Wakala_Wa_Shetani - 4...




KWA TAARIFA ZAIDI NICHEKI HAPA 0785848566 
ILIPOISHIA;
“Ni kweli la..la..kini...” Mathayo hakumalizia kutokana na donge la uchungu kumkaba kooni huku machozi yakimdondokea mkewe.
SASA ENDELEA...
“Hakuna cha lakini, tumuachie Mungu ndiye aliyetupa kiumbe huyu, mbona kuna viumbe wasio na faida duniani wanaishi kwa furaha itakuwa mwanadamu. Mungu atamlinda mwanangu, nina imani atakuwa tu na siku moja kutoa ushuhuda hata kama wazazi wake tumetangulia mbele ya haki,” Ngw’ana Bupilipili alizidi kumpa moyo mumewe.
“Nashukuru mke wangu kunipa moyo.”
“Ni wajibu wangu, basi wahi ukaandae chochote kitu, njaa naisikia imeanza kunichonyota.”
Mathayo aliondoka kwenye maficho na kurudi nyumbani kumuandalia mkewe chakula kutokana na njaa kali iliyokuwa imemshika hasa baada ya kujifungua hakuwa ameweka kitu tumboni. Alipofika nyumbani alimchemshia uji na viazi ambavyo vilikuwa vimebaki jana yake. Haraka
haraka alianza kurudi shambani. Hakufika mbali mvua kubwa ilianza kunyesha.
Hakukubali kusimama, alitembea nayo huku akilowa kila kona ya mwili. Alipofika pangoni alimkuta mkewe akiwa amemkumbatia mtoto wake ambapo maji yalikuwa yameanza kuingia ndani ya pango.
Wasingeweza kutoka nje kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha kuwa kubwa. Mathayo alipofika aliingia mle pangoni alipokuwa mke wake na kiza kilianza kutanda huku baridi ikizidi kuwa kali.
Mvua nayo ilikuwa kama imetumwa kwani ilizidi kuongeza kasi ya kunyesha ikiambatana na upepo mkali. Maji yakazidi kuingia kwenye pango, kila dakika yalizidi kujaa na kuelekea mafutini huku Ng’wana Bupilipili akimkumbatia mwanaye na kuendelea kumuomba Mungu asitishe mvua ile kwani haikuonesha dalili za kukatika mapema.
Maji nayo yalizidi kupanda juu kuelekea kiunoni, mvua nayo ndiyo kama imechochewa kuni kwa jinsi ilivyokuwa ikinyesha kwa kasi huku upepo ukizidi kuvuma.
Walifikiria watoke nje ili wakimbilie kwenye makazi ambako kulikuwa mbali, waliamini wasingefika kwani wangeweza kuuawa hata na radi ambayo ilikuwa ikipiga kwa nguvu na upepo mkali.
Nje kulikuwa hapatamaniki kutokana na mvua na upepo mkali uliokuwa ukivuma hadi kuifanya baadhi ya miti kung’oka. Ilikuwa mvua ambayo haikuwahi kunyesha muda mrefu pale kijijini.
Pangoni maji nayo yalizidi kujaa na yalivuka kiunoni kuelekea kifuani. Ilibidi mtoto wamweke mabegani, hawakuacha kumuomba Mungu kila dakika ili kuwanusuru na janga lile zito ambalo lilikuwa lina kila dalili za kuchukua uhai wao.
Mvua nje iliendelea kunyesha na maji nayo kila dakika yalizidi kujaa mle pangoni. Yalivuka kifuani na kuanza kuelekea shingoni. Mathayo na mkewe waliamini kabisa hakukuwa na dalili zozote za kutoka salama. Ila Mathayo alikumbuka huenda mvua ile ni laana ya kumficha mtoto wao albino ambaye alionekana kama mkosi.
Wazo lake alifikiria kumtupa yule mtoto ili waangalie itakuwaje. Aliona ampe mkewe wazo aone atalipokeaje.
“Mke wangu nilikuwa na wazo.”
Wakati huo walikuwa wamekumbatiana huku mtoto wao wamembeba kichwani japokuwa walianza kuchoka kutokana na kuiweka mikono juu kwa muda mrefu.
“Wazo gani mume wangu? Siamini kama tutatoka salama, muda si mrefu maji yatatufunika. Ona sasa hivi yanakimbilia kidevuni...Eeeh, Mungu, sikiliza kilio chetu waja wako,” Ng’wana Bupilipili hakuacha kumuomba Mungu muda wote.
“Mke wangu nina wazo moja, japo huenda usiliafiki lakini nahisi ndilo litakaloyaokoa maisha yetu.”
“Wazo lipi mume wangu?” alisema huku akiyapuliza maji yaliyotaka kuingia mdomoni.
“Mimi nafikiria kabisa mvua hii si bure, huenda tumevunja mila na desturi.”
“Kuvunja kivipi?”
“Ni wazi huyu mtoto ni mkosi na hii mvua ni hasira ya mizimu.”
“Sasa hizo hasira zao sisi zinatuhusu nini?”
“Huenda wameamua kututia adabu kwa kiburi tulichokionesha kwao.”
“Sasa wewe ulikuwa na wazo gani? Naona muda si mrefu maji yatatufunika hata mikono imeishiwa nguvu kwa sababu ya kumshikilia mtoto kwa muda mrefu.”
“Kwa nini tusimtupe huyu mtoto?”
“Mume wangu unasemaje?” kauli ile ilimshtua Ng’wana Bupilipili.
“Tumtupe huyu mtoto ili kuyaokoa maisha yetu.”
“Tukishamtupa tupata nini?”
“Nina imani mvua itakoma na sisi kuokoka.”
“Mume wangu, maisha yako ni bora kuliko ya mtoto wetu?”
“Hapana mke wangu, siku zote vitu vya jadi si vya kuvipuuza, matokeo yake leo tunakufa tunajiona.”
“Mume wangu, kwa taarifa yako mtoto wangu siwezi kumtupa kama tutakufa basi tutakufa wote na kama kupona ni pamoja na mtoto wetu.”
“Mke wangu, unafanya mzaha, tutakufa huku tunajiona.”
“Hata siku moja siwezi kuua mwanangu, mimi ndiye ninayeujua uchungu wake. Kama tutakufa sawa lakini tukipona naomba uachane na mimi, nitajua jinsi gani ya kuishi na mwanangu,” Ng’wana Bupilipili alimjia juu mumewe.
“Mke wangu kwa nini hutaki kuwa mwelewa, mtoto nini? Tutatafuta mwingine lakini hatuwezi kuwa na bomu ambalo linatulipukia tumelikumbatia.”
“Kwani tatizo nini? We’ toka, niache peke yangu nife na mwanangu. Kama kufa nitaanza mimi kisha mwanangu atafuatia.”
“Mmh! Sawa nitafanyaje nawe umekuwa mbishi.”
“Siamini kumbe nawe ni walewale, basi wafuate ili waje wamchukue mtoto wangu wakamuue kama mlivyomuua mwanangu wa kwanza,” Ng’wana Bupilipili alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka.
Maji ya pangoni yalikuwa ya baridi na kiza kinene kilitanda mmle ndani kutokana na mvua ambayo ilianza kupunguza kasi yake. Lakini wingu lilikuwa bado zito likiambatana na baridi kali.
Waliendelea kuwemo mule pangoni, mtoto wao alikuwa bado yupo juu huku mikono yao ikizidi kuchoka. Nje mvua ilikuwa imekoma, hata maji kuingia pangoni yaliacha lakini bado maji yalikuwa chini ya kidevu.
Kutoka ndani ya pango ilikuwa vigumu kwa vile hapakuwa na sehemu ya kushika, pia giza la mle pangoni liliwafanya wasione njia ya kutokea nje.
Waliendelea kukumbatiana huku baridi la maji kilizidi kuwapiga, Ng’wana Bupilipili alianza kutetemeka kwa meno kugongana.

Itaendelea

No comments:

Powered by Blogger.