Kilichotibua bunge hiki hapa

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MUSSA Azan Zungu, Mwenyekiti wa Bunge leo asubuhi aliahirisha bunge mpaka saa 10 jioni baada ya
kuzuia usomwaji wa Hotuba ya Godbless Lemba, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imezuia, anaandika Faki Sosi.
Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Lema iliyosababisha bunge kusitishwa shughuli zake.
5.1 Mkataba tata wa Lugumi na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali , ilihoji utekelezaji wa mkataba wenye utata wa vifaa vya Mfumo wa Alama za Vidole (AFIS) ulioingiwa kati ya Jeshi la Polisi Tanzania na Kampuni ya Lugumi Enterprises.
Mheshimiwa Spika, kumetokea majibishano na malumbano mengi kwenye vyombo vya habari na miongoni mwa wabunge wa Bunge lako tukufu, hasa pale walipoanza kuhoji utekelezaji wa mkataba huo hasa kuhoji juu endapo vifaa hivyo vinafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia majibishano na malumbano yaliyojaa utata ambao lazima upatiwe majibu yasiyo na shaka yoyote, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kutoa majibu ya moja kwa moja bila kupepesa macho. Tunataka Maswali yafuatayo yajibiwe hapa bungeni;
Mheshimiwa Spika,
1)                       Kwa kuwa mikataba ya serikali kwa mujibu wa sheria lazima ufuate sheria za manunuzi na kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Je, Utaratibu huu ulifuatwa?
2)                       Je Mkataba huu wa LUGUMI ENTERPRISES na JESHI LA POLISI umetekelezwa ama haukutelezwa, na kama ulitekelezwa ni kwa kiwango gani, na ikiwa kulikua na tatizo la utekelezaji, Je, Jeshi la Polisi lilichukua hatua zipi?
3)                       Je, ni kampuni ngapi ambazo zinahusika na hatua za utekelezaji wa Mkataba kati ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi, kwa kuwa kampuni ya INFOSYS ambayo mmoja wa wamiliki wake ni Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga inatajwa kufunga vifaa hivyo (AFIS).
4)                       Ni kwanini C.A.G katika ukaguzi wake hakuhoji kuhusu uhalali na ulinganishi wa thamani ya pesa ya manunuzi na faida ya vifaa hivyo?
5)                       Kampuni ya INFOSYS (inayomilikiwa na Mhe. Kitwanga) imedai kulipwa na Jeshi la Polisi, takribani Dolla za Marekani 74,000, Je fedha hizi Kampuni ya Mhe. Kitwanga ililipwa kwa kazi ipi iliyofanya na Jeshi la Polisi?
6)                       Ni kwanini mpaka sasa , Rais Magufili hajachukua hatua dhidi   Said Lugumi, na aliyekuwa IGP Said Mwema / Emmanuel Nchimbi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani   na kuwasimamisha kazi wale wote ambao bado wako kazini juu ya mkataba tata wa Lugumi ?
7)                       Tunamtaka Rais , kutengua mara moja uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe na kumrudisha nchini mara moja , kwani alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na ni imani ya Kambi rasmi kuwa alijua mambo yote yanayoendelea ya mkataba wa Lugumi
Mheshimiwa Spika , Ni imani ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa Mhe.Waziri Charles Kitwanga, anazo taarifa za Mkataba huu na utekelezaji wake aidha kutoka kwenye Kampuni yake ambaye yeye ni Share holder ( Mbia ) ambayo ilifunga vifaa hivi au anazo taarifa ya utekelezaji wa Mkataba huu kutoka Jeshi la Polisi ambalo liko chini yake kwa kiwango chote kuhusu mambo yote ya Mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) , alinukuliwa na vyombo vya habari pale alipoulizwa kuhusu sakata la Lugumi na Mikataba yake na Jeshi la Polisi kutotekelezwa, alijibu majibu mafupi Katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 27/04/2016 namnukuu “siyo kweli, watu wana ugomvi wao kibiashara, lakini nakueleza wazi kwamba, tembelea vituo vyote tulivyokubaliana, utakuta mashine zipo. Inawezekana zingine hazifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa internet” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na maswali ambayo tumeuliza hapo juu na uchambuzi wetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika,
  1. Kwa vile Waziri wa Mambo ya Ndani anahusika kwa karibu katika Mkataba huu kupitia Kampuni yake ya INFOSYS na vile vile Jeshi la Polisi liko chini yake , je ? haoni kuwa ni busara kwa yeye kujiuzulu ili kutoa nafasi ya Uchunguzi kuepusha mgongano wa maslahi ndani ya Jeshi la Polisi na kwenye Kampuni ambayo yeye ni mmoja wa wamiliki ?
Mheshimiwa Spika,
  1. kwa vile inaonekana kupitia vyombo vya habari na kauli za viongozi mbali mbali kuwa upo uwezekano wa Polisi kuwa wametapeliwa na vifaa hivyo havijafungwa, Kambi ya Upinzani Bungeni inautaka uongozi wote wa juu wa Jeshi la Polisi kujiuzulu mara moja, kwani kama wao wameshindwa kujua ukweli wa vifaa vilivyofungwa kwenye vituo vyao vya Polisi ama vipo au havipo, watawezaje kuchunga na kulinda mali na usalama wa raia wengine?
Mheshimiwa Spika,
  1. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka majibu yote yanayohusu Mkataba wa Lugumi na Jeshi la Polisi kuhusu utekelezaji wake uwekwe wazi hapa bungeni na wizara husika

No comments:

Powered by Blogger.