- Kuna tabia moja ambayo Barcelona na Bayern Munich wanafanana kwa kiasi kikubwa sana, nayo ni udhaifu katika eneo lao la ulinzi. Inawezekana kabisa kwa upande wa Bayern limechangiwa na majeruhi ya walinzi wake hivyo kulazimika kupanga viungo katika eneo hilo, lakini kwa timu yenye akili timamu katika eneo la ushambuliaji ni kazi rahisi sana kuwadhuru hawa wawili na ndio jambo ambalo wapinzani wanaofuata walitizamie kulitumia wanapokutana nao.
- Manchester City hawajawa tayari kuwa mabingwa wa UEFA Champions League kwa tabia zao. Bingwa wa UEFA mara zote ni yule anayejua kupata matokeo latika uwanja wake wa nyumbani. Kwa Man City hili bado ni somo gumu ambalo inaonekana hawajapata mwalimu anayelipatia katika viwanja vyao vya mazoezi na vyumba vya kubadilishia nguo. Hii ndio imekuwa tabia inayowaua siku zote huku ikiwa ndio silaha ya vilabu vingine vikubwa.
- nawawaza Barcelona sana au Bayern Munich, usiwapotezee Paris St Germain, inawezekana wakawastua watu wengi. Rekodi ya safu yake ya ulinzi katika mashindano haya ni nzuri sana jambo ambalo linanipa sababu ya kuamini kuwa wanaweza kufika mbali sana. Tatizo kubwa ambalo wanatakiwa waliweke sawa ni Zlatan kung’aa mechi kubwa, lakini pia kuondoa tabia ya Man City ya kutokupata matokeo chanya katika uwanja wa nyumbani. Ukizingatia wameshatwaa ubingwa wa ligi mapema kabisa, nguvu yao huku itakuwa kubwa kupindukia na wana kila silaha ya kupambana kwa majinaya mgongoni ya wachezaji.
- Ukomavu alionao Neymar kwa sasa hivi ndio ambao unaleta hatari kubwa waliyonayo MSN kwa vilabu vingine. Sababu kubwa ni kwamba ndiye mchezaji ambaye watu au wapinzani wa Barcelona humtizama kwa jicho changa Zaidi kuliko wale wenzake na kusahau kuwa ndiye nishati inayowawasha hawa wawili. Neymar ndiye mchezaji anayekimbia sana na mpira kuelekea upinzani huku akipunguza wingi wa mabeki katika eneo la ulinzi na kutoa mianya inayofaa kwa wawili waliobaki kuwa hatari kupindukia kila mipira inapowafikia kwa sababu mfumo wa kiulinzi unakuwa umeshasambaratika.
- Wenger angekuwa Masia angechukua maamuzi mazito sana ambayo hata mashabiki wa Arsenal wangesubiri yasifanikiwe wamkate kichwa lakini naamini yangefanikiwa. Kwa mwenendo mzima wa Arsenal ya sasa, mtu wa kwanza anayetakiwa kwenda kwenye mbao ndefu ni Alex Sanchez. Tangu arejee kutoka katika majeruhi timu haifanyi vyema, nayo ni kwa sababu timu inamzunguka yeye wakati uwanjani kuna kivuli chake, yeye mwenyewe amepotea kusikojulikana. Ozil anakuwa mbali Zaidi na mpira na akiwa nao anakuwa mbali Zaidi na washambuliaji wake kuwapa pasi za mwisho. Si ajabu tangu arejee Sanchez ana assist 3 pekee.
- Kilichowaondoa Juventus katika mashindano haya ni akili yao wenyewe kuanzia kwa kocha, wachezaji mpaka mashabiki wa timu hiyo na wala sio ubora wa Bayern Munich katika mchezo huo. Ni nadra sana kupata bahati ya kucheza na Bayern Munich nyepesi namna ile, lakini tabia za mchezo wa kwanza ndizo zilizowarudisha nyuma Juventus. Baada ya kuwa mbele magoli mawili, walihisi kabisa yale yaliyotokea kule Turin ya kurejesha bao mbili yangeweza kutokea na huku Allianz Arena, hivyo walivyofika dakika za 65 Allgeri akauvaa ujinga wake na kuhitaji kuzuia Zaidi. Waenga walisema mdomo na fikra uumba. Guardiola alivyogundua nafasi ya Morata ambaye alikuwa na uwezo wa kuisogeza timu nzima kwa miguu miwili ametoka na kaingia Mandzukich ambaye sio bora katika kukokota mipira huku Juventus ikiwa imejigawa kati ya wachezaji 9 dhidi ya mshambuliaji mmoja, kazi ikawa nyepesi ni kucheza mbele tu huku Neuer akiwa mbele ya goli lake kuiwahi mipira.
- Real Madrid wanacho ambacho Atletico Madrid hawana na Atletico Madrid wanacho ambacho Real Madrid hawana. Siku ambayo mastaa wa Real Madrid wakiwa nje ya mchezo unatamani kabisa walau timu ingekuwa inacheza kwa moyo kama majirani zao, na kile kipindi ambacho PSV Eindhoven inawamiliki kabisa Atletico Madrid unatamani kabisa Ronaldo angekuwa kavaa ile jezi ya Fernando Torres au Carrasco. Tatizo pekee ni kuwa Real Madrid haina muunganiko na pia haina moyo walionao Atletico Madrid, moyo wa kukutuma kukimbia kilomita 100 ndani ya mchezo mmoja, ile roho ya kuhakikisha mchezo unamalizika wapinzani wakiwa hawajui walikuwa wanacheza na binadamu wenzao au wanyama. Hawa majirani wawili wote ni ngumu kiasi kutwaa ubingwa huu lakini wakiviazima hivi kwa muda uliobakia hasa Real Madrid basi watakuwa hatari Zaidi, hata akina Griezman wanatakiwa kujua wakati wa kuonyesha upekee.
- Wolfsburg wanamiliki moja ya viungo bora kabisa katika mashindano haya kupitia kwa Julian Drexler. Ukiachana na Barcelona na pengine Bayern Munich hakuna kikosi kingine ambacho kwa kiwango chake cha sasa angekosa kucheza vyema katika kikosi cha kwanza. Najua unawaza pengine Real Madrid au Paris St Germain lakini sio Moura wala James Rodriguez aliyeweza kuonyesha ubora wa kijana huyu katika mashindano haya. Nakukumbusha tu shabiki wa Arsenal kuwa huyu na Higuain waliwahi kuwa wachezaji wa Arsenal katika ulimwengu wa kufikirika kabla Wenger hajamwamini Sanogo na Alex Oxlade Chamberlain.
- Masimilliano Allegri anaamini kuwa anaanza Mandzukich, Dybala kisha Morata lakini katika upande wa pili wa shilingi Nicasius ninaamini pale Uingereza ingeweza kuwa Morata kisha mastraika wa Vilabu vingine. Inawezekana kabisa Madrid wakafanya kila wanaloweza kumrejesha mwisho wa msimu na wakafanikiwa, lakini hii ndio nafasi ya Wenger kuachana na ndoto za Giroud ama wale Liverpool kupunguza matumaini ya Benteke. Akirejea Madrid na kwa sababu Perez hajawahi kuwa na akili timamu za kisoka basi Benzema naweza kupatikana hasa wakati huu ambao Aubameyang analilia kwenda Santiago Bernabeu.
- Pamoja na udogo wake au mwonekano wake wa kidhaifu dhaifu usijaribu kumkumbatia Nungunungu wataalamu wa porini wanasema. Rui Vitoria kocha wa Benfica ametengeneza timu ambayo ina uwiano mzuri na kikubwa kinachovutia ni kuwa wakongwe wengi wapo katika eneo la ulinzi huku eneo la kiungo mpaka ushambuliaji likiwa bado na wachezaji wengi vijana au wenye umri wa kati hali inayowafanya kuwa na nguvu na kasi sana katika kuweka presha katika upinzani. Inaweza isiweze kufika mbali lakini ni timu ya kuchungwa sana kwa yoyote atakayekutana nayo.
MAMBO KUMI NILIYOJIFUNZA BAADA YA HATUA YA 16 UEFA CHAMPIONS LEAGUE
Reviewed by
Unknown
on
02:22
Rating:
5
No comments: