JESSE WERE APIGA CHINI MILIONI 300 ZA YANGA

YANGA imemwajiri Kocha Mzambia, George Lwandamina ambaye alikuwa kocha mkuu wa Zesco huku kukiwa na taarifa ya kwamba anakuja na nyota kadhaa kutoka kwenye kikosi hicho na mmoja wao ni mshambuliaji Jesse Were raia wa Kenya ambaye inadaiwa Yanga wamemtengea kiasi cha Ksh 14 milioni ambayo ni takribani Sh 300 milioni ambazo amezitosa.

Baada ya kuwepo kwa taarifa hizo Were amefunguka na kuweka wazi kuwa hawezi kuja nchini kucheza ligi ya Tanzania kwani ligi hiyo si rafiki kwa wachezaji wa Kenya ambao baadhi yao wameshushwa viwango mara tu walipotua nchini.

Baadhi wa Wakenya walioshindwa kufanya vizuri ni Raphael Kiongera aliyeichezea Simba na Dan Sserunkuma ambaye ni raia wa Uganda ila makazi yake ni Kenya huku Donald Mosoti yeye akivunjiwa mkataba pasipokuwepo na makubaliano yoyote kosa ambalo lilifikishwa FIFA na Simba kuamuliwa kulipa Sh 64 milioni.

Yanga tayari wamefanya mazungumzo na mshambuliaji huyo na kumpa ofa nono lakini amegomea ofa hiyo na kwamba yupo tayari kwenda kucheza soka nchini Afrika Kusini na moja ya timu inayosemekana kuwania saini yake ni timu ya Free States hivyo Yanga hajaipa kipaumbele.

Katika mahojiano mbalimbali na mitandao ya nchini Zambia ikiwemo Zamfoot mshambuliaji huyo mwenye mabao 16 mpaka sasa alisema hata kama mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini, Yanga wataendelea kumshawishi, bado mawazo yake hayapo kabisa katika soka la Bongo kwani hata ofa anazopata ni kubwa kulizo hiyo ya Yanga.

darubiniyako ilimtafuta Were ambapo alikiri kuwepo kwa dili hilo na Yanga ila hajaamua kwani ana mipango mingine na si Yanga.

"Kweli Yanga wamefanya mazungumzo na mimi na kuahidi ofa nzuri lakini nina ofa kama mbili kutoka Afrika Kusini ambapo naendelea kuzitathimini, mawazo yangu hayapo kucheza soka la Tanzania, naogopa ligi ya Bongo kutokana na mambo ambayo tumeyashuhudia kwa wenzetu waliowahi kuja kucheza huko," alisema Were.

No comments:

Powered by Blogger.