Mgambo na JKT Ruvu nani kushuka daraja leo


Mgambo JKT itaamua kubakia au kushuka daraja hii leo katika mpambano wake dhidi ya JKT Ruvu
mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Mkwakwani Mkoani Tanga.

Kitendo cha kushindwa kuifunga JKT Ruvu katika mechi hiyo moja kwa moja kitamaanisha kuwa timu nyingine ya mkoa wa Tanga, JKT Mgambo itakuwa imeteremka daraja kuwafuata ‘ndugu zao’ Coastal Union ambayo tayari imeteremka daraja.

Mgambo yenye pointi 24 baada ya kucheza mechi 28 inahitaji kushinda mechi zote mbili zilizobaki ukiwamo wa leo dhidi ya JKT Ruvu na dhidi Azam FC ili kufikisha alama 30 na kusubiri matokeo ya washindani wenzake katika vita ya kuepuka kushuka daraja ili kujua hatma yao.

Ikiwa imeshinda michezo mitano tu msimu huu, Mgambo inaweza kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu walipopanda Ligi Kuu msimu wa 2012/13.

JKT Ruvu inahitaji walau pointi mbili katika mechi zao mbili za mwisho
dhidi ya Mgambo kisha Simba SC ili kuwa na uhakika wa kubaki katika Ligi Kuu msimu ujao.

Ruvu imekusanya alama 29; ambazo haziwezi kuwafanya wawe salama kwa sababu Kagera Sugar iliyo nafasi ya 14 ina alama 25 huku wakiwa na michezo miwili mkononi, wakati African Sports ina wafuata kwa karibu ikiwa na alama 26 baada ya kucheza mechi 28 pia.

Sare itakuwa na maana kiasi kwa Ruvu lakini itakuwa na maana mbaya kwa Mgambo kwa kuwa watateremka daraja rasmi baada ya misimu yao minne katika Ligi Kuu.

Mchezo mwingine utakaopigwa hii leo ni Ndanda FC wakiwakaribisha Yanga Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ambapo mara baada ya mchezo huo Yanga atakabidhiwa kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

No comments:

Powered by Blogger.