Polisi ‘wajitosa’ sarakasi za CUF
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, linadai kuwakamata watuhumiwa 22, waliojitambuulisha kama wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiwa na zana za kufanyia uhalifu ikiwemo mapanaga na visu,
Simon Sirro, Kamishina wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya askari kupata taarifa kwamba, wamekuja Dar wakitokea Zanzibar kwa ajili ya kufanya fujo pamoja na kuchoma moto ofisi za chama hicho.
“Tumewakamata watu 22 na baada ya mahojiano, walibainika kuwa ni wanachama wa CUF kutoka Unguja katika matawi mbalimbali na wapo katika kitengo cha ulinzi, wamekuja kwa kazi maalum ya kufanya vurugu na uhalifu,” amesema.
Sirro amedai kuwa, watu hao wamekuja kwa maelekezo ya Nassoro Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Zanzibar ambaye aliwaamuru kuungana na walinzi wenzao wengine waliopo ofisi za makao makuu ya chama hicho Buguruni.
Amezitaja zana za kufanyia uhalifu walizokutwa nazo watu hao kuwa ni pamoja na mapanga, jambia, visu na chupa 10 za dawa ya kupulizia (spray) zikiwa kwenye boksi lenye maandishi ya kichina.
Wakati polisi Dar wakisema hayo, MwanaHALISI online inafahamu kuwa, jeshi hilo ‘lilisimamia’ uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Prof. Lipumba katika Ofisi Kuu za CUF Buguruni mnamo Jumamosi ya tarehe 24 Septemba mwaka huu.
Polisi waliokuwa na silaha za moto katika eneo la nje ya ofisi hizo, walishuhudia wafuasi wa Prof. Lipumba wakiruka uzio na kuwapiga walinzi wa CUF huku wakivunja kufuli za lango kuu sambamba na mlango wa kuingilia ofisi za viongozi.
Pamoja na uvamizi na uharibifu huo lakini Jeshi la Polisi halikuchukua hatua zozote kuzuia zaidi ya kutazama tu kilichokuwa kikiendelea.
Kitendo cha polisi kujitokeza na kudai limekamata wahalifu waliokuwa wakipanga kuvamia ofisi hizo na kuzichoma moto kinaweza kuhusishwa na siasa za mvutano zinazoendelea ndani ya CUF ambapo Prof. Lipumba ambaye amefukuzwa uanachama amekuwa akipewa ulinzi kila anapofanya uvamizi dhidi ya chama hicho.
Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Julius Mtatiro, aliyekuwa mwenyekiti wa kikao cha mkutano mkuu wa CUF taifa, alilishutumu Jeshi la Polisi kwa kumuongoza na kumsaidia Prof. Lipumba kuvamia mkutano huo kwa kumuingiza ndani yeye na kundi lake ingawa hawakuwa mjumbe.
No comments: