Rais kikwete atoa nishani kwa maofisa wa majshi

RAIS Jakaya Kikwete amewatunuku nishani za utumishi uliotukuka, utumishi mrefu na tabia njema maofisa wa majeshi mbalimbali 30. Kati ya maofisa hao, 10 ni kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), 10 kutoka Jeshi la Polisi na 10 wengine wanatoka Jeshi la Magereza.
Akiwataja maofisa waliopata nishani za utumishi uliotukuka, Mkurugenzi wa Shughuli za Ikulu Julius Magore, alisema nishani hiyo hutunukiwa kwa maofisa walio hai wa cheo cha Meja kwenda juu kwa JWTZ na kwa Polisi hutolewa kwa Mrakibu au maofisa Waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliotimiza si chini ya miaka 20.
Waliotunukiwa nishani hiyo ni Meja Jenerali Yacub Mohammed, Brigedia Jenerali Jacob Kingu, Kanali Fadhil Nondo, Luteni Kanali Ian Haule, Kamishna wa Polisi Elice Mapunda, Naibu Kamishna wa Polisi Samson Kasala, Rashid Omar, Mohammed Mpinga na Gaston Sanga.
Wengine ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gideon Nkana, Augustine Mboje na Venant Kayombo. Aidha, Magore alisema Nishani ya Utumishi Mrefu hutunukiwa kwa maofisa walio kwenye utumishi hai wenye Kamisheni wa JWTZ na maofisa waliotangazwa gazetini wa Polisi, Magereza na Idara ya Usalama wa Taifa waliotimiza utumishi wa miaka isiyopungua 15 wakiwa wenye tabia njema ya kuweza kusifiwa.
Aliwataja maofisa waliotunukiwa nishani hiyo kuwa ni Kanali Mary Hiki, Kanali Msafiri Hamisi, Meja Bernard Mlunga, Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola, Naibu Kamishna wa Polisi Ally Lugendo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mboje Kanga, ACP Vincent Marissa, Bakari Ndembo na Vincent Karata.
Aidha, alisema Nishani ya Utumishi Mrefu na Tabia Njema hutunukiwa kwa maofisa wasiokuwa na kamisheni walio katika utumishi wa JWTZ na wakaguzi, wakaguzi wasaidizi, stesheni sajini, sajini na koplo wa polisi na magereza.
“Wanaotunukiwa nishani hii ni wale waliotumikia jeshi mfululizo kwa muda usiopungua miaka 15 katika vyeo hivyo watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliotumikia idara hizo mfululizo kwa tabia ya kuweza kusifika,” alisema.
Aliwataja waliotunukiwa kuwa ni Ofisa Mteule Atilio Mgimbe, Sajini Taji Banda, Sajini Taji Haji, Inspekta Ally Haji, Sajini Charles Simon, Staff Sajini Asia Maji, Inspekta Msaidizi Rukia Mopey, Sajini Yasin Msangi na Sajini Regina Elias.
-HABARI LEO

No comments:

Powered by Blogger.