JK ampongeza Magufuli kwa fikra, mabadiliko
RAIS Jakaya Kikwete amesema ni jambo jema kwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli kueleza fikra na matumaini ya kuleta mabadiliko katika uendeshaji wa Tanzania tofauti na uendeshaji ulivyo chini ya uongozi wake.
Amesema anatamani muda uende kwa kasi ili akabidhi madaraka ya kuongoza Tanzania kwa Rais wa tano ili yeye apumzike baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo amesema ni mzigo mkubwa.
Rais Kikwete aliyasema hayo mapema wiki hii wakati alipozungumza na wafanyakazi wa taasisi nne za Marekani ambazo zimefanya kazi na Serikali yake katika miaka 10 ya uongozi wake alipokuwa mjini Washington, D.C, wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Taasisi hizo ni taasisi za National Democratic Institute (NDI) International Republican Institute (IRI) International Foundation for Electoral Systems (IFES) na United States Institute of Peace (USIP).
Wafanyakazi wa taasisi hizo walimuuliza Rais Kikwete hakuna tatizo kwa mgombea urais kwa chama chake kukosoa baadhi ya mambo yaliyofanyika au yanayofanyika katika utawala wake.
“Wamepata kuja watu kwangu… wakaniambia kuwa mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji wake kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia hili analofanya mgombea wetu ni jambo sahihi kabisa na lazima afanye hivyo,” alisema Rais Kikwete.
Aliwaambia nchi inahitaji mawazo mapya na mwelekeo mpya ulio tofauti na uongozi wake na asiporuhusu jambo hilo kufanyika, nchi itabakia pale pale ambako ameifikisha yeye. Alisema hayo yatakuwa makosa makubwa kwa sababu nchi lazima isonge mbele kwa mawazo mapya, uongozi mpya na staili mpya ya uongozi.
“Haya ndiyo anayoyasema mgombea wetu, vinginevyo ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari kukubali kuwa kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na namna yake ya kuongoza na kuendesha nchi yetu,” alifafanua Rais Kikwete.
Dk Magufuli katika kampeni zake amekuwa akikosoa masuala mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa dawa hospitalini wakati madukani zipo, utoaji wa huduma za elimu, pembejeo kwa wakulima na masuala mengine.
Wakati Rais Kikwete akiyasema hayo, Dk Magufuli anaendelea na kampeni zake mkoani Shinyanga leo, baada ya kumaliza Geita huku msimamo wa kusema ukweli ukionekana kumbeba kisiasa katika mikutano anayohutubia.
Magufuli ambaye amemaliza ziara mkoani Geita jana, chini ya kile anachosisitiza kuwa hawezi kuahidi uongo, amekuwa akipangua baadhi ya hoja na ahadi za mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jambo linaloongeza na kumpandisha chati katika majukwaa ya kampeni.
Katika kuaminisha wapiga kura juu ya msimamo wake, Magufuli amekuwa akiweka wazi juu ya mambo au vitendo anavyochukia bila kujali kundi la watu linaloangukia eneo hilo watamnyima kura.
Kuhusu mambo anayochukia katika mikutano mbalimbali aliyoifanya mikoa ya Tabora, Kigoma, Kagera na Geita, Dk Magufuli amekuwa akikemea mafisadi na watumishi wazembe kwa kutamka bayana kuwa anaamini pia wanamchukia.
Amewataka watu wa namna hiyo wakae sawa kwa kile anachosisitiza kwamba akiingia madarakani, atakomesha vitendo hivyo kwa ajili ya kuiletea Tanzania maendeleo. Kwa upande wa ahadi, Magufuli amebainisha msimamo wake kuwa hawezi kufanya ushawishi wa kupata kura kwa kusema uongo au kuahidi mambo yasiyowezekana kutekelezeka.
Magufuli amekuwa akishangiliwa katika mikutano mbalimbali pale anapotamka kwamba yeye ni mtu wa ukweli na mwenye kumaanisha kwa kila anachosema “Ni vyema nihukumiwe kwa mambo mengine lakini kwa kusema uongo, hapana.
Msema kweli ni mpenzi wa Mungu…, na siyo kwamba naahidi haya kwa kuwa natafuta kura,” ni kauli ambayo amekuwa akiitoa kwenye maeneo mbalimbali wakati akitoa ahadi mbalimbali za kuhakikisha inapatikana Tanzania mpya.
No comments: