Rais Magufuli atema cheche ndege mpya
RAIS John Magufuli amezindua ndege mpya mbili za serikali zilizonunuliwa aina ya Bombardier Dash 8 Q400 huku akiwapasha wale waliokuwa wakibeza ununuzi wa ndege hizo, akitaka Bodi mpya ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutosita kuwafukuza kazi wafanyakazi watakaobainika kuhujumu kampuni hiyo.
Aidha, ametangaza kuwa serikali imeanza mazungumzo ya kununua ndege nyingine mbili mpya, ikiwamo itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 240.
Kwa upande wao, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imependekeza ndege hizo kuitwa ‘Hapa Kazi tu’ iwapo Rais ataridhia jina hilo kwani serikali haijanunua ndege mpya tangu mwaka 1978. Ndege hizo zitakodishwa kwa ATCL.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1), Dar es Salaam, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Makatibu Wakuu na Mawaziri wa wizara mbalimbali.
Rais Magufuli alisema watu wengi wamekuwa wakibeza ununuzi wa ndege hizo zilizotengenezwa nchini Canada na wakati mwingine alifikiria kwa nini aliamua kufanya jambo hilo; kwani wengine wamekuwa wakisema haina spidi na wengine kuwa ni mkweche, jambo ambalo siyo la kweli na kusema watu hao watakuwa wa kwanza kupanda kwani zinatumika na nchi nyingine kama Marekani wanazo 40 na pia Ethiopia.
“Wengine walilalamika kwa nini tumenunua kwa fedha taslimu, sasa mtu ukiwa tajiri kwa nini usinunue ‘cash’, kwa nini ukopeshwe ili watu wapate faida, kuna fedha za Watanzania na wanataka ndege ndiyo maana tukanunua ‘cash’, ” alisema Rais Magufuli.
Alisema ndege hizo ni nzuri na ukitaka kujenga uchumi wa kisasa lazima uwe na ndege na ukitaka kuwa na watalii hakuna sababu ya kuwafanya waende kwenye nchi nyingine ili waje nchini mwenu lazima ziwepo ndege.
Rais Magufuli alisema kwa ndege ya aina ya Jet kutoka Dar es Salaam kwenda Songea unatumia mafuta ya Sh milioni 28.5 lakini ukitumia ndege hizo mpya unatumia Sh milioni moja kwa umbali huo wakati kufika tofauti yake ni dakika 20 tu.
Alisema wanaopiga vita ni wafanyabiashara, hivyo kama wanataka spidi wakapande za jeshi ili wafike haraka wanapotaka kwani inafanyika biashara lazima kuangalia mazingira yote na viwanja vyote kutumika.
Alisema nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ni Sh 800,000 lakini hizi hazitafika huko na uzuri wa ndege hizo zitatua katika viwanja vya ndege vya mazingira yote nchini.
Rais aliwaomba Watanzania kutopuuza vitu vyao na kama hataki ni kukaa kimya na kuacha kiherehere na kuzoea kusifia wengine na kuhoji, kwa nini wasisifie vya kwao kwani ndege hiyo itatumika na watu wa itikadi mbalimbali kwa kuwa ni ya Watanzania.
“Ni lazima Watanzania kujifunza kujivunia vya kwao… lazima mfahamu kwa kulipa ndege hizo polepole tungelipa gharama kubwa tofauti na tulivyolipa fedha taslimu, tumepunguza gharama na tuna mpango wa kununua ndege mbili kubwa na fedha zipo,” alisema.
Alieleza kuwa ndege hizo ipo itakayokuwa na uwezo wa kubeba watu 160 na nyingine 240 na kwamba yalipofanyika majadiliano wahusika walikuwa wanaweka muda mrefu kwa kusema ndege ya abiria 240 italetwa mwaka 2021, lakini tunajadiliana ili kuzipata mapema na fedha zipo.
Alisema ndege hizo zikinunuliwa itaondoka Dar es Salaam mpaka Marekani, China bila kutua na itawawezesha watalii kutoka nchini mwao na kuingia moja kwa moja hapa nchini bila kupitia nchi nyingine. Alitaka wizara kuendelea na mchakato kwa kuitisha kampuni ili uwepo ushindani na kununua kwa bei nafuu kwani wananunua kwa fedha taslimu.
Alisema ndege hizo mbili mpya zilizozinduliwa jana wanazikodisha kwa ATCL na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kutengeneza bodi nzuri ya wasomi wakati Mkurugenzi Mkuu wa ATCL akitokea nchini Senegal alipokuwa akifanya kazi huko hivyo mwendo wa kucheza umekwisha.
Alielezea baadhi ya vitu vilivyofanya ATCL kutofanikiwa kuwa ni pamoja na kutokuwa na mfumo wa kujiendesha kwa kujitegemea kibiashara muda wote kutegemea serikali, kubweteka kwa wafanyakazi wake, hujuma ya wafanyakazi, kutengeneza hasara za ajabu ajabu, mafuta hewa kwa kudanganya ndege imesafiri, lakini kumbe bado iko hapo hapo pamoja na kujilipa malipo ya ziada.
Aliwaomba bodi na wizara kutokuwa na huruma kwa wasiofaa kwa kuwafukuza kazi kwa kuchambua kweli kweli na kuwachekecha ili kupata watu wanaotaka kubadilika na kuwaomba wafanyakazi wanaotaka kufanya kazi kweli kujisalimisha.
“Nakueleza waziri usiogope kupunguza wafanyakazi kama tulipunguza NIDA 600 hatuwezi kushindwa hawa 200 kwa ambaye hawezi kwenda na spidi yetu atupishe na kwenda na waliojipanga kwenda kwa spidi tunayotaka wengine wape fedha zao wapumzike, kwani tunataka siku moja shirika hili liwe na ndege hata 10,” alisema.
Aliomba uongozi wa ATCL kutotumia mawakala kukatisha tiketi ila wazingatie huduma watakazotoa na huku akikosoa sare za wafanyakazi ambazo alisema zinatia kichefuchefu na kuwataka kujipanga vizuri ili walipakodi waone matunda yake.
Aliomba pia bodi na menejimenti kutoruhusu kiongozi wa serikali kusafiri bure hata kama ni yeye au waziri wa wizara hiyo au bodi kwani kuna wakati wanakuwa wanajipendekeza wakati wanatakiwa kufanya biashara.
Akizungumzia uboreshaji wa Reli ya Kati, Rais Magufuli alisema kwa sasa ujenzi wa reli mpaka Mwanza na Isaka mpaka Burundi zabuni zimetangazwa na fedha zipo.
Alisema kwa reli ya zamani umepatikana mkopo kutoka Benki ya Dunia na mabehewa yameongezeka na siku zijazo Dar es Salaam itakuwa na treni ya umeme kwani haya yanawezekana siyo Ulaya tu hata hapa nchini yatafanyika.
Akizungumzia ununuzi wa ndege hizo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mara ya mwisho kwa serikali kununua ndege mpya ilikuwa 1978 na shirika lilikuwa likitumia ndege za kukodisha na kusababisha madeni.
Akizungumzia sifa za ndege hizo mpya, alisema ni miongoni mwa ndege za kizazi kijacho na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kutumia mafuta kidogo huku zikitua viwanja vyote nchini vya lami na visivyokuwa na lami.
Alisema ndege hizo kila moja ina uwezo wa kubeba mizigo tani 1.6 na abiria 76 na kati yao sita wanabebwa katika daraja la kibiashara na katika hatua za awali wamejipanga kutoa huduma katika viwanja 12.
Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya, Mtwara na Comoro huku wakiendelea na upembuzi yakinifu ili kuongeza viwanja vingine ili ndege ziweze kutua.
Alimpongeza Rais kwa uamuzi wa kununua ndege hizo na kuonesha kuwa ni kiongozi wa vitendo kuliko maneno na wanapendekeza ndege hizo kama rais ataridhia ziitwe ‘Hapa Kazi Tu’.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema uamuzi wa kununua ndege za aina hiyo ulifanyika kwa kuzingatia sifa za kutua na kuruka katika viwanja vya lami na visivyo na lami, kutumia mafuta kidogo kwenda umbali mrefu hivyo gharama za uendeshaji kuwa ndogo.
Alisema ndege hizo zina uwezo wa kubeba mzigo mkubwa na injini zenye kazi hivyo kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga na unafuu wa bei na kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji.
Balozi Kijazi alisema ndege hizo ni za serikali na siyo za ATCL hivyo wataingia mkataba kwa kukodisha ndege kwa kampuni hiyo na kuzilipia hivyo lazima kampuni hiyo kujipanga kuingia katika ushindani wa usafiri huo.
No comments: