Rais Magufuli atisha wananchi


RAIS John Magufuli ametisha wananchi kwamba, wanaweza kuingia kwenye machafuko kama yale ya Rwanda, anaandika Moses Mseti.

“Jamani wana Sengerema nyie wenyewe mnafahamu matukio ya watu kupoteza maisha nchini Rwanda.


“… watu walikufa sana, sasa na nyie mnataka na sisi tuingie katika hali hiyo?” aliuliza Rais Magufuli ambapo hata hivyo, wananchi hawakujibu.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnadani, Kata ya Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema, Mwanza ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuwashukru wananchi.

Rwanda iliingia kwenye Mauaji ya Kimbari mwaka 1994 kutokana na mapigano ya kikabila kati ya Wahutu na Watusi tofauti. Rais Magufuli anatumia machafuko hayo kuwatisha wananchi.

Amesema kuwa, katika utawala wake hatakubali kuona chokochoko kutoka vyama vya siasa ambavyo hakutaja majina  huku akidai, kama wanataka kufanya hivyo wasubiri hadi ang’atuke.

Amesema, katika utawala wake pia hatokubali kuona watu wanakifanya maadamano na mikutano ya hadhara kwa madai, kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama na amani ya taifa hili.

“Wao wasubiri siku nikitoka ndio waje wavuruge amani ya nchi, lakini kama mimi nipo hakuna atakayekuja kuvuruga amani na kama wanataka kufanya hivyo, wasubiri mpaka siku niondoka,” amesema.

Julai 27 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza kuanza Oparesheni iliopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) inayotarajiwa kuanza Septemba Mosi mwaka huu nchi nzima.

Julai 29 mwaka huu, Rais Magufuli akiwa Ikungi mkoani Singida alisema kuwa, wanaoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara ni wabunge waliochaguliwa na kuelekeza wafanyie mikutano katika majimbo yao.

Katika mkutano huo pia Rais Magufuli amesema kuwa, serikali yake haina mpango na utaratibu wa kugawa chakula kwa kila mtu na kwamba, kama Watanzania watashindwa kufanya kazi, watakufa njaa.

“Mkuu wa mkoa (John Mongella) amesema kuhusiana na suala la chakula katika mkoa huu mkaguna, sasa nasema hakuna chakula cha bure na serikali haina chakula cha kugawa bure.

“Kama haufanyi kazi hakuna atakaekuketea chakula,  watu mmekaa tu na mvua inanyesha hamlimi chakula na watu mnaendelea kupiga stori kwenye vijiwe vya kahawa, ninawaambiwa ukweli kuwa hakuna chakula ambacho serikali itakitoa,” amesema rais Magufuli.

Pia amesema, Watanzania wengi hususani vijana wamekuwa wakikaa kutwa mtaani wakicheza ‘pool table’ bila kufanya kazi na kwamba, chakula kikikosekana huanza kuilaumu serikali.

No comments:

Powered by Blogger.