Vigigo hawa kun`goka kikao cha CCM
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM inakutana leo huku kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” ikitarajiwa kutawala kikao hicho cha kwanza kwa mwenyekiti John Magufuli, ambaye ameonyesha dalili za kufumua sekretarieti wakati huu wa kuelekea uchaguzi wake mkuu.
Kikao hicho cha siku mbili kitachofuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa, pia kinatarajiwa kujadili mambo mengine nyeti, kama maandalizi ya uchaguzi utakaofanyika mwakani kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa kwa kuchagua kamati Kuu mpya na suala la uchaguzi wa meya wa Kigamboni ambayo sasa ni wilaya.
Pia kikao hicho kinatarajiwa kujadili chaguzi ndogo za mbunge wa Dimani na madiwani pamoja na ripoti ya wasaliti ambayo Magufuli alikabidhiwa na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete Julai 23 baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti.
Suala jingine linalotarajiwa kuchukua nafasi ni hali ya kisiasa nchini, ikijumuisha suala la Zanzibar, upigaji marufuku mikutano ya hadhara, hali ya kiuchumi ambayo inalalamikiwa na watu wa kada tofauti wakiwemo wafanyabiashara, wananchi na wabunge ambao walidiriki kuomba ushirikiano na wapinzani wakati wa Bunge la Bajeti kumshinikiza Waziri wa Fedha na Mipango arekebishe mwenendo wa uchumi.
Kutokana na jukumu la Kamati Kuu kuwa ni kuandaa ajenda za kikao cha Halmashauri Kuu, masuala hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye chombo hicho cha pili kwa ukubwa kwa ajili ya maamuzi.
Lakini mabadiliko ambayo yanaonekana ni bayana ni ya sekretarieti.
Rais Magufuli, ambaye alikabidhiwa nafasi ya uenyekiti baada ya kupata kura zote 2,398 za wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, amekuwa akiteua wajumbe wa sekretarieti kushika nafasi kadhaa, hali inayomaanisha kuwa anaweza kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wajumbe wapya.
Mabadiliko ya kiuongozi yanayotarajiwa ni kusuka upya sekretarieti inayoongozwa na katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye anasifika kwa kukipa nguvu chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kinana, aliyeshikilia nafasi hiyo tangu mwaka 2012, aliomba kujiuzulu pamoja na sekretarieti nzima baada ya Rais Magufuli kuchaguliwa kuwa mwenyekiti Julai mwaka huu, lakini Rais akakataa ombi lake.
Kwa kuwa Kinana ameshaonyesha nia ya kutaka kuachia ngazi, kuna uwezekano mkubwa wa mwenyekiti kuwasilisha pendekezo la jina la kada atakayeendana na kasi ya “Hapa kazi Tu” kumbadili mwanasiasa huyo mkongwe.
Hata hivyo, uwezekano mkubwa ni Kinana kuendelea na nafasi yake mpaka Uchaguzi Mkuu wa CCM mwakani.
Kutokana na msimamo wa Rais kuwa hawezi kumpa mtu mmoja nafasi mbili, ni dhahiri kuwa nafasi ya aliyekuwa katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye itatakiwa kujazwa baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari.
Kutokana na uteuzi wa Nape, CCM ilimteua Christopher Ole Sendeka kuwa msemaji wa chama, lakini sasa naye ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Njombe na hivyo nafasi yake sasa inakaimiwa na Selemani Mwenda.
Wengine walioondoka kwenye sekretarieti ni walioteuliwa kuwa mabalozi, ambao ni naibu katibu mkuu wa CCM-Bara, Rajab Omari Luhwavi na naibu katibu wa Halmashauri Kuu anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa, Dk Pindi Chana.
CCM inatarajiwa kupanga mikakati ya kuweka mgombea atakayeshinda kwenye uchaguzi wa meya wa wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa kuzingatia nguvu ya upinzani iliyopo.
Kwa sasa jiji la Dar es Salaam linaongozwa na Meya kutoka Chadema, Isaya Mwita, huku manispaa za Ilala na Ubungo zikiongozwa pia na mameya kutoka chama hicho.
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika hivi karibuni na kulalamikiwa na vyama vya upinzani, mgombea wa CCM Benjamin Sitta alishinda na kuwa meya wa Manispaa ya Kinondoni.
Jina la Edward Lowassa limekuwa likitawala vikao vya CCM tangu waziri huyo mkuu wa zamani aondoke chama hicho na kujiunga na upinzani mwaka jana. Hakuna shaka kwamba safari hii jina hilo litarudi wakati wajumbe watakapokuwa wakijadili ripoti ya wasaliti ambao wanasadikiwa kumuunga mkono Lowassa wakati wa uchaguzi.
Ripoti hizo ziliandaliwa kuanzia ngazi ya wilaya na baadaye kupatikana moja ambayo Kikwete alimkabidhi Magufuli Julai mwaka jana.
Mabadiliko hayaepukiki
Wakitoa maoni kuhusu kikao hicho cha kwanza kwa Rais Magufuli, baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema mabadiliko CCM hayaepukiki, lakini yanatakiwa yawe ya kimfumo. “Ninachotegemea ni kuona mabadiliko,” alisema kada mkongwe wa CCM, Njelu Kasaka.
“Kwanza tayari baadhi ya waliokuwa viongozi kwenye kamati kuu na sekretarieti wamepangiwa kazi nyingine, hivyo ni lazima azibe mapengo ili awe na chombo imara cha kufanyia kazi,” alisema.
Kuhusu utendaji mpya wa Rais Magufuli ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM, Kasaka alisema ili chama kiendelee kuwa hai lazima kifanye operesheni za hapa na pale.
“Mtu aliyekabidhiwa madaraka hayo lazima alete mabadiliko, lazima aweke watu watakaokiinua chama. Hawezi kubaki palepale alipokikuta. Kwa hiyo tutarajie kuona mikutano ya kukuza chama,” alisema waziri huyo wa zamani.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, mtindo wa utendaji wa Rais Magufuli serikalini, hautatofautiana na wa kwenye chama, hivyo lazima atafanya mabadiliko makubwa.
“Nadhani kutakuwa kuna mageuzi kwenye chama. Anataka kuona chama kwenye mtazamo mpya na anaweza kubadilisha muundo wa chama. Kwa mfano anaweza kupunguza muundo wenye watumishi wengi ili kubana matumizi,” alisema.
“Kuna matatizo ameyakuta kwenye chama kama vile watumishi kudai stahiki zao, lazima atayatatua na kwa kuwa sasa chama kimetoka kwenye uchaguzi kumekuwa na makundi, lazima ataleta suluhu ili chama kiwe kimoja.”
Kwa upande wake Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa alisema hakutakuwa na mabadiliko makubwa zaidi ya watu.
“Tusubiri tuone yatakayoamuliwa kwenye kikao hicho, lakini sitarajii makubwa maana wengine wameshaanza kutabiri mabadiliko kwenye kamati kuu. Anaweza kubadilisha watu, lakini mfumo ukabaki pale pale,” alisema Profesa Mpangala.
No comments: