Magufuli: Mliotaka kumkwamisha Dangote mtakiona

HATIMAYE Rais John Magufuli ameweka bayana ukweli kuhusu uwekezaji wa kiwanda cha saruji cha Dangote, mkoani Mtwara. Rais Magufuli amesema, ‘wapiga dili’ walitaka kujinufaisha kupitia mradi huo, lakini mbinu zao zimeshindwa na sasa waliotaka kuukwamisha watakiona cha moto.

Rais Magufuli amemuhakikishia mmiliki wa kiwanda hicho, Aliko Dangote kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na kumtaka mmiliki huyo kununua gesi moja kwa moja kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), badala ya kutumia watu wenye nia ya kutengeneza faida binafsi.

Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Dangote na kusema hakukuwa na tatizo lolote la kiserikali baina ya mwekezaji huyo, bali kulikuwa na watu waliotaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo.

“Hakuna tatizo lolote baina ya serikali na mmiliki wa kiwanda hiki, bali kulikuwa na watu waliotaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huu kwa kufanya biashara za ujanja ujanja jambo ambalo serikali haliruhusu, na tutawachukulia hatua wote,”alisema Rais Magufuli.

Alisema mradi huo uliingiliwa na wapiga dili wakiwemo wanasiasa na kusema serikali haitaruhusu michezo hiyo na kwamba mianya yao imefungwa na wote waliohusika kutaka kuuvuruga, watashughulikiwa na serikali.

Rais Magufuli alimueleza mmiliki huyo nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inatimiza malengo ya kuwa nchi ya viwanda na kuwa iwapo atataka maelezo yoyote au iwapo atakwamishwa ni vyema awasiliane na viongozi wa serikali badala ya kutumia watu ambao nia yao ni kutengeneza faida tu.

“Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mmiliki huyo alitaka eneo dogo kwa ajili ya kusafirishia saruji yake ila walijitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43, jambo ambalo halina uhalisia wowote bali ni watu wenye nia ya kutaka faida na kusema jambo hilo haliwezekani katika serikali yake.

Akizungumzia hilo la eneo, Rais alisema wapo watu waliosikia Dangote anataka kununua eneo hilo dogo kwa ajili ya kusafirisha saruji na wao wakakimbilia kununua maeneo hayo na kutaka wamuuzie kwa bei kubwa, jambo ambalo alisema halikubaliki hata kidogo.

Kuhusu gesi Rais alimtaka mmiliki huyo kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC kwa kuwa ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu wa kati ambao nia yao ni kutengeneza faida pekee na kusema kampuni iliyoingia kati kutaka kuwa kiunganishi wa kupata gesi kiwanda hicho, itafutiliwa mbali.

Kuhusu makaa ya mawe jasi (gypsum) Rais Magufuli alisema rasilimali hizo zipo hapa nchini na na kwamba nchi za Congo na Rwanda wananunua malighafi hizo hadi kwenye viwanda vyao na kwamba kiwanda cha Dangote kiko umbali wa kilomita mbili tu kutoka yaliko makaa hayo hivyo na makaa yenyewe ni bora na yanauzwa bei nafuu kuliko kuagiza kutoka nje.

Dangote alisema ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari vilivyoandika kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya Tanzania, jambo ambalo halina ukweli wowote.

“Nimeshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuandika nimefunga kiwanda kwa sababu nimekatazwa kuagiza makaa ya mawe na kutoka nje ya Tanzania, huu ni uzushi kwanza haiingiii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje,” alisema Dangote.

Katika kuthibitisha hilo, Dangote alisema tayari malori mapya 600 ameshaagiza na baadhi yako tayari bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusambazia saruji yake na pia lengo lake ni kuendelea kutengeneza ajira nyingine zaidi ya 1,500” Dangote alimhakikishia Rais Magufuli kuwa kabla ya Sikukuu ya Krismasi, magari yote 600 yatakuwa yamefika nchini na kusema hana mpango wa kufunga biashara zake nchini na badala yake ana mpango wa kufungua uwekezaji mwingine kwenye sekta nyingine kama kilimo.

Alisema yeye amekuja kutengeneza ajira nchini na amemuhakikishia rais kuwa atatumia malighafi kutoka nchini badala ya kuagiza nje kwa sababu kuagiza malighafi ni sawa na kuondoa uchumi wa nchi kuupeleka nje na kuingiza umaskini.

“Sitakuwa sehemu ya kuhamisha uchumi wa nchi hii, bali nitahakikisha natengeneza nafasi nyingi za ajira, nitatumia rasilimali za ndani makaa ya mawe na malighafi ‘clinker’ kwa maana zipo hapa hakuna sababu ya kuagiza nje”,alisisitiza Dangote.

Alimshukuru rais Magufuli kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kusema anaamini yuko mahali salama na ataendelea kuwekeza nchini kwa lengo la kunufaisha pande zote na kwamba nia yake ni kuendeleza Afrika kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli amuapisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole-Sendeka anayechukua nafasi ya Dk Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Wengine walioapishwa na Rais Magufuli ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (Kilimo), Dk Maria Sasabo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Dk Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Grace Alfred Martin kuwa Balozi (Mkuu wa Itifaki).

No comments:

Powered by Blogger.