Hadithi ya kusumisimua #Mimba_ya_Jini -9-

Hadithi ya kusumisimua #Mimba_ya_Jini -9-
Mtunzi: #Mzizi_Mkavu
ILIPOISHIA:.
“Nashukuru, lakini tatizo siyo kubwa?”
“Siyo kubwa, damu ndiyo iliyopotea nyingi, lakini jioni ya leo atakuwa vizuri.”
“Nashukuru dokta.”
Mustafa alitoka na kurudi nyumbani kufanya usafi wa damu iliyomtoka mkewe. Lakini alishtuka kukuta nyumba ipo katika hali ya usafi, hakukuwa na hata chembe ya damu.
SASA ENDELEA...
Hakutaka kuwaza sana aliwasha gari na kurudi kazini, alipofika alishtuka kukutana na manukato makali ambayo aliamini ni ya Shehna. Alipoingia tu Sara alimwambia.
“Bosi hukupishana na mwanamke mwenye hijabu hapo mlangoni?”
“Hapana.”
“Mmh! Kapitia wapi? Sasa hivi katoka.”
“Basi sijamuona.”
“Yaani sasa hivi hata dakika haijafika, nina imani hata getini hajafika.”
“Amesemaje?”
“Anashida na wewe.”
“Hakutaja jina lake?”
“Amesema ukifika niseme sijui Shena.”
“Shena au Shehna.”
“Shehna, unajua tena lafudhi ya Kimwambao.”
“Duh!” Mustafa alisema huku akigeuka na kukimbilia nje amuwahi mgeni wake.
Mpaka anafika getini hakumuona mtu yeyote, alimfuata mlinzi na kumuuliza.
“Shabani kuna mgeni amepita hapa?”
“Ndiyo.”
“Mwanamke au mwanaume?”
“Mwanamke aliyevaa hijabu.”
“Ameenda wapi?”
“Baada ya kutoka nje lilipita gari ambalo lilimchukua.”
“Duh! Yaani alipotoka tu gari lilipita?”
“Amesimama barabarani kama dakika mbili hivi akisubiri, baada ya muda gari lilisimama na yeye kuondoka.”
“Atakuwa ameenda wapi, kwa nini hakunisubiri?”
“Kwani bosi hukuonana naye?”
“Sikuonana naye.”
“Yaani mmepishana, baada ya wewe kuingia na yeye akatoka.”
“Mungu wangu sasa nimepishana naye wapi?” Mustafa alijilaumu kwani alikuwa ana hamu ya kumuona Shehna kwa macho baada ya kuvutiwa na sauti yake iliyomfanya aamini ni mwanamke mzuri.
“Yupo vipi?”
“Kwa kweli umbile kalificha na vazi alilovaa ni mweupe, kwa lafudhi yake anaonekana kama Mpemba vile. Ila yule mwana mke ana umbile la utata. ”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Toka anaingia na kutoka, upepo ulikuwa ukiisukuma nguo yake na kuonekana ramani ya umbile lake na kuonesha mwanamke mzuri sana. Kwani bosi hujawahi kuonana naye?”
“Sijawahi.”
“Mbona alivyokuuliza kama mnajuana sana?”
“Kwenye simu si kwa kuonana.”
“Labda atarudi.”
“Mmh! Sidhani.”
Mustafa aligeuka na kurudi ofisini, alipofika kwa msaidizi wake Sara alimuuliza.
“Vipi bosi umemuona?”
“Walaa.”
“Anapaa?”
“Hapana nimekuta ameisha panda gari na kuondoka.”
“Bosi nilipokueleza ungetoka ungemuwahi.”
“Labda atarudi.”
“Nina imani atarudi amekusuburi sana.”
“Sijui atarudi?”
“Yaani unatoka tu yeye akaingia kama mmepishana mlangoni, nilimweleza akuwahi akasema atakusubiri. Baada ya kuchoka alitaka kuondoka nilimsihi akusubiri, akakubali. Nilikutafuta kwenye simu lakini haukuwa hewani.”
“Mbona simu yangu sijazima?”
“Yaani kila nikipiga inakata.”
“Labda mawasiliano.”
Mustafa alipotaka kuingia ofisini Sara alikumbuka kitu.
“Bosi.”
“Unasemaje?”
“Ha...halafu mbona manukato ya yule mwanamke yanafanana na yale ya siku ile tuliyoyakuta ofisini kwako?”
“Hata mimi nayasikia, yupo vipi?”
“Kwa kweli sikumuona mwili mzima ila ni mrembo sana mrefu tena anayejijali sana.”
“Poa, akirudi nitamuona,” Mustafa alijibu huku akienda ofisini kwake.
Alipofika alikaa kwenye kiti na kutulia kwa muda kabla ya kuanza kazi, aliwaza kuhusu hali ya mke wake na yaliyomtokea.
Itaendelea SHARE ZIKIWA NYINGI NAPOST NYINGINE NOW

No comments:

Powered by Blogger.