Matusi ya CCM yakera wadau

Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji TGNP

KAULI chafu zilizotolea na wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya bunge hivi
karibuni, zimechefua wengi, anaandika Aisha Amran.
Miongoni mwao ni Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambao umeeleza kulaani vikali kitendo cha udhalilishwaji na matumizi ya lugha chafu na za kejeli dhidi ya wanawake bungeni,
Kauli ya kulaani imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji TGNP ambapo amesema, kilichotokea bungeni hivi karibuni ni ambacho kimekuwa ni muendelezo wa matukio ya utumiaji wa lugha ya kudhalilisha wanawake na kuwa, kitendo hicho hakivumiliki.
Miongoni mwa kauli chafu zinazolalamikiwa ni pamoja na ya Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga Mashariki (CCM) ambapo alinukuliwa akisema kuwa, “Mheshimiwa Spika, kuthibitisha hilo ili upate ubunge ndani ya Kambi ya Upinzani lazima uitwe ‘baby’.
“Watu hawa wamefikia hatua ya kuwa na mahusiano ya jinsia moja,” alinukuliwa Mlinga.
Kauli hiyo ilisababisha mtifuano ambapo Job Ndugai, Spika wa Bunge alilazimika kuwatoa nje wabunge wanawake wa Ukawa kutokana na kuibua zogo.
Kabla ya kutolewa nje, wabunge hao waliomba muongozo kutoka kwa spika kutaka Mlinga afute kauli yake, spika hakuruhusu na hapo ndipo fujo zilianza kuibuka na hatimaye kutimuliwa nje.
Liundi wa TGNP amesema, tukio hilo ni kinyume na tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu, mkataba wa kimataifa wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na mikataba mingine ya haki za binadamu na usawa wa kijinsia ambayo nchi imeridhia.
Hata hivyo amesema, ni kinyume pia na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 9(f),(g) na (h) na ibara ya 12 (2) na ni uvunjwaji wa sheria namba 15 ya mwaka 1984 ibara ya 6.
Amesema, “ikumbukwe kuwa Bunge ni nguzo na muhimili mmojawapo mkuu katika nchi, hivyo basi halipaswi kuruhusu mbunge yeyote yule awe wa kiume au wa kike kutumia chombo hiki muhimu kukandamiza sauti za wanawake.”
Aidha amesema, wanataka kuona hatua stahiki za kinidhamu zikichukuliwa dhidi ya wale wote wenye tabia kama hizi ili kukomesha mwenendo huo ambao unarudisha nyuma harakati za kutetea haki za wanawake katika uongozi na kukiuka misingi ya utawala bora nchini.
“Hali kadhalika tunatoa wito kwa jamii kwa ujumla kukemea na kuwawajibisha wabunge wao ambao wamewapa kura ili wakatetee maslahi ya kimaendeleo kwa wananchi wote,” amesema Liundi na kuongeza;
“Tunakemea na kulaani vikali mwenendo huu ambao unarudisha nyuma harakati za kutetea haki za wanawake katika uongozi na kukiuka misingi ya utawala bora nchini.”

No comments:

Powered by Blogger.