KKKT lahaha kumsafisha Askofu Malasusa
TAMKO limeandaliwa ili kusafisha tuhuma zinazomkabili Dk. Alex Malasusa, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri
Tanzania, (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), anaandika Josephat Isango.Taarifa kutoka kwenye kanisa hilo zinaelezwa kwamba, tamko hilo limeandaliwa ili kushawishi waumini wapuuze taarifa zilizoandikwa kuhusu Askofu Malasusa na kwamba, yeye (Malasusa) hatotakiwa kusema lolote kuhusu tuhuma zake.
MwanaHALISI online, limeona waraka unaotarajiwa kusambazwa wakati wowote kuanzia sasa ambao umeelekezwa kwa wakuu wa majimbo, wachungaji, viongozi, wakuu wa vituo na taasisi pamoja na washirika wote.
Wakati kanisa likiandaa tamko hilo, Dk. Malasusa hajaandika wala kukanusha tuhuma zinazoelekezwa kwake wala kuzungumzia sakata la Muhimbili, sakata la watoto watatu ambao walitarajiwa kusafiriwa nje ya nchi.
Mzazi wa watoto hao, Venance Mwakilima aliiomba Mahakama ya Mwanzo Maili Moja kumpa amri kamishana wa uhamiaji azuie watoto wake wasisafiri nje ya nchi kama ilivyodaiwa.
Tamko hilo halijawataja Sijenuna Venance Mwakilima, mwenye hati ya kusafiria Na. AB 524934, Stephania Venance Mwakilima Na. AB 524933, Simon Venance Mwakilima Na. AB 599057 na mama yao Leita Ngoyi Mwakilima Na. AB.524932.
Tamko linasomeka “Wapendwa watu wa Mungu. Habari zilizoandikwa na gazeti la MwanaHALISI na Mseto yanayomilikiwa na kampuni moja ya Hali Halisi Publishers Ltd, kuhusu Askofu wetu sio za kweli,”
Linaongeza kwamba, “Kanisa limetafakari kwa kina kuhusu habari hizo na malengo ya mwandishi huyo kuandika kwenye magazeti yote mawili kwamba, alilenga kulishambulia Kanisa kwa sababu anazozijua mwandishi na mmiliki wa magazeti hayo.
“Kanisa linapenda kuwaomba waumini wote na jamii kwa ujumla, kuwa wavumilivu na kuendelea kuliombea Kanisa na uongozi wake huku hatua stahiki zikichukuliwa.”
Baadhi ya wachungaji walioongea na mwandishi katika Ibada za Jumuiya leo Jumamosi, wamesema Kanisa halihusiki na tuhuma za mtu binafsi, kwani Kanisa halikuenda Muhimbili, wala halikuandika ujumbe wa simu za kimahusiano na mke wa mtu, wala kutoa maelekezo ya kuwaficha watoto.
“Hilo ni suala lake binafsi, na watu wanapolalamika hawalalamikii Kanisa, wanalalamikia tabia ya mtu,” amesema mchungaji aliyedai kuwa anamfahamu Dk. Malasusa kwa karibu.
Kwa upande mwingine, familia ya Venance Mwakilima wamezungumza na mwandishi na kuahidi kuwa, wanasubiri tamko hilo lakini kama watakuwa na suala la kujibu watasema kwani wao hawana ugomvi na Kanisa bali tabia ya Dk. Malasusa.
“Nimemwandikia Askofu ujumbe mfupi kwa njia ya simu ukisema, Baba Askofu nilikwambia tukae kikao ukadharau, ukanipuuza sasa mambo yalipofika huku ndio unafurahi?”
Amesema Asime Mwakilima, kaka wa mume ambaye ameahidi kuwa, akirejea kutoka Mbeya atazungumza mengi zaidi huku akimlaumu Askofu kwa kutojibu ujumbe wa simu aliomwandikia.
Aidha mume aliyelalamika na kumtuhumu Askofu Malasusa, ameyashukuru magazeti ya MwanaHALISI na Mseto kwani baada ya habari hizo kuandikwa, kesi alizokuwa anabambikizwa zimefutwa zote, na watoto wote walikuwa wamefichwa wamerejea nyumbani leo asubuhi tarehe 30 Aprili 20016.
Askofu Malasusa anatuhumiwa kujihusisha kimapenzi na mchungaji wa kanisa hilo ambaye ni mke wa mtu.
Anayemtuhumu Dk. Malasusa ni Mwakilima, mkazi wa eneo Vikawe, Bagamoyo ambaye ni mfanyakazi wa Shule ya Msingi Dunda.
Dk. Malasusa anadaiwa kuwa na uhusiano na Leita Ngowi, mchungaji na mkurugenzi wa idara ya wanawake usharika wa Azania Front, Jijini Dar es Salaam aliyepandishwa cheo siku za karibuni na askofu huyo.
No comments: