KESI YA UBAKAJI YA MBASHA, MUNGU AMETENDA!


 Emmanuel Mbasha akilia kwa furaha baada ya hukumu hiyo.
AHSANTE! Hatimaye kesi nzito na ngumu iliyokuwa ikimkabili Emmanuel Mbasha, mume wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha ya kumbaka shemeji yake, imemalizika juzi kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Ilala kumwachia huru na yeye mwenyewe kutamka kuwa Mungu ametenda!

KISA KIZIMA
Emmanuel ambaye awali alikuwa na mgogoro wa kifamilia na mke wake, Flora Mbasha, alipelekwa mahakamani na msichana wake wa kazi, aliyekuwa na umri wa miaka 17 wakati huo, akidaiwa kumbaka, huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Katika shitaka la kwanza, Mbasha alidaiwa kuwa Mei 23, 2014 alimbaka shemeji yake huyo katika eneo la Tabata Kimanga na katika shtaka la pili, alidaiwa kufanya kosa hilohilo kwa mtu huyo huyo ndani ya gari aina ya Toyota Ipsum wakati akitoka kumtafuta mkewe, Flora.
Hakimu Flora Mujaya aliyetoa hukumu hiyo majira ya saa 4: 37 alisema kwa mujibu wa sheria juu ya madai hayo, Mbasha hana hatia na hivyo chombo hicho cha kutafsiri sheria kinamuachia huru.
HALI KABLA YA HUKUMU
Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya kuwa karibu na Emmanuel Mbasha na kuzungumza naye kabla ya hukumu kusomwa huku uso wake ukionesha wasiwasi na woga wa wazi.Mara kwa mara, Mbasha ambaye pia ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, alisikika akinong’ona kuashiria kusali kwa kumuomba Mungu amuepushe huku akiwaomba watu waliokuwa wakimsalimia kumuombea juu ya hukumu hiyo akisema…. “Mungu atanisaidia, niombeeni jamani”.
MUDA WA KESI WAWADIA
Wakati mazungumzo yakikolea nje ya chumba cha mahakama, ghafla sauti nzito inayokwaruza na yenye mamlaka ilisikika ikilitaja jina la Emmanuel Mbasha kuwa anahitajika kortini na mwanahabari wetu aliushuhudia uso wake ‘ukisinyaa’ kwa hofu.
WAANDISHI WAPIGWA MKWARA!
Bila maelezo yenye kujitosheleza, askari polisi waliokuwa eneo hilo waliwazuia waandishi wa habari kusogea karibu na chumba cha mahakama kusikiliza kesi hiyo, nao walilitii bila shuruti.
HUKUMU YAKAMILIKA
Wakati wanahabari wakiwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya kesi hiyo iliyokuwa ikiendelea ndani ya chumba, mara Emmanuel Mbasha alionekana akitoka na moja kwa moja akaenda kupiga magoti mchangani huku akiangusha kilio, jambo lililoteka hisia za wengi.
ASALI BABA YETU MWANZO MWISHO!
Akitambua kuwa hayo ni matokeo ya maombi yake kwa Mungu, mwimbaji huyo akiwa amepiga magoti mita chache kutoka chumba cha Pilato, Mbasha alisikika akisali mfululizo sala ya “Baba yetu uliye mbinguni…” huku akizidi kuangua kilio, kilichowalazimu baadhi ya watu wakiwemo mawakili wake, kumuondoa eneo hilo.
RISASI MCHANGANYIKO LAMTAITI!
Baada ya Mbasha kuangua kilio chake cha furaha iliyochanganyika na uchungu, gazeti hili lilimfuata na kuzungumza naye kwa muda mchache na alimshukuru Mungu kwa kumnusuru na msala huo mzito.
“Sina cha kuzungumza kwa sasa, namshukuru sana Mungu wangu wa mbinguni kwa kuninusuru na hili, hakika ametenda, nawashukuru ndugu, rafiki, jamaa na mashabiki wangu kwa kuwa nami karibu katika kipindi chote cha maumivu haya, nashukuru,” alisema Mbasha huku akijifuta machozi na jasho jingi lililokuwa likimtiririka.
 Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha.
AWAZUNGUMZIA MKEWE, GWAJIMA
Katika mazungumzo na mwandishi wetu muda mfupi kabla ya kuitwa kwa kesi hiyo, ambayo yalifanyika nje ya chumba cha mahakama hiyo, Mbasha alisema amepitia katikia kipindi kigumu sana cha kumuondoa moyoni mkewe, Flora huku akimtupia lawama nyingi juu ya madai ya kesi hiyo, ikiwemo kumdhalilisha.
Hata hivyo, Mbasha alikiri kumpenda kwa dhati Flora na kwamba mara nyingi alikuwa akimuomba warudiane na kurejesha uhai wa ndoa yao, jambo ambalo Flora hakutaka kabisa kulisikiliza huku akishinikizwa na ndugu zake ambapo Mbasha alisema hawakutenda haki kwa kile alichokiita… “wana roho mbaya”.
Mbali na madai hayo kwa Flora na ndugu zake, Mbasha pia aliweka wazi namna ambavyo aliwahi kumfuata mchungaji wa kanisa walilokuwa wakisali wanandoa hao la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima kwa lengo la kumuomba msaada juu ya ndoa yake, lakini badala yake, aliambulia maneno ambayo hakuyategemea kutoka kinywani mwa mtumishi huyo.
Bila kuyaweka wazi maneno hayo, Mbasha alisema mara nyingi Gwajima alionekana kuwa upande wa Flora huku akimwambia kwa uwazi kuwa …“Flora ameshaamua, heshimu msimamo wake” jambo ambalo lilimuumiza kwa kiwango kisichotamkwa.

No comments:

Powered by Blogger.