HATIMAYE KOCHA WA ARSENAL ..ARSENE WENGER AKUBALI YAISHE KWA MASHABIKI
Wakati shinikizo la kutakiwa kuondoka likiendelea kupamba moto katika
mitaa mbali mbali ya kaskazini mwa jijini London, meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesalimu amri kwa kukubaliana na hali halisi.
Wenger ambaye anashinikizwa kuondoka Emirates Stadium kufuatia kushindwa kuipatia taji la ligi kuu ya soka nchini England klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 12, amekiri kufanya kosa hilo ambalo limeonyesha kuwachukiza walio wengi.
Babu huyo mwenye umri wa miaka 66, amesema anatambua amefanya kosa la kutowafurahisha mashabiki wa Arsenal kwa kipindi kirefu na hana budi kukubaliana na hali hiyo.
Amesema ni vigumu kwenda kinyume na matakwa ya mashabiki wengi walionyesha kumchoka kwa sasa, zaidi ya kukubali kosa na kuamini atafanikisha kila linalowezekana ili kurejesha furaha miongoni mwao.
“Nina jukumu la kumfurahisha kila mmoja klabuni hapa, na sina njia ya mkato zaidi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini England, ninakiri hilo ni kosa nililolifanya kwa muda mrefu.”
“Ninaamini hakuna kinachoshindikana nitajitahidi kufanikisha azma iliyokusudiwa na walio wengi na ninaahidi kufanikisha hilo kipindi kijacho.”
Wenger alikubaliana na hali inayomzunguuka, baada ya mashabiki kuonyesha mabango wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita ambapo The Gunners walifanikiwa kupata ushindi wa bao moja sifuri lililofungwa na danny Welbeck dhidi ya Norwich City.
Kikundi cha mashabiki waliokua wamejitokeza uwanjani siku hiyo walionyesha mabango hayo katika dakika ya 12 na 78 huku wakiimba nyimbo za kuhitaji mabadiliko kwa kuashiria meneja huyo hana nafasi ya kuendelea na kazi yake klabuni hapo zaidi ya kuwapisha wengine.
Mabango yaliyokua yamebebwa na mashabiki hao yalikuwa na ujumbe uliosomeka “Tunakupenda Arsenal, Tumejitahidi Kwa Kila Hali “, Tunataka Mabadiliko Baada Ya Kuwa Wadhaifu Kwa Kipindi Cha Miaka 12 Bila Ya Kutwaa Ubingwa Wa Ligi Ya England.”
No comments: