SIMBA HII BALAA TUPU


Beki wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou.

Said Ally, Dar es Salaam

BEKI wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, ameweka wazi kuwa kutokana na kiwango cha hali ya juu kilichoonyeshwa na Simba, ni wazi kuwa wana kazi kubwa watakapokutana nao kwenye kuwania ubingwa.

 

Bossou ameyasema hayo kutokana na kuishuhudia Simba ikicheza dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, Jumatatu ya wiki hii ambapo Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Akizungumza na Championi Ijumaa,Bossou alisema kuwa timu hiyo imebadilika mno ukilinganisha na msimu uliopita ambapo hayo yametokana na kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa ambao wanaweza kuwapa presha katika kuwania ubingwa kwa msimu huu.

“Simba hii imebadilika sana kwa jinsi nilivyoiona leo (Jumatatu hii) na kiukweli nikiri kwamba sasa wana wachezaji ambao wanaweza kutupa presha tutakapokutana nao lakini hata kwenye mbio za kuwania ubingwa kwa msimu huu.

“Lakini tayari tumeshawaona na hata Kocha Hans van Der Pluijm naye amewashuhudia, hivyo tutakachoenda kukifanya ni kuandaa mbinu na namna ambayo tutaweza kuwadhibiti pale tutakapokutana nao,” alisema Bossou raia wa Togo ambaye alikuwepo Uwanja wa Taifa kuishuhudia Simba.

Kuhusu mshambuliaji wa Simba, Laudit Mavugo, Bossou alisema: “Ni mchezaji mzuri lakini huu ni mchezo wa kirafiki inawezekana Wakenya labda hawakuwa vizuri.”

Simba imeshindwa kufanya vizuri kwa misimu minne mfululizo hali ambayo ilizipa nafasi Yanga na Azam FC kutamba Yanga wakienda mbele zaidi kwa kujiita Wakimataifa kutokana na ushiriki wao kwenye michuano ya kimataifa huku Simba wakishindwa kufuzu kutokana na kuonyesha kiwango cha chini.

Usajili wa wachezaji wa kimataifa waliopo Simba kina Vicent Angban, Mavugo, Juuko Murshid, Musa Ndusha, Janvier Bokungu, Fredrick Blagnon na Method Mwanjali umewapa imani Wanasimba kuamini kuwa huu ni mwaka wao wa kufanya vizuri.

No comments:

Powered by Blogger.