CCM inatikiswa Z’bar
MSIMAMO wa Chama cha
Wananchi (CUF)
kutoshiriki uchaguzi uliovurugwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC) kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado unatikisa, anaandika
Faki Sosi.
Taarifa ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, yapo makundi mawili
ambayo kwa sasa yamekuwa mwiba; moja likiamini kurudiwa kwa uchaguzi huo na
lingine likionesha hofu kutokana na msimamo wa CUF.
Hata
hivyo, makada wa chama hicho wanaonesha hasara na hofu endapo mtikisiko wa
kisiasa uliopo sasa utaendelea kupuuzwa na Serikali ya CCM.
“Tunakwenda
lakini tuna hofu kubwa,” amezungumza mmoja wa makada aliyeomba kuhifadhiwa jina
lake kutokana na nafasi yake ndani ya chama hicho na kuongeza “sijui kama
tutavuka salama.”
Mohammed
Yusuf Mshamba, aliyekuwa miongoni mwa wasaka kuteuliwa kugombea urais ndani ya
CCM mwaka 2010 visiwani Zanzibar ameonesha mashaka kutokana na hali ilivyo sasa
visiwani humo.
Akizungumza
na mtandao huu leo Mshamba amesema,marudio ya uchaguzi yanaweza kuhatarisha
amani kwa kuwa hakuna makubaliano kati ya vyama vikuu visiwani humo.
Na
kwamba, idadi kubwa ya Wazanzibari hawako radhi kuona nchi hiyo inaingia kwenye
uchaguzi mwingine mbali na ule wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.
“Uchaguzi
wa awali ulifutwa kinyume na katiba na kuitishwa kinyume na katiba,” amesema na
kuongeza “Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha hakuwa na ushahidi wa
kutosha wa kufuta uchaguzi huo.”
Mshamba
amesema kuwa, uchaguzi uliofutwa umelisababisha taifa kuingia kwenye matatizo
ya kikatiba na kwamba, Jecha hakuwa na sababu za msingi za kufuta uchaguzi huo.
Akikumbusha
uchaguzi wa mwaka 2000 amesema kuwa, ulikuwa unahitilafu za wazi ambapo majimbo
takribani 16 yalirudiwa uchaguzi lakini haukufutwa uchaguzi wote.
“Nimeshangazwa
na uhalali wa matokeo ya Rais wa Jamhuri yaliyotokana na uchaguzi huo amabao
ulikuwa chini ya uangalizi mmoja na uharamu wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar,
Wawakilishi, na Madiwani.
“Tumepiga
kura tano mwaka jana 25 Oktoba ya Rais wa Muungano wa Tanzania, Rais wa
Zanzibar, Wabunge wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Wawakili na Madiwani
(Masheha), iweje matokea ya kwenye uchuguzi uleule mengine yawe halali na
matokeo mengine yasiwe halali? Alihoji Mshamba.
Mshamba
amesema, yeye anaamini kwenye mazungumzo ingawa wakuu wa vyama vya siasa
vilivyokinzana kwenye uchaguzi marudio ya uchaguzi walikutana takribani mara
nane lakini mazungumzo yaligonga mwamba.
Hata
hivyo amesema, mgombea urais ambaye amesimamishwa au kufukuzwa uwanachama na
chama chake, hapaswi kuwa mgombea wa nafasi yeyote kwa mujibu wa katiba pia
hana haki ya kupewa ulinzi.
“Huwezi
kuwa mgombea bila kuwa mwanachama wa chama chochote, hii haiwezekani lakini
unapoona mambo haya yanalazimishwa mwenye akili timamu atajua nini kinatafutwa
hapo.”
Juma
Said Makame Mkazi wa Donge ameuambia mtandao huu kwamba, kilichofanywa na ZEC
ni sawa na mtu mkubwa kujifanya mtoto.
“Mfano
wa uchaguzi uliofutwa ni sawa na mtu kuwa na sufuria la wali, halafu unatoa
wali wa juu kwamba ni msafu lakini wa chini una kinyesi.
“Hivi
ukiambia wa chini ulikuwa na kinyesi na huu wa juu hauna, je unaweza kula
chakula hicho? Yaani inakuwaje matokeo yaliyohusu bunge na urais bara yawe
sahihi na yaliyohusu Zanzibar yawe haramu?” ameshoji.
Kufutwa
kwa uchaguzi Zanzibar tarehe 28 Oktoba mwaka jana kumeibua sintofahamu na hata
kufikiriwa kuibuka kwa vurugu pale uchaguzi huo utapolazimishwa kufanyika tarehe
20 Machi mwaka huu.
No comments: