polisi kupeleka wapelelezi kenya juu watanzania wanaoshukiwa kuwa Al-Shabaab.
POLISI imesema inaandaa mipango ya kumtuma mtu nchini Kenya kwa ajili ya kupata taarifa kamili kuhusu, madai ya kukamatwa kwa Watanzania sita na kuhusishwa na ugaidi nchini Kenya.
Vyombo vya habari vya Kenya, viliripoti juzi kuwa Watanzania sita walikamatwa katika Mji wa Garissa nchini humo, wakiwa na bastola na mabomu saba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watanzania hao walikuwa wanakwenda Somalia kwa ajili ya kujiunga na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab.
Akizungumza na gazeti hili, kuhusu taarifa hizo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani, alisema hawajapata taarifa kamili kuhusu suala hilo, kutoka Kenya.
“Hatujapata taarifa kutoka Kenya kuhusu suala hilo, sisi tumelisikia kwenye vyombo vya habari. Lakini tunaandaa mipango ili tuweze kumtuma mtu Kenya ili kupata hali halisi kuhusu kukamatwa kwa watanzania hao,” alisema Athumani.
Juzi Mratibu wa Polisi wa Kanda ya Kaskazini Mashariki, Kenya, Mohamud Saleh, alipozungumza na waandishi wa habari katika mji wa Garissa, alisema wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 40, walikamatwa katika mji wa Daddab wakijaribu kuvuka mpaka kuingia Somalia.
Alisema watu hao wanashikiliwa katika mji huo wa Garissa ambako watahojiwa kupata taarifa zaidi. Aidha, alisema mapema wiki hii, wanawake wawili mmoja raia wa Kenya na mwingine wa Tanzania, walikamatwa wakienda Somalia kwa ajili ya kuolewa na wanaume wa Al-Shabaab
No comments: