JB: Awachanganya wasamabazaji wawili wa filamu mmoja achachamaaa
Hakika simulizi hii ya maisha ya JB, inabadilisha mtazamo wa watu wengi juu ya maisha. Waliokuwa wamekata tamaa, wamepata matumaini mapya. Wametiwa moyo na jinsi ambavyo msanii huyu ameweza kupambana na maisha hadi kufika mahali alipo sasa.
Mateso, maumivu, dhoruba na mikikimikiki ambayo JB amekutana nayo katika safari ya maisha, imekuwa somo kubwa kwa wengi. Nimekuwa nikipokea simu na meseji nyingi sana kutoka kwa wasomaji, wakieleza jinsi na namna ambavyo simulizi hii ya maisha ya JB imeweza kubadili fikra zao.
Msomaji, endelea kufuatilia simulizi hii tamu yenye mafunzo mengi, hakika hutabaki kama ulivyo, juhudi zako za kufuatilia ndoto ulizonazo maishani, zitakufikisha kwenye maisha ambayo unatamani kuishi, ni suala la kupambana tu.
Wiki iliyopita, tuliishia pale msanii Vincent Kigosi ‘Ray’ amemfuata na kumpa wazo la kubadili msambazaji. Yaani kuachana na Kampuni ya Wananchi Store, ili ajiunge na Steps Entertainment. Jambo ambalo linampa wakati mgumu sana kuamua. Hata hivyo, anaingia tamaa mbaya ya fedha, akashindwa kuachana na Kampuni ya Wananchi, pia akawa hayuko tayari kuacha ‘dili’ la Steps limpite kushoto. Hapo ndipo anaamua kucheza mchezo mbaya na wa hatari zaidi.Je, ni mchezo gani huo? Atafanikiwa? Nini kitafuata? Banana nayo hapa chini sasa.
“Sijawahi kuwa na wakati mgumu maishani mwangu kama kipindi hicho, niliyumba na kukosa msimamo na unajua ni kwa nini mdogo wangu?,” anasema na kunisogelea kwa ukaribu zaidi huku akinikazia macho.
“Mmh,” naishia kuguna na kuikamata vyema kalamu yangu ili inidondoshee vyema wino.
“Mmh,” naishia kuguna na kuikamata vyema kalamu yangu ili inidondoshee vyema wino.
“Kila binadamu ana kitu kinaitwa sensor, yaani kitendo cha kusutwa na nafsi, sikuwahi kugombana na Farhaji yule wa Mwananchi Store, alikuwa mshauri wangu mkubwa sana, sasa naanzaje kuachana naye? Ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwangu,” anasema JB huku akipiga mwayo wa kivivu.
“Tena nimekumbuka jambo, hivi unajua mimi ndiye msanii wa kwanza kabisa kutengeneza sinema yenye sehemu ya kwanza na ya pili?,” anasema JB kwa mtindo wa kuhoji.“Hapana, sijui,” nakataa kwa staili ya kutingisha kichwa.
“Sinema ya kwanza kuwa na sehemu mbili, yaani Part One na Two, ilikuwa ni Stranger, kifupi ni Farhaji huyohuyo wa Wananchi, alinishauri juu ya kutengeneza faida zaidi kwa kuikata filamu moja kwenye vipande viwili, naanzaje sasa kuachana naye?, dhamira ikazidi kuniuma sana,” anasema.
“Wakati huohuo, tayari utamu wa pesa ulikuwa umeninogea sana, sikutaka kabisa kuachana na dili la Steps, kwa hiyo nikabaki njia panda, kwamba niachane na Farhaji au niendelee naye?,” anasema.“Nikawazaa nikawazaaaa, nikawaza weee, hatimaye nikapata wazo la kucheza mchezo ambao niliamini ungefaa sana,” anasema JB.
“Mchezo wenyewe ni hivi, nilitengeneza filamu mbili za Wakti na Signature, ambapo moja nikaipeleka Wananchi Store na nyingine nikaipeleka Steps, sikuwa na jinsi bwana,” anasema huku akisindikiza maneno hayo kwa kicheko cha sauti ya juu huku akikunja ndita.
“Mchezo wenyewe ni hivi, nilitengeneza filamu mbili za Wakti na Signature, ambapo moja nikaipeleka Wananchi Store na nyingine nikaipeleka Steps, sikuwa na jinsi bwana,” anasema huku akisindikiza maneno hayo kwa kicheko cha sauti ya juu huku akikunja ndita.
“Basi, kilichotokea, sinema zote mbili zikatoka siku moja, yaani Steps waliitoa Signature na Wananchi Store wakaitoa Wakti, sasa niambie balaa la siku hiyo, mbona nilikoma mwenyewe,” anasema JB kwa sauti ya juu huku akinipigapiga begani kama ishara ya msisitizo na hamasa zaidi.
“Steps walichukizwa sana na kitendo hicho, kwani ile ya Wakti iliuza mno kuliko ile ambayo walisambaza wao, wakaamua kukaa mezani na mimi, ili tukubaliane mkataba wa kutengeneza sinema zao tu,” anasema.
“Tukakaa na kukubaliana kuwa niwe chini yao, nikawa nimeachana kabisa na Farhaji, japo iliniuma lakini sikuwa na jinsi kwa sababu nilikuwa nimetengewa ‘fungu’ la kutosha, ni kipindi hicho ndipo kazi ya uigizaji inaanza kuwa ya maslahi tofauti na zamani ambapo tulifanya kama hobby tu,” anasema.
“Nikawa nimeungana na Ray pamoja na wasanii wengine wakubwa, kuwa chini ya Steps, lakini wakati mambo yakiwa ndiyo yameanza, ghafla nikapata wazo lingine tena, japo nilijua lingewashangaza wengi, lakini niliamini lilikuwa sahihi, safari ya kutafuta fedha, ndiyo kwanza ilikuwa imekolea ubongoni mwangu, sikuwa na mchezo kabisa lilipokuja suala la fedha, hata sasa niko hivyo,” anasema JB
No comments: