Mabango ya Lema yawa tatizo kwa ccm Arusha

By Filbert Rweyemamu na Mussa Juma,

Arusha. Mabango ya mgombea ubunge Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema yamezua kizazaa baada ya CCM kutaka yaondolewe.
Mabango hayo yenye sura ya Lema yanayosomeka: “Nyie siyo Wapumbavu, Nyie siyo Malofa, Nyie ni wana wa Mungu, sisi tunawapenda, Lema tena 2015,” yamebandikwa katika miti, kuta za nyumba na maduka na mengi yako katikati ya Jiji la Arusha.
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Feruz Banno alidai jana kuwa mabango hayo yana lugha ya uchochezi, hivyo, wanaandika barua ya kumwomba msimamizi wa uchaguzi atoe amri yaondoshwe.
Akizungumzia sakata hilo, Lema alisema Rais mstaafu Benjamin Mkapa ndiye aliwaita Watanzania wanaotaka ukombozi kuwa malofa na wapumbavu.
“Mimi nikiwa mbunge wao na mgombea kwa mara nyingine, ninawapenda sana wananchi wangu, ujumbe huo una lengo la kuwatia moyo tu na siyo uchochezi,” alisema Lema.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wa Arusha, Juma Idd alisema bado hajapokea barua hiyo ya malalamiko kutoka CCM.
“Kama wataileta tutatazama wanacholalamikia kama kina mantiki,” alisema Idd.
Wakati huohuo, Lema amemsihi Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa kurejea ofisini kuendelea na majukumu yake kwani muda aliopumzika unatosha.
Lema alitoa wito huo wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi jimboni Karatu uliofanyika katika Uwanja wa Mbowe.
“Nakuomba sana Dk Slaa urudi tufanye kazi, heshima ya Chadema iliyonayo sasa, wewe una mchango mkubwa na hakuna sehemu ya nchi hii ambayo hujafika ili kuhakikisha wananchi wanapata mabadiliko ya kweli, kama mapumziko yanatosha,” alisema Lema.
Alisema licha ya wito wa kumtaka Dk Slaa arejee ofisini kutolewa na watu kadhaa, bado kuna kundi dogo la watu lisilotaka kiongozi huyo arudi kwenye nafasi yake hiyo baada ya sintofahamu iliyotokea kutokana na ujio wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na baadaye kuteuliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.
Lema aliwaambia wakazi hao kuwa katika mchakato wa Lowassa kuhamia Chadema, Dk Slaa alishiriki kikamilifu tofauti na inavyozungumzwa na baadhi ya watu. “Nawaomba ninyi wananchi ambao Dk Slaa alikuwa mbunge wenu wa kwanza baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini, mumsihi arudi ofisini tuendeleze mapambano ya kuwakomboa Watanzania,” alisema Lema.
Mbunge wa Viti Maalumu aliyemaliza muda wake, Cecilia Paresso aliiponda kauli iliyotolewa na mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan kuwa watajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Karatu hadi Mbulu.
Paresso alisema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kujenga barabara hiyo hata kwa kilometa mbili tu, zilizopo Mbulu Mjini kwa kipindi chote cha miaka mitano.
-chanzo: mwananchi

No comments:

Powered by Blogger.