Uchaguzi huu mbona natakoma

CHEKANAKITIMEYaani nimekaa hapa nakumbuka wimbo wa zamani wa NUTA Jazz band, ulikuwa unasema Nimuokoe nani. Mtumbwi unazama, ndani ya mtumbwi yuko jamaa na mkewe na mtoto na baba na mama yake, uwezo wake kumuokoa mtu mmoja sasa amuokoe nani? Na ndiyo yanayonikuta.
Kisa na mkasa ni demokrasia. Shangazi kachukua fomu ya ubunge wa chama kipya hata jina sijalishika na kapitishwa agombee, baba mdogo kapitishwa agombee kwenye chama mafuriko, mdogo wangu amepitishwa ubunge kwenye goli la mkono, babu amepitishwa udiwani chama gani sijui, mamdogo anapeperusha bendera ya Ubunge chama cha mchungaji, kali kuliko zote, yule mjomba wangu mlevi kuliko mtu yeyote kwenye ukoo anadai anachukua fomu ya urais, sasa haya yote yasingenisumbua tatizo wote wanataka niwaunge mkono.
Babu kanifuata uso kwa uso anataka hela za kuhonga wajumbe na za kufanyia kampeni, kasema niweke mahesabu akipata udiwani ananilipa na riba juu. Shangazi kanitumia kikaratasi kunikumbusha tu kuwa yeye ndiye dada’ke baba, hivyo nina wajibu wa kumchangia kwa hali na mali katika lengo lake la kupata nafasi ya kutetea haki za wanyonge.
Meseji ya baba mdogo ilikuja kwa simu inaonekana imekwenda kwa watu wengi maana haikunitaja jina ila inanikumbusha kuwa kama ndugu na jamaa nichangie kupitia namba yake ya simu kufanikisha azma ya kuwa mbunge.
Mdogo wangu katumia jukwaa la kifamilia, mama kasema lazima tumchangie mdogo wetu maana akiwa mbunge sisi wote ni kama tumekuwa wabunge na pia itakuwa ni mara ya kwanza familia yetu kuwa na mbunge ambaye tukiroga vizuri anaweza kuwa waziri, na mama kasema anatamani akifa awe japo ana mtoto waziri.
Lakini yote hayo tisa, kumi mimi niko chama kingine kabisa, chama cha utemi, sisi bwana ukitubishia tunakurushia mitusi, na ole wako upite mbele yetu umevaa jezi ya chama kingine ni matusi tu, sasa hawa ndugu zangu naona wanaongea mawenge tu.
Sisi ndio tutashinda viti vyote bungeni, na urais tunachukua nani anabisha? Ole wako ubishe. Hicho ndicho kipaumbele cha chama chetu. Chama letu hoyeeeeee.

No comments:

Powered by Blogger.