Ukawa waipa talaka CCM

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG)
WABUNGE 53 wanaotoka kwenye vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
wametengana rasmi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kujiondoa kwenye Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), anaandika Pendo Omary.
Hatua hiyo inakuja baada ya Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga (CCM) hivi karibuni kudai kwamba, anayeteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) lazima aitwe ‘beby’ ikiwa na maana ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa barua ya kujitoa iliyotolewa 6 Mei yenye saini 53 za wabunge hao 53 na kunakiliwa kwa Job Ndugai, Spika wa Bunge, wabunge hao wamesema;
“Licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na wabunge wa upinzani kutaka mwongozo wa spika ili Mlinga afute kauli yake, Naibu Spika (Dk. Tulia Ackson) alipuuza miongozo hiyo.”
Wamesema kauli hiyo imewadhalilisha kama wanawake na pia wabunge wa upinzani.
Juzi Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) alilaani vikali kitendo cha udhalilishwaji na matumizi ya lugha chafu na za kejeli dhidi ya wanawake bungeni na kwamba, kilichotokea bungeni ni muendelezo wa matukio ya utumiaji wa lugha ya kudhalilisha jambo ambalo halivumiliki.

No comments:

Powered by Blogger.