitaka kupunguza mshahara
wake itabidi kwanza abadilishe kifungu hicho cha Katiba.
“Anaweza kujitolea mchango wa kudumu utakaokatwa kutoka kwenye
mshahara wake kusaidia sekta ya afya au elimu,”alisema.
Profesa Lipumba ambaye ni mshauri wa Benki ya Dunia (WB) na Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) katika masuala ya uchumi, alisema ili kuimarisha utawala
bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie mamlaka waliopewa kwa manufaa ya
Taifa.
“Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi na yaamuliwe na
kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka utaratibu ulio wazi wa kuamua mishahara
na marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais na makamu wake, mawaziri,
wabunge, majaji, makatibu wakuu na viongozi wengine,”alisema.
Alisema ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora, uwajibikaji na
uwazi wa viongozi wa umma kwa wananchi wanao waongoza.
“ Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge lililopita ulikuwa
Sh3.4 milioni kila mwezi.Pia mbunge alilipwa Sh8.2 milioni, nyingine kama posho
ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wake na dereva.
“Vile Vile, mbunge anapohudhuria kikao cha Bunge alilipwa posho ya
Sh80,000 za kujikimu, Sh50,000 za mafuta ya gari na Sh200,00 za kuhudhuria
kikao cha Bunge, jumla ni Sh330,000 kwa siku.
“Posho ya siku moja ya
mbunge ni zaidi ya mara mbili ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali kwa
mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara inakatwa kodi, marupurupu hayakatwi
kodi,”alisema.
No comments: