Mbunge Profesa Jay Afunguka Kuhusu Chid Benz Kutumia Madawa ya Kulevya


Mbunge wa Mikumi kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (pichani) amesema hali ya Mbongo Fleva, Rashid Abdallah Makwiro (31) ‘Chid Benz’ ni matokeo ya matumizi yaliyobebea ya madawa ya kulevya ‘unga’, Amani lina mchirizi wake.

Hivi karibuni, Chid Benz aliripotiwa na baadhi ya mitandao ya kijamii akionekana na hali isiyoridhisha kiasi kwamba, baadhi ya wachangiaji walisema; inauma sana!

Mwonekano wa sasa wa Chid ni wembamba wenye maswali mengi huku marafiki zake wa karibu wakidai kwamba ‘unga’ umemfanya afikie hali hiyo.

Akizungumza na gazeti hili juzi Jumanne jijini Dar baada ya kuombwa mchango wake kuhusu hali ya Chid, mbunge huyo alisema:

“Hili ni tatizo sana kwa sasa. Si kwa Chid Benz tu, bali kwa vijana wengi sana wa nchi hii ambao ni nguvu kazi ya taifa hili. Tusiwanyanyapae wale wanaoathirika na madawa bali tuwasaidie tunavyoweza ili warudi kwenye hali zao za kawaida.

“Naomba sana serikali ilichukulie suala la madawa ya kulevya kama janga kubwa sana na ilikimee kwa nguvu zote na kuweka sheria na adhabu kali ili kulinusuru taifa hili linalopoteza nguvu kazi kubwa kwa madawa ya kulevya.”

Jumatatu iliyopita, Amani lilimsaka Chid mwenyewe ili kuweza kuzungumza naye kuhusu hali yake lakini mara zote alionesha kutokuwa na utayari wa kukutana na gazeti hili hata pale gazeti lilipowatumia watu wake wa karibu, akiwemo Mwanamuziki wa Kizazi Kipya, Kalama Masoud ‘Kalapina’.

Akizungumza na Amani juzi kuhusu watu walioathirika na unga, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alisema wale ambao vipimo vinaonesha wameathirika, wajitokeze wakatibiwe kuondoa madhara mwilini, lakini serikali inaendelea kuwakamata wasambazaji wa biashara hiyo haramu.

“Serikali inafanya juu chini kuikomesha biashara hiyo. Kuhusu kuwakamata watumiaji, kunataka uhakika. Inawezekana mtu alitumia muda mrefu akaathirika, hao waende wakatibiwe tu ili kuondoka athari,” alisema Masauni…

KUMBUKUMBU ILIYOPITA
Oktoba mwaka 2014, Chid Benz alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar akikabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kukutwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin yenye thamani ya Sh. 38,638, bangi ya Sh. 1, 720 na vifaa ya kuvutia dawa hizo, kijiko na kigae.

Chid Benz alisomewa mashtaka yake saa 7:50 mchana na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Mwanaamina alisema Chid alinaswa na mzigo huo Oktoba 24, mwaka huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Ilala jijini Dar es Salaam.

Februari mwaka jana, Chid alipatikana na hatia ambapo Hakimu Lema alimhukumu kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh. 900,000 ambapo aliweza kulipa kiasi hicho na kuwa huru.

No comments:

Powered by Blogger.