Mbwana Samatta Kuitoa Kimasomaso Genk leo
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta leo ataiongoza timu yake ya KRC Genk kusaka ushindi dhidi ya US Sassuolo ya Italia katika Kundi F la mashindano ya Ligi ya Europa.
Genk itakuwa nyumbani kuwakaribisha Waitaliano hao, Sassuolo ambao katika mchezo wao wa kwanza walifungwa na Athletic Club Bilbao ya Hispania, hivyo kufanya mchezo huo kuwa na umuhimu wa pekee kwa timu zote leo saa 4:05 usiku.
Samatta katika mchezo uliopita alishindwa kufurukuta kabla ya kutolewa kutokana na kuumia walipopokea kipigo kutoka kwa SK Rapid vienna ya Austria inayocheza dhidi ya mabingwa wa zamani wa mashindano hayo, Athletico Bilbao.
Samatta ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alianzia benchi na kuingia dakika 70, alitengeneza bao la kufutia machozi la Genk lililofungwa na Leandro Trossard. Walichapwa 4-1 na KV Kortrijk ukiwa ni mchezo wa pili mfululizo wakipoteza kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Manchester United yenye nyota wengi akiwamo Paul Pogba iliyoanza vibaya kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Feyenoord ya Uholanzi itakuwa nyumbani, Old Trafford kuwakaribisha Zorya Luhansk, wakati Ajax ya Uholanzi ikiivaa Standard Liege ya Ubelgiji na Sparta Prague ya Czech itakuwa wenyeji wa Inter Milan ya Italia.
No comments: