MGOMBEA MWINGINE UBUNGE AKATALIWA MBELE YA LOWASSA, SOMA HAPA

Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa jana alimwomba mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Dk Emmanuel Makaidi kujitoa kugombea ubunge katika Jimbo la Masasi na kumwachia mgombea wa CUF, Ismail Makombe baada ya kukataliwa na wananchi.

Uamuzi huo ulifikiwa katika Uwanja wa Bomani mjini Masasi, baada ya Lowassa kuwasimamisha wagombea hao jukwaani kuwanadi, lakini akapata upinzani mkali kutoka kwa wananchi alipompa nafasi Dk Makaidi.

Lakini kabla Makaidi hajasema chochote aliondoka katika mkutano huo na meza kuu ilijadiliana, ndipo mke wa Makaidi, Modesta aliposhauri waachwe wote wawili wachuane hoja ambayo ilikubaliwa na Lowassa ambaye alitangaza tena kuwa wagombea hao kila mmoja atapambana kivyake.

Awali, Lowassa alipotoa uamuzi wa kumuomba Dk Makaidi amwachie kijana huyo, uwanja mzima ulilipuka kwa nderemo na vifijo huku wananchi wakinyoosha mikono juu kuonyesha kukubaliana na uamuzi huo.

Hata hivyo, alivyobadilisha uamuzi huo, umati huo ulionekana kutomuunga mkono.

Lowassa alifika katika mkutano huo saa 7.28 mchana akitokea Mtwara baada ya kushindwa kufanya mkutano Tunduru kutokana na helikopta kukosa mafuta yaliyokuwa yameagizwa Dar es Salaam na yalipopatikana aliamua kwenda moja kwa moja Masasi.

Ilivyokuwa
Dk Makaidi alipopewa nafasi ya kuzungumza, wananchi walipiga kelele huku wakionyesha mikono juu kumkataa na kukatisha hotuba aliyokuwa ameanza kuitoa.

Lakini aliposimamishwa mgombea wa CUF, Makombe maarufu kama Kundambanda, alishangiliwa huku akimweleza Lowassa kuwa kura zake za urais anazo mfukoni kwa kuwa ndiye wananchi wanayemkubali.

Mgombea wa Chadema katika jimbo hilo, Mussa Sakaredi alijitoa ili kumuunga mkono mgombea aliyepitishwa na Ukawa.

Ndanda yaleyale
Kama ilivyokuwa Masasi, katika Jimbo la Ndanda, pia mgombea mmoja kati ya wawili wa Ukawa waliojitokeza kuwania ubunge alikataliwa na wananchi mbele ya Lowassa na kumfanya alikimbie jukwaa.

Hali hiyo ilijitokeza pale Meneja Kampeni wa Chadema, John Mrema aliposema anafahamu kuna mgogoro wa nani atakayegombea ubunge chini ya mwamvuli wa Ukawa kati ya NLD na Chadema, hivyo akatoa nafasi kwa kila mgombea kueleza matatizo ya jimbo hilo jipya.

Mgombea wa NLD, Angelous Gabriel alipopewa nafasi aliishia kumsifia Lowassa, jambo lililowafanya wananchi kupiga kelele wakisema anapoteza muda.

“Toka unapoteza muda, tokaaaaa,” walisikia wakipaza sauti.

Ilipofika zamu ya mgombea wa Chadema, Cecil Mwambe uwanja mzima ulilipuka huku akieleza kuwa katika jimbo hilo kuna tatizo la bei ya mazao, hivyo kama Lowassa akiingia madarakani, serikali yake iwatatulie matatizo yao.

Baada ya Mwambe kusema hayo wananchi walimshangilia na Lowassa alipopanda jukwaani aliwaita wagombea wote wawili na kuwahoji wananchi wanamtaka nani kati yao ambapo kwa sauti ya pamoja walijibu “Mwambeeeeeeeee”

Jambo hilo lilimfanya Gabriel wa NLD kushuka jukwaani na kuondoka. Alipoulizwa sababu ya kukataliwa alisema: “Kuna watu wameandaliwa na kununuliwa ili nisigombee Ndanda.”

Hata hivyo, wakazi wa Ndanda waliohojiwa walisema hawamjui mgombea huyo na wanashangaa kwa nini anang’ang’ania kugombea huku wakisema hajajiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo, jambo ambalo Gabriel alikiri.

Mmoja wa wakazi hao, Charles Mtutu alisema: “Hatumjui hata jina na NLD haina kiongozi katika jimbo hili na hawajawahi kufanya mikutano.”

Mkazi mwingine, Athuman Hassan alisema: “Kwanza hatumjui, pili hajawahi kufanya kampeni zozote tangu Jimbo la Ndanda lilipopatikana.

No comments:

Powered by Blogger.