Wakala_wa_Shetani -6..



KWA TAARIFA ZAIDI NICHEKI HAPA 0785848566 
ILIPOISHIA;
Wazo alilokuwa nalo lilikuwa ni kukiulia mbali kile kitoto na kumweleza mkewe kuwa kilindondokea kwenye maji.
Lakini aliamini mkewe hawezi kumwamini hasa baada ya kutaka kumuua mara ya kwanza.
Alijua chochote kibaya hata kama cha bahati mbaya kitaonekana ni cha makusudi.
SASA ENDELEA...
Hali ya kusimama kwa muda mrefu huku akimbeba mtoto bila sehemu ya kukaa ilimte sa sana. Kutokana na kujaa maji na matope kila sehemu, hakukuwa na sehemu ya kumweka mtoto ili apumzike. Aliona mateso yale yalikuwa ni ya kujitakia, aliamini hakukuw na haja ya kuteseka kama wangemuulia mbali yule mtoto.
Baridi lilikuwa kali mpaka likaanza kumwingia tumboni na kuzidi kumweka kwenye wakati mgumu. Kuna wakati alichoka sana na kuamua kutafuta sehemu yenye mwinuko kidogo na kukaa ndani ya maji.
Kila mateso yalivyozidi kumpata alizidi kumchukia yule mtoto na kufikia kuwaza kwenda kwa siri kwa wana kijiji kuwaeleza habari za mkewe kujifungua mtoto Albino ili achukuliwe na kuuawa.
Aliamini ile ndiyo njia itakayowafanya waishi maisha ya amani. Pamoja na kuyawaza yote, bado aliamini mkewe lazima atamfikiria vibaya. Alijuta kutoa wazo la kumuua yule mtoto, aliamini kama angekaa kimya mkewe asingejua mpango wake, hivyo, ingemrahisishia kutimiza dhamira yake bila mkewe kujua.
Kilichomchanganya zaidi akiwa katikati ya dimbwi la mawazo, mtoto alianza kulia tena kwa sauti ya juu. Wasiwasi wake mkubwa kama atatokea mpita njia lazima angemsikia na kusogea. Alijitahidi kumbembeleza lakini mtoto aliendelea kulia. 
Alijiuliza mkewe kachelewa wapi au njia imefunga kutokana na maji kuwa mengi, alipata wazo la kumfuata mkewe akiwa na mtoto wao na mengine yangejulikana hukohuko. 
***
Wakati mama Sabina akimtafakari Ng’wana Bupilipili na mumewe, juu ya mabadiliko alioyaona juu yake.
Pia, mumewe na mawazo mabaya kwa mtoto wao. Ngw’ana Bupilipili alikuwa njiani kurudi shamba alipomuacha mumewe na mtoto. Ilibidi apite njia ileile ya kuingia ndani ya mito na vidimbwi vya maji ambavyo vilikuwa havikwepeki.
Alishangaa kukutana na mumewe njiani, ile ilimshtua na kumuuliza.
“Vipi mbona huku unakwenda wapi?”
“Nilikuwa nanyoosha miguu kidogo kukaa sehemu moja nilichoka,” Mathayo alidanganya.
“Mume wangu unakuja huku watu wakimuona utanibebea mbeleko gani?” Ngw’ana Bupilipili alimlalamikia mumewe.
“Mke wangu nisingefika mbali.”
“Mmh! Sawa, vipi ameanza kulia muda mrefu?”
“Si mrefu sana lakini nilichanganyikiwa nashukuru umerudi haraka, sijui ungechelewa ningemfanyaje?”
“Inawezeka amekojoa,” Ngw’ana Bupilipili alisema huku akimchukua mwanaye, mwili wote ukiwa umetoka maji na kuhisi baridi kali.
Alimpakata mwanaye na kuanza kumnyonyesha, hapakuwa na sehemu ya kukaa kutokana na kila kona kujaa maji. Yalikuwa nki mateso mazito sana katika maisha yao.
Walikubaliana kurudi nyumbani kiza kikiingia ili kumpeleka mtoto kwenye joto kwa kuogopa mtoto kupatwa na ugonjwa wa Nimonia.
Waliendelea kuvumilia kukaa kule shamba pamoja na baridi kali pia wingu zito likitanda tena kuonesha mvua ingeteremka tena wakati wowote.
Ng’wana Bupilipili alimuomba Mungu kwa kila lugha aliyoifahamu ili mvua isishuke kwa kuamini lazima mtoto wao watampoteza kwa baridi au kufa maji. Alijua kama mvua itanyesha muda ule lazima hata maisha yao yatakuwa mashakani kwa kushindwa kuona sehemu watakayojificha kutokana na kiza kilichoanza kutanda tena.
Baridi lilizidi kuwa kali huku wakimkumbatia mtoto wao kwa kumweka kati ili apate joto la wazazi wake, kutokana na ubaridi kuwa mkali na sehemu ya kukaa haikuwepo, ilikuwa ni adhabu kubwa sana kwao kusimama kwa muda mrefu bila kukaa huku wakipokezana kumbeba mtoto.
***
Usiku uliingia wakiuona huku wakiwa hoi kama wapo kwenye adhabu. Mathayo bado aliamini ule ni mkosi kutokana na kukiuka masharti ya kumficha yule mtoto Albino. Lakini aliogopa kumweleza mkewe kwa kuamini hatakubaliana na chochote atakachomweleza.
Kiza kilipoingia waliongozana na mtoto wao huku wakitetemeka kurudi kijijini kwa kuingia kwenye vidimbwi vya maji kuna kipindi walipita kwenye maji yaliyowafikia vifuani.
Ilikuwa adhabu kubwa kama ingekuwa amri ya Mathayo angemtupa mtoto ili afie mbali na yeye kurudi kijijini bila hata mshipa wa fahamu kumgonga kama amepoteza damu yake. Aliamini tabu yote ile isingewafika kama wangekubali kumtoa mtoto wao na kuuawa.
Wasiwasi wake kama kijiji kitajua kuwa mkewe amejifungua mtoto albino, basi wangetengwa pia kutozwa faini ya ng’ombe na kuchukuliwa sehemu ya shamba. Alimuona mkewe kama anataka kumitia kwenye umaskini kwa kunyang’anywa mali zake kwa ajili ya mtoto ambaye hata wakimficha lazima angeonekana tu, kwani lazima amgelia na sauti ingesikika kwa watu.
Walirudi nyumbani kwa taadhari kubwa huku mkono wa Ng’wana Bupilipili ukiwa hauchezi mbali na mdomo wa mtoto wake ili akitaka kulia amzibe mdomo asitoe sauti.
Walifanikiwa kuingia ndani kwao bila mtu yeyote kuwaona. Baada ya kuingia ndani waliwasha moto ambao waliuota na miili yao kupata joto kisha waliandaa chakula cha usiku.
Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa inakimbilia saa tatu usiku. Lakini ilionekana ni kama saa sita za usiku kutokana na kiza na wingu zito la mvua.
Baada ya kula walichemsha maji ya moto na kwenda kuoga kutokana na kushinda na kupita kwenye maji machafu. 
Kwa vile mtoto alikuwa amelala baada ya kunyonya na kushiba. Walikwenda kuoga kwa pamoja, wakiwa wanaoga mtoto alianza kulia na kutoa sauti ambayo kutokana na utulivu wa usiku ilifika mbali.
Ngw’ana Bupilipili aliposikia sauti ya mtoto aliacha kuoga hata bila kukumbuka nguo alitoka mbio kuwahi kumnyamazisha. Kwa vile ilikuwa kiza hakuna ambaye alimuona ametoka bila nguo.
Alipofika alimbeba mtoto wake na kuanza kumnyonyesha huku akimbembeleza, ilionekana alikuwa amejikojolea na kutokana na hali ya baridi ilimfanya alie. 
Baada ya kunyonya na kumbadili nguo alinyamaza na kupitiwa tena na usingizi.
Baada ya kumlaza alirudi bafuni na kumalizia kuoga, wakati huo mumewe alikuwa ameishamaliza kuoga na kukaa na mtoto.
****
Mama Sabina usiku ule alikuwa akiangalia mifugo kabla ya kulala, alisikia sauti ya mtoto akilia, lakini hakuwa na uhakika inatoka wapi.
Sauti ilimjulisha ni mtoto mchanga na eneo lile hakukuwepo na mtoto mchanga. Baada ya kuhakikisha mifugo ipo tayari alirudi ndani ambako mumewe alikuwa amekwishatangulia kitandani.
“Mume wangu nimesikia sauti ya mtoto mchanga akilia,” alisema huku akirudisha mlango kabla ya kupanda kitandani.
“Mtoto mchanga?” mumewe alishtuka huku akigeuka.
”Eeh.”
“Sasa tatizo nini?”
”Unajua hapa kitongojini kwetu aliyekuwa na ujauzito wa kujifungua ni mke wa Mathayo Ngw’ana Bupilpili.”
Itaendelea

No comments:

Powered by Blogger.