Jecha aendesha uchaguzi Zanzibar kutoka mafichoni
Hatimaye uchaguzi mkuu wa marudio Zanzibar unafanyika leo huku Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha akishindwa kuonekana hadharani kuzungumzia uchaguzi huo.
Kwa kawaida, kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25 kabla ya kufutwa siku tatu baadaye, Jecha alitarajiwa kuwa mstari wa mbele na kuzungumza na waandishi wa habari kwa nia ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na uchaguzi huo.
Hata hivyo, katika tukio nadra kuwahi kutokea hapo kabla, Jecha aliendelea kuadimika na hadi kufikia jana jioni, taarifa zake kwa umma zilitolewa kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na wasaidizi wake tu huku yeye mwenyewe akiendelea kutoonekana hadharani.
Uchaguzi huo wa marudio unafanyika leo baada ya ule wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015 kufutwa na Jecha kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa kasoro nyingi zilizouondolea sifa ya kuwa ‘uchaguzi huru na wa haki’.
Rais Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anatarajiwa kushinda kirahisi katika uchaguzi wa leo baada ya mpinzani wake wa karibu, Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi huo kwa maelezo kuwa siyo halali huku kikiitaka ZEC iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura zilizotokana na uchaguzi wa Oktoba na kumtangaza mshindi.
Katika taarifa yake iliyodsambazwa kwa vyombo vya habari visiwani Zanzibar jana, Jecha alisema waangalizi wa kimataiafa wakiwamo kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) hawatakuwapo kushuhudia uchaguzi huo.
Badala yake, taarifa hiyo ya Jecha ilieleza kwamba kutakuwa na waangalizi wa ndani pamoja na wengine watokao Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika uchaguzi wa awali, waangalizi karibu wote, kutoka ndani na nje ya Tanzania waliusifia uchaguzi huo wa Zanzibar kwa kuulezea kuwa ulifanyika kwa uhuru na haki; baadhi yao wakiwa ni kutoka EU, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), SADC, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Taasisi ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO).
Hata hivyo, baada ya Jecha kutangaza kufutwa kwa uchaguzi huo Oktoba 28 kwa kudai haukuwa huru na wa haki, EU na Marekani zilipinga taarifa hiyo na hivyo haikutarajiwa kuwa zingetuma wawakilishi wake katika uchaguzi wa leo ulioibua mgogoro mpya wa kisiasa visiwani humo baina ya CCM na mahasimu wao, CUF.
UCHAGUZI PEKEE VYAMA VINGI BILA CUF
Uchaguzi wa leo ni wa kihistoria tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi visiwani Zanzibar kwa kuwa unafanyika huku mgombea wa CUF, Maalim Seif akiwa siyo miongoni mwa wagombea na pia wafuasi wa chama hicho wakitarajiwa kutoshiriki kwa wingi kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.
Tangu mwaka 1995, CUF imekuwa ikichuana vikali na CCM huku vyama vingine vikiambulia jumla ya kura za idadi ya chini ya asilimia moja.
Katika kuleta maelewano visiwani Zanzibar, katiba ya mwaka 1984 ilifanyiwa mabadiliko na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lengo likiwa ni kuunganisha nguvu ili kuimarisha umoja miongoni mwa Wanzanzibar ambao kwa kiasi kikubwa wamegawanyika kiitikadi kupitia kambi za CCM na CUF.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Zanzibar, ili chama cha siasa kipate sifa ya kuwamo katika kuunda SUK, ni lazima kipate walau asilimia 10 ya kura zote halali zilizopigwa katikia Uchaguzi Mkuu.
Kutokana na matakwa hayo ya katiba, kuna kila dalili kuwa uchaguzi wa leo utaipa CCM mamlaka ya kuongoza peke yake kwa kuwa vyama vingine, mbali na CUF ambayo imegomea uchaguzi huo, havitarajiwi kuwa na uwezo wa kufikisha asilimia 10 ya kura zote.
ULINZI MKALI
Hadi kufikia jana jioni, maeneo mengi ya Unguja visiwani Zanzibar yalikuwa na askari wenye silaha wa vikosi mbalimbali wakiwamo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku wengi wao wakionekena kwenye maeneo nyeti kama ya Bandari, makao makuu ya ZEC na Uwanja wa Ndege.
Aidha, upekuzi mkali kwa kila abiria aliyekuwa akiingia Unguja kupitia bandarini ulikuwa ukifanyika kwa siku nzima, huku taarifa zikidai kuwa ulinzi huo mkali umelenga kuhakikisha kuwa amani inakuwapo muda wote na kuwapa fursa wananchi wote kujitokeza kwenda kupiga kura pasi na bughudha.
WANAOCHUANA NA SHEIN LEO
Baada ya wagombea wa vyama vingine akiwamo Maalim Seif na chama chake (CUF) kutangaza kuwa hawatashiriki uchaguzi huo, waliobaki kuchuana na Dk. Shein katika uchaguzi wa leo ni Khamis Iddi Lila wa (ACT-Wazalendo), Juma Ali Khatib (TADEA), Soud Said Soud (AFP), Hamad Rashid Mohamed(ADC), Issa Mohamed Zonga(SAU), Hafidh Hassan Suleiman (TLP) na Ali Khatib Ali wa CCK.
MARAIS WALIOTANGULIA ZANZIBAR
Katika historia ya visiwa vya Zanzibar, marais waliowahi kuongoza ni Sheikh Abeid Amani Karume aliyeongoza kuanzia Januari 12, 1964 hadi Aprili 7, 1972; Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi aliyeongoza Aprili 11, 1972 hadi Januari 30, 1984; Alhaji Ali Hassan Mwinyi Januari 30, 1984 hadi Oktoba 24, 1985; Idris Abdul Wakil Oktoba 24, 1985 hadi Oktoba 25, 1990; Dk. Salmin Amour Juma Oktoba 25, 1990 hadi Novemba 8, 2000; Amani Abeid Karume Novemba 8, 2000 hadi 2010 na kisha Dk. Shein aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza Novemba, 2010.
No comments: