Maalim Seif azindua safari ya Urais


MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema endapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, atahakikisha anaurudisha bungeni mchakato wa Rasimu ya Katiba. Kwa Maalim Seif, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa tano kwake kuwania urais, kwani alichawania katika chaguzi nne zilizopita, ingawa kura zake hazikutosha mbele ya wagombea wa CCM.
Alianza mwaka 1995 akashindwa mbele ya Dk Salmin Amour, mwaka 2000 akaangushwa na Amani Abeid Karume kama ilivyokuwa mwaka 2005 kabla ya mwaka 2010 kuzidiwa kura na Rais anayemaliza muda wake, aliyepitishwa tena na CCM kuwania nafasi hiyo, Dk Ali Mohammed Shein.
Akizungumza kwa kujiamini wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu kwenye Uwanja wa Kibandamaiti mjini hapa jana, alisema atashirikiana na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kurudisha mchakato wa Katiba kwa lengo la Zanzibar kuwa na mamlaka kamili.
Akifafanua, alisema katika muundo wa muungano uliopo sasa, Zanzibar haina fursa za kiuchumi, akidai imebanwa katika sekta mbalimbali.
“Wananchi mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, nitahakikisha mchakato wa rasimu ya Katiba inarudishwa tena bungeni kwani rasimu ile ilitekwa,” alisema.
Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni ambao ulihudhuriwa na Lowassa, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema licha ya kuwepo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa bado Wazanzibari hawajanufaika na serikali hiyo.
Alitoa mfano kuwa akishika madaraka atahakikisha anaunda wizara ya mafuta na gesi katika kipindi cha siku 100 za kwanza za utawala wake huku sera na sheria ikipatikana.
“Hiyo ndiyo mikakati yangu, nataka kuona mabadiliko ya kweli yanapatikana kwa wananchi wetu,” alisema katika mkutano huo ambao Lowassa alisalimia kwa dakika tatu na kuwasilisha kwa wananchi wa Zanzibar kilio chake, akidai wapinzani wao wanachana mabango na kuyatupa porini.
Lowassa alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi hao, wawapigie kura yeye na Maalim Seif, huku akisisitiza `ushindi’ upo.
Wakati CUF wakizindua kampeni zake jana, Jumapili itakuwa zamu ya CCM ambayo mgombea wake, Dk Shein, amesema hana shaka ya ushindi kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, iliyochochea ustawi wa maendeleo ya Zanzibar

2 comments:

Powered by Blogger.