Kigaila kuivunja CDA,Dr Lwaitama ajiunga chadema

Dk. Ezaveli Lwaitama
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Dodoma Mjini, kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila amewahakikishia wananchi
wa Dodomakuwa iwapo watamchagua kuwa mbunge wakazi hao watakuwa na uhuru wa kumiliki ardhi tofauti na ilivyo sasa.
Kigaila alitoa kauli hiyo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge kwa jimbo la Dodoma Mjini ambayo iliwajumuisha wagombea wote wa ubunge na udiwani katika mkoa wa Dodoma wenye majimbo kumi ya uchaguzi.Akizungumza na umati wa wakazi wa mji wa Dodoma katika viwanja vya Barafu, Kigaila amesema wakazi wa Dodoma wamekuwa watumwa katika maeneo yao kwa kuporwa viwanja vyao na mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
“Nataka wananchi wa Dodoma kuhakikisha mnaondokana na utumwa wa kuporwa maeneo yenu ambayo mlikuwa mnayamiliki kihalali kwa muda mrefu.
“Hapa mtaona wazi kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imewageuza wananchi wa Dodoma kama watumwa, haiwezekani kuona mtu tangu siku nyingi anamiliki mashamba au kiwanja lakini eti CDA imekuwa ikiwapora viwanja hivyo na kuwauzia kwa bei kubwa,” anasema Kigaila.
Mbali na kuwepo kwa kero ya ardhi katika mji wa Dodoma Kigaila amesema kuna tatizo kubwa ambalo linawakumba wafanyabiashara kwa kutozwa kodi nyingi ambazo hazipo kisheria.
Amesema wafanyabiashara kwa sasa wamegeuzwa mitaji ya serikali kwa kuwatoza faini ambazo si halali jambo ambalo ni kuwakwamisha katika kujikomboa kiuchumi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema Taifa (BAWACHA), Kunti Majara amesema sasa yatosha Dodoma kuendelea kuwa koloni la CCM.
Amesema Dodoma kuna changamoto nyingi hivyo kunatakiwa kuwepo kwa mbunge makini na mwenye uwezo wa kujenga hoja bungeni na si vinginevyo.
“Bungeni hatutaki mtu ambaye anaenda kuvaa nguo za vitenge na kufanya ubishoo, tunataka mtu ambaye ni makini na mwenye uchungu wa kuwatetea wananchi na siyo kwenda kuuza sura,” amesema
Katika hatua nyingine chama hicho kimemkabidhi kadi ya uanachama pamoja na katiba ya chama hicho, Dk. Azaveli Lwaitama ambaye amesema kujiunga kwake kutamfanya aendelee na harakati za ukombozi kwa wananchi malofa na wapumbavu.
Dk. Lwaitama ambaye ni mwalimu mkongwe katika vyuo vikuu amesema yeye tangu mwaka 1976 alikuwa ni mwanachama mfu wa CCM kutokana na kutolipia kadi yake jambo ambalo amesema ni kutokana na kuwa na chama ambacho ni cha ukandamizaji.
Akizungumzaia kuhusu rais wa UKAWA, Edward Lowassa, amesema mgombea huyo ndiye anayefaa kushika nchi kutokana na uwezo wake wa kufanya kazi kwa umakini zaidi.
-mwanahalisi online

No comments:

Powered by Blogger.