UKAWA Watoa Tamko Baada Ya Uchaguzi Wa Umeya Jijini Dar Kuhairishwa Leo

Uchaguzi Mkuu ulifanyika tarehe 25.10.2015
na wananchi wa Jiji
la DSM Waliamua kuongozwa na UKAWA na ndio maana walichagua Madiwani na Wabunge
wengi kutoka UKAWA. Kati ya Majimbo 10 ya Uchaguzi katika Jiji la DSM CCM
ilipata Majimbo 3 tu baada ya kuchakachua na UKAWA ilipata yaliyosalia.
Hali ni hiyo hiyo kwenye kata. Wananchi waliamua kuipumzisha CCM
kwa kuwa walikua wamechoshwa na uendeshaji mbaya wa Jiji la Dar es Salaam .
Tangu Uchaguzi umalizike mpaka leo wananchi wanakosa huduma za Jiji kwa sababu
CCM ilitaka kushinda Umeya wa Jiji kwa staili ileile waliyozoea ya goli la
mkono.
Mara wakaletwa wapiga kura feki kutoka Zanzibar huku Wakijua
wazi kuwa TAMISEMI sio jambo la Muungano. Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI
hajawahi kutoa kauli wala kukemea hali hiyo hata siku moja huku akijua wazi
kuwa vitendo hivyo vilikua ni kinyume Cha sheria za Nchi.
Leo tarehe 27.02.2016 tumeshuhudia Uchaguzi ukiitishwa na baada
ya wajumbe Kuwasili wakakutana na kilichoitwa zuio la Mahakama la Tangu tarehe
05.02.2016 .
Jambo hili limetokea baada ya Taarifa kusambaa jana tarehe
26.02.2016 kuwa CCM walipeleka shauri mahakamani la kuweka zuio na kuwa shauri
hilo lilitupiliwa Mbali.
Nini kinafichwa Jiji la DSM ? Tuna taarifa kuwa ni Ufisadi
mkubwa uliofanywa na viongozi wa Jiji waliopita na wakishirikiana na Viongozi
wa CCM kupora Mali za Jiji kama vile UDA, Mali za soko la Kariakoo, Viwanja na
majengo ya Jiji.
Pili tuna Taarifa kuwa hawataki majipu ya Jiji yatumbuliwe kwani
kuna vigogo wakubwa wa CCM watatumbuliwa kutokana na kushiriki kwenye Ufisadi
mkubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam . Mipango iliyopo.
Mkutano wa Uchaguzi Leo uliitishwa pamoja na kuwepo hicho
kinachoitwa zuio la Mahakama kwa lengo la kuwaudhi Madiwani wa UKAWA ili
waonekane kuwa wanafanya fujo .
Hii ni kutokana na ukweli kuwa kama zuio lipo Tangu siku CCM
wanaadhimisha miaka39 ya kuzaliwa kwake ni kwanini Mkurugenzi aliitisha mkutano
wakati akijua Mahakama imeweka zuio?.
Mpango huu umesukwa ili kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana
na TAMISEMI anatengenezewa sababu za kuweza kuvunja Halimashauri ya Jiji la Dar
es Salaam na kuunda Tume ya kuongoza Jiji.
Ni vyema tukaweka angalizo mapema kuwa Mafisadi wana mikakati
mingi sana ya kuhakikisha kuwa hawatumbuliwi Majipu. Kama Rais ambaye ndio Waziri
mwenye dhamana na TAMISEMI hakubaliani na mbinu hizi za Mafisadi, aingilie Kati
Mara moja na kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa Meya unafanyika na kazi ya kutumbua
majipu ya Jiji inaendelea kama ambavyo imeshaanza katika Manispaa za Ilala na
Kinondoni zinazoongozwa na UKAWA .
Imetolewa na John Mrema.
Mkurugenzi wa Bunge na Halimashauri CHADEMA.
No comments: