Sare dhidi ya Simba yamsikitisha Pluijm

Kocha mkuu wa Yanga mholanzi Hans van der Pluijm amesema amesikitishwa na matokeo ambapo timu yake iliruhusu goli dakika za majeruhi na kuufanya mchezo kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 dhidi ya Simba ambao ni wapinzani wao wa kihistoria.

Pluijm amesema inasikitisha unaposhindwa kulinda matokeo dakika za lala salama na kumruhusu mpinzani wako kusawazisha.

“Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza tukapata goli na tukatarajia tungetawala zaidi katika kipindi cha pili lakini kukawa na tension kubwa kwa timu na wachezaji, tulipata nafasi lakini hatukuzitumia. Simba wakapata nafasi moja ya pekee wakasawazisha”, amesema Pluijm ambaye amekiongoza kikosi chake katika mechi tatu mfululizo bila kupoteza dhidi ya Simba.

“Ukishindwa kulinda matokeo ndani ya dakika nne za mwisho, inasikitisha. Kwahiyo nimesikitishwa na matokeo.”

Yanga walitangulia kupata goli dakika ya 26 kipindi cha kwanza kupitia kwa Amis Tambwe kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87.

No comments:

Powered by Blogger.