waliokopa HESLB walipe ili wengine wapate mkopo



BODI ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), inasema kwa miaka 10 tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 74.7
, ikiwa ni sehemu ya marejesho ya mikopo ya wanafunzi.
Kaimu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bertha Minja anasema, fedha zilizokusanywa ni za mwaka wa fedha 2014/15, na kwamba, kwa mwaka 2006/7 HESLB imekusanya Sh milioni 53.6. “Hii ni ishara kuwa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba bado tunaendelea kukusanya madeni tunayowadai wanafunzi na waajiri walionufaika na mikopo hii,” anasema Minja. Minja anayasema hayo wakati anatoa taarifa kwa wadau wa bodi katika sherehe za kumbukumbu ya miaka 10.
Anasema, licha ya changamoto zinazoikabili bodi hiyo, wametoa Sh trilioni 2.09 kwa ajili ya kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu vyuoni. Kwa mujibu wa Minja, awali bodi hiyo ilikuwa na wafanyakazi tisa lakini sasa wapo 135. Minja anasema, mwaka 2005 walianza kukopesha wanafunzi 42,000 na kwamba idadi hiyo imeongezeka kwa kuwa sasa HESLB inatoa mikopo kwa wanafunzi 963,661.
‘’Tulipewa jukumu la kukusanya kodi tangu mwaka 1994 na kwamba bodi ilianzishwa rasmi Julai, 2005 huku ukopeshaji ulianza mwaka 2006, tunajivunia mafanikio haya na tunaimani tutaendelea kuimarika zaidi,’’ anasema Minja. Minja anasema, kutokubalika kwa sera ya uchangiaji ni moja ya kikwazo kinachosababisha wanafunzi wengi kutokuelewa maana ya mikopo hiyo.
Anasema baadhi ya wanafunzi hawatambui maana ya gharama za mikopo hiyo hivyo kusababisha kutokubali sera iliyowekwa na serikali. Minja anasema, wanafunzi wengi wanafahamu kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya ruzuku, hivyo bodi inaendelea kuelimisha wanafunzi na umma kwa ujumla maana halisi ya fedha hizo ili wasiweke vikwazo. Anataja changamoto nyingine kuwa ni waajiri ambao hawawajibiki ipasavyo kulipia wafanyakazi waliokopa katika bodi hiyo.
Anasema wameomba ushirikiano kwa waajiri kurahisisha ukusanyaji madeni kwa wafanyakazi wao. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anasema, sera ya uchangiaji wa huduma za jamii ikiwemo uchangiaji wa elimu ya juu, ilianza mwaka 1993. Anasema, wanafunzi hao walikuwa wanalipia usafiri, ada ya mitihani chakula na mambo mengine ambapo serikali kupitia wizara zilizokuwepo wakati huo, ziliona ni vyema kuwepo kwa bodi ili kusimamia shughuli hizo.
Wakati wa kuanzisha HESLB, ilikuwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, chini ya Pius Ng’wandu na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, ilikuwa kuwa chini ya Profesa Peter Msolla. Dk Kawambwa anasema, wanafunzi wa kipindi hicho walikuwa wanalipia gharama hizo pale wanapoingia mwaka wa kwanza wa masomo. ‘’Kipindi kabla ya kuanza kwa bodi hii, wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wanalipia Sh 350,000 fedha ambayo ilikuwa kubwa ukilinganisha na kipindi cha sasa,’’ anasema.
‘’Serikali iliona kuwa wanafunzi wasio na uwezo wa kujigharimia wakopeshwe waweze kusoma na wakishaajiriwa, warudishe.’’anasema Waziri Kawambwa. Anasema, serikali imeongeza bajeti ya HESLB kutoka Sh bilioni 56.1 mwaka 2005 wakati mwaka huu imeipatia bodi hiyo Sh bilioni 341 kwa lengo kuboresha utendaji. Kiongozi huyo anasema, kuongezeka kwa bajeti hiyo ni sehemu ya kuongeza kasi ya kuwapatia wanafunzi wengi mikopo kwa lengo la kupunguza migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Anasema katika kipindi alichokuwa bungeni, amewawakilisha vyema na kuwapigania katika kuwaongezea bajeti na kwamba kiwango cha makusanyo ya mikopo hiyo kimekuwa kikiongezeka hivyo kuliletea Taifa faida.
Anawataka waajiri wote na wanafunzi walionufaika na mikopo ya elimu ya juu, kurejesha fedha hizo ili Watanzania wengine wanaohitaji wanufaike na mikopo hiyo. Dk Kawambwa anasema, waajiri wengi wamekuwa wakikaidi kuwalipia mikopo waajiriwa wao kitendo kinachokwamisha uendeshaji wa bodi hiyo. Anasema, endapo waajiri hao watalipa kwa wakati, wanafunzi wengine wataweza kunufaika na mikopo hiyo ambayo itawasaidia katika masomo.
‘’Ninawataka waajiri wote walionufaika na mikopo kurejesha ili wengine wanaohitaji waweze kunufaika na mikopo hiyo,’’ anasema Waziri Kawambwa. Anasema, baadhi ya wadaiwa sugu wameshitakiwa mahakamani na kwamba kesi bado zinaendelea. Anasema hatua hiyo imefikiwa baada ya waajiri hao kukaidi maombi waliyotumiwa na bodi kurejesha mikopo hiyo. ‘’Serikali itaendelea kuwasaidia kufanikisha shughuli zenu ili wanafunzi wengi zaidi wapate mikopo na wanufaike,’’ anasema Dk Kawambwa.
Anasema, serikali ipo katika mkakati wa kuongeza Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere ambacho kitakuwa cha Sayansi na Teknolojia huko, Butiama Musoma. Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega anasema katika sherehe hiyo kuwa, wamewakumbuka waanzilishi wa bodi hiyo ambao ni aliyekuwa Waziri wa Sayansi , Teknolojia na Elimu ya Juu, Pius Ng’wandu na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla.
Anasema wanatambua mchango wa makatibu wakuu wawili wa wizara hizo akiwemo Dk Naomi Katunzi pamoja na wadau ambao kwa pamoja wameshiriki katika mchakato wa kuundwa kwa bodi hiyo. ‘’Katika sherehe hii tunakumbuka mchango mkubwa uliotolewa na mawaziri wawili, makatibu wawili pamoja na wabunge, madiwani na wastaafu ambao walichangia uanzishwaji wa bodi hii,’’ anasema Nyatega.
Anasema, bodi hiyo imeadhimisha miaka 10 tangu Agosti Mosi, mwaka huu kwa kutoa huduma za jamii ikiwemo kutoa vifaa vya usafi katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Nyatega anasema, idadi ya vyuo imeongezeka kutoka 35 hadi 65 na wanaamini kuwa watatoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi kutokana na mafanikio waliyoyapata kwa kipindi cha miaka 10. Anasema mpaka sasa asilimia 45 ya wanafunzi wamerudisha mikopo hiyo kinyume na lengo la bod

No comments:

Powered by Blogger.