Rais Magufuli Atumbua Mapapa Wauza ‘Unga’..Adai Haiwezekani Wauza Unga Wakawa na Nguvu zaidi ya Serekali

Kasi ya
Rais John Magufuli ya kutumbua
majipu sasa imeanza kuvunja mtandao wa dawa za
kulevya (unga) nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Rais
Magufuli ametoa maelekezo mahsusi kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles
Kitwanga akielekeza kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji na
watumiaji ‘unga’.
Rais
amenukuliwa akisema haiwezekani wauza unga wakawa na nguvu kuliko Serikali.
Tayari
maofisi wa Serikali wameanza kulifanyia kazi agizo hilo kimyakimya na kwa kasi
ya aina yake, ambako sasa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakihoji
wafanyabiashara wenye ukwasi usioelezeka na katika kufanya hivyo wamekutana na
‘maajabu’.
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha operesheni ya
kukamata wafanyabiashara wote wanaohusishwa na dawa za kulevya jijini Dar es
Salaam.
Katika
operesheni hiyo, tayari polisi wamekamata ‘mapapa’ wawili wanaoelezwa kuwa
miongoni mwa ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu nchini. Mapapa hao wanashikiliwa
Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni.
Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni umeanza msako mkali wa kimyakimya kwa wafanyabiashara
hao; operesheni inayoelezwa kuwa inahusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa na kitengo maalum kutoka Ikulu.
JAMHURI
limethibitishiwa kuwa Hemed Horohoro na Lwitiko Samson Adam, ni kati ya mapapa
waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba na sasa wametiwa nguvuni.
Lwikito
ambaye anaelezwa kuwa na makazi nchini Afrika Kusini, alikamatwa nyumbani kwake
Magomeni jijini Dar es Salaam. ‘Papa’ huyo, amekutwa kwenye ‘nyumba ya ajabu’.
“Huwezi
kuamini. Lwitiko aliishi maisha ya peponi. Ukiiona nyumba yake pale Magomeni,
nje si nyumba ya maana, lakini ukiingia ndani utashangaa. Nyumba imejengwa
chini ya ardhi (underground). Huko kuna maisha ya peponi.
“Kule
chini ya ardhi ana bwawa kubwa la kuogelea huko huko, baa na magari yote ya
kifahari yapatayo manane tuliyakuta huko chini ya ardhi, tulistaajabu,” anasema
mmoja wa watu waliofanya kazi ya kumkamata.
Magari
yaliyokuwa huko chini ya ardhi mengine yana thamani ya hadi Sh milioni 500.
JAMHURI limefanikiwa kupiga picha sehemu ya magari hayo katika Kituo cha Polisi
Oysterbay, ambayo yamo BMW X6, Lexus, Lumma CLR RS, Cooper na mengine ya
kifahari.
Wakati
Lwitiko akikamatwa na baadhi ya mali zake, Hemed alikamatwa na gari moja ambalo
nalo pia linashikiliwa katika kituo hicho.
Watuhumiwa
hao waliokamatwa wanatajwa kuwa wamekuwa wanauza dawa aina ya heroine kutoka
Pakistan; cocaine kutoka Brazil, huku wakiishi maisha ya kifahari nchini
Tanzania na Afrika Kusini.
Katika
kinachohofiwa kuwa taarifa zimevuja ukamataji ulipoanza wiki iliyopita, kundi
kubwa la wafanyabiashara waliolengwa lilikimbia nchi.
“Wengi
wamekwenda Kenya na Afrika Kusini. Weengine wameikimbia Dar es Salaam, taarifa
za kiintelijensia zinaonyesha wako mikoani, lakini kwa vyovyote vile chini ya
Rais [John] Magufuli wanapoteza muda. Watakamatwa tu,” amesema mtoa habari
wetu.
Kamanda
wa Polisi Kanda ya Kinondoni, ACP Christopher Fuime, anasema ukamataji huo ni
endelevu, lakini hakutaka kuingia kwa undani zaidi akisema wananchi wasubiri
kuona ‘wazungu wa unga’ wote wanapotea mtaani.
Anasema
kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya si watu wadogo, bali wana uwezo na
wanamiliki mtandao mkubwa, hivyo kukabiliana nao kunahitaji “muda na usiri
mkubwa”.
Alipoulizwa
ni lini wanatarajia kuwafikisha mahakamani ‘mapapa wawili’ waliokamatwa,
amesema hawezi kuzungumzia hilo kwani upelelezi bado unaendelea na kwamba
unahusisha taasisi nyingi, hivyo ni vigumu kubainisha hilo.
Hata
hivyo, amekiri kukamatwa kwa Horohoro na Lwitiko na anasema: “Hapa tunafuatilia
mambo mengi. Tunavyopeleleza kesi za dawa za kulevya tunaangalia umiliki wa
mali, utakatishaji wa fedha, na mambo mengine mengi. Ila kwa sasa tumeamua
ingawa wengine wanakimbia baada ya kubonyezwa, lakini hiyo siyo tatizo,”
anasema Kamanda Fuime.
Katika
eneo la kutakatisha fedha za dawa za kulevya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini
kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanamiliki mabasi yanayofanya
kazi ya daladala jijini Dar es Salaam na mengine yanakwenda mikoani.
“Mabasi
haya mengi yanatoka Mbagala kwenda Posta, yameandikwa jina la moja ya taasisi
kubwa za uzalishaji mafuta duniani, na pembeni yameandikwa majina yao kwa
kuongeza herufi mbili mwishoni tu zisomekazo ‘so’. Huyu anaingiza hadi kilo 500
ze heroine kutoka Pakistan, na fedha anazopata anazitakatisha kwa kuonyesha
anafanya biashara ya daladala na mabasi ya mikoani,” amesema mtoa habari wetu.
“Wiki
iliyopita, Wapakistani sita wameingiza kilo 500 za heroine, wakahifadhi robo
Segerea jijini Dar es Salaam, nyingine zimehifadhiwa Pemba, nyingine Zanzibar
na nyingine zipo kwenye boti majini hazijaingia nchini,” kiliongeza chanzo
chetu.
Ukiacha
magari, wanaouza dawa za kulevya wanajenga majengo makubwa katika miji ya Dar
es salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza, Tanga na Mbeya, kisha wanatumia majengo
hayo kudanganya umma kuwa fedha zao zinatokana na kodi ya pango.
Kamanda
Fuime, alipoulizwa mkakati wa kupambana na wauzaji waliotajwa kuikimbia nchi,
amesema kuzungumzia hilo ni sawa na kuanika mipango ya polisi; jambo ambalo si
sahihi.
Miezi
miwili iliyopita polisi nchini walifanya uhamisho kwa askari wa Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni na Tanga kuvunja mtandao wa uhalifu, hususan dawa za
kulevya ndani ya Jeshi hilo.
Asilimia
kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu wapo jijini Dar es Salaam, hasa
maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach.
Waziri
Kitwanga ameshakabidhiwa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara hiyo
haramu ambako majina hayo aliyakabidhi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),
Inspekta Jenerali Ernest Mangu.
Baada
ya IGP Mangu kukabidhiwa majina hayo, aliwataka askari wa Oysterbay kumkabidhi
orodha ya majina ya wauza ‘unga’ haraka.
Mpango
huo ulienda sambamba na kuwapangua baadhi ya polisi walioonekana kushindwa
kuukabili mtandao wa wauza ‘unga’.
Maofisa
waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni Camillius
Wambura, aliyepelekwa Manyara na Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya
askari wa kitengo cha upelelezi na wengine kutoka idara mbalimbali.
Kuhamishwa
kwao kulitokana na kushindwa kwao kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini,
kiasi cha kuifanya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazojihusisha na
biashara hiyo kwa kiwango cha juu.
Awali,
kabla ya matukio hayo, Tanzania ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia dawa
za kulevya kwenda Afrika Kusini, Ulaya na Amerika, lakini kadri siku
zinavyokwenda inakuwa soko la dawa hizo.
Kinachotokea
vijana wengi mitaani wanaoitwa mateja, ndiyo wenye kufanya kazi ya kuiba na
kupora vitu vya watu mbalimbali. Fedha wanazopata wanazitumia kununua ‘kete za
dawa’ na kuzitumia.
Kundi
hili limeongezeka, na inaelezwa kuwa wafanyabiashara vijana wa kundi la kati
wengi sasa wanatumia dawa za kulevya na hilo ndilo linachangia magari mengi
kuwekewa ‘tinted’, kwa nia ya kuficha maovu.
Serikali
ya Awamu ya Nne, iliamua kupambana na dawa za kulevya kwa kubadili sheria na
ikaelekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, lakini hadi leo
chombo hicho hakijaundwa.
Ukiacha
kutoundwa kwa chombo hicho, wafadhili walikuwa wakitoa fedha za kununulia dawa
ya methodine kwa ajili ya vijana walioathirika na dawa za kulevya, lakini
maofisa waliopo katika Tume ya Dawa za Kulevya wakaishia kuzifuja na hivyo
mradi ukafutwa.
Matumaini
makubwa ya Watanzania sasa yapo mikononi mwa Rais Magufuli, kwani inaelezwa
kuwa yeye hana ushirika na wafanyabiashara ambao baadhi yao wanafanya biashara
ya dawa za kulevya.
“Tunachosema,
Rais sasa achunguze wanaomiliki mabasi, majumba makubwa na biashara
zisizoelezeka mitaji yake ilipatikanaje, kisha kuanzia hapo atajua kina nani
wanafanya biashara haramu na kina nani wanatumia biashara kutakatisha fedha za
dawa za kulevya,” ameshauri mtoa habari wetu.
Gazeti
la JAMHURI limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vilivyo mstari wa mbele
kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Mwezi uliopita lilichapisha orodha
ya wauza unga 560 wanaofanya biashara hiyo nchini, na ambao wengi wao wapo
mikononi mwa dola kwa sasa.
Hata hivyo, kumekuwapo
madai kuwa wanaokamatwa wengi ni wachuuzi wa chini na wa kati, lakini wahusika
wakuu wanaogharimia biashara hiyo, wakiwamo viongozi serikalini na katika
vyombo vya dola, wakiwa hawajakamatwa.
No comments: