Jaji Mutungi, wakala wa CCM?

Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania
JINA la Francis Mutungi, msajili wa vyama vya siasa nchini, limegonga tena vichwa vya habari. Jina hili huwa linajitokeza kwa nadra. Ila linapojitokeza, huwa ni kwa masuala yenye utata, 

Mara ya mwisho Jaji Mutungi alisikika akitetea “amri” ya Rais wa Jamhuri, John Pombe Magufuli ya kuzuia mikutano ya hadhara.
Mara hii, Jaji Mutungi ameibukia kwenye tamko lililotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa tarehe 1 Septemba 2016, itakuwa siku ya mikutano na maandamano nchi mzima.
Msajili wa vyama anasema, tamko la Chadema “juu ya hali ya kisiasa na mfumo wa vyama vingi nchini,” linalenga kuingiza nchi kwenye machafuko.
Anasema tamko limejaa lugha ya uchochezi, kashfa na maudhi na kwamba linakiuka sheria na linahamasisha uvunjifu wa amani.
Amenukuu kifungu cha 9 (2) (f) cha sheria ya vyama vya siasa, anachodai kinakataza viongozi wa vyama vya siasa na wanachama wao, kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi.
Anasema, kwa kutumia kanuni 6 (2) ya maadili ya vyama vya siasa, anakemea tamko hilo hadharani; na anaitaka Chadema kutoendelea na tabia yake ya kutoa alichoita kauli za uchochezi.
Anaongeza, “…kwa dhamana niliyopewa kama msajili wa vyama vya siasa, nalikemea tamko hili na naviasa vyama vyote nchini kutimiza wajibu wao kwa weledi kama taasisi.”
Mkutano wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema ulitangaza tarehe 1 Septemba 2016, kuwa siku ya mikutano na maandamano nchi mzima.
Kamati Kuu ilikutana jijini Dar es Salaam, Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita. Sasa tujadili:
Kwanza, Jaji Mutungi anajua kuwa Jamhuri ya Muungano inaongozwa na Katiba. Rais wake wa sasa – John Pombe Magufuli – kama walivyo watangulizi wake, ameapa kulinda na kutetea katiba ya nchi.
Kile ambacho rais ana mamlaka nacho ni kusimamia mchakato wa Katiba Mpya; siyo kama rais binafsi.
Anatekeleza matakwa ya wananchi ambao wote kwa umoja wao, wamempa yeye – rais wa Jamhuri – mamlaka ya kusimamia raslimali, ulinzi na usalama wa mali zao.
Naye mjasili wa vyama vya siasa, aliyepo sasa na waliomtangulia, wameapa kulinda katiba na kuitetea.
Pamoja na kwamba miongoni mwa sifa za kuwa msajili wa vyama vya siasa, ni kuwa jaji wa mahakama kuu, hakuna ambako kunamruhusu kutunga katiba; au kutafsri sheria za nchi.
Kazi kuu ya msajili wa vyama vya siasa – huwa anajiita “mlezi wa vyama vya siasa” – ni kuandikisha vyama.
Haikutegemewa kuwa msajili wa vyama aliyeapa kulinda katiba, mtaalamu wa sheria na mtu ambaye ni jaji wa mahakama kuu, kushindwa kusimamia sheria na kanuni za msingi za vyama vya siasa.
Katiba imeruhusu uwapo wa vyama vya siasa, mikusanyiko, mikutano ya hadhara na maandamano.
Ndivyo ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Jamhuri inavyoeleza.
Hata katika utangulizi wake, Katiba ya Jamhuri, inaelekeza taifa hili litajengwa kwa misingi inayozingatia uhuru na haki. Litajengwa kupitia vyama vya siasa, chini ya mfumo wa vyama vingi.
Kilichofanywa na Chadema – kujadili na kutangaza kuchukua hatua – dhidi ya wanaotaka kutenda uhalifu unaolenga ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi, siyo uvunjaji wa katiba. Ni ulinzi wa Katiba.
Pili, vyama vyote nchini vilivyopata usajili katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, vinapaswa kufanya kazi za kisiasa na zenye lengo la kushika dola.
Kazi kuu ya chama cha siasa, ni kutunga sera za kuongoza nchi na kunadi sera zake kwa wananchi.
Kukizuia chama cha siasa kutimiza wajibu wake huo wa kikatiba, ni kutaka kuingiza nchi katika utawala wa mtu mmoja. Ni kuruhusu uvunjifu wa katiba na sheria Na. 5 ya vyama vya siasa.
Kuzuia mikutano ya kisiasa ni kuruhusu uvunjifu wa katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 na marekebisho Na.32 ya mwaka 1994.
Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, kila chama cha siasa kitakuwa na uhuru wa kutafuta wanachama, kutoa elimu ya uraia na elimu ya uchaguzi na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano.
Vyama haviwajibiki kunyenyekea kwa jeshi la polisi, usalama wa taifa wala Ikulu ili kuomba ruhusa.
Msajili wa vyama, badala ya kumkemea Rais Magufuli anayezuia vyama kufanya kazi zake za kikatiba, amejipa mamlaka ya kutafsiri kauli za Chadema na kuitishia.
Mutungi anadai rais “hajapiga marufuku shuguli za kisiasa.” Anasema alichofanya ni kufungua milango ya ushirikiano na wanasiasa katika alichoita, “kuendeleza taifa.”
Mtungi ametaka wanasiasa kutopotosha wito wa rais kisiasa kwa kudai kuwa rais amefuta harakati za siasa.
Lakini sote tumemsikia rais Magufuli akieleza, “wanasiasa wasubiri 2020 ndiyo warejee kwenye harakati za siasa.”
Amesisitiza tena hili akiwa mkoani Singida juzi Jumamosi. Ameng’aka, “sijaribiwi” katika suala la vyama vya upinzani kufanya mikutano ambayo ameizuia.
Kinachoonekana hapa ni kwamba Mwenyekiti wa CCM na Rais John Pombe Joseph Magufuli, anataka kuongoza chama chake na kisha aongoze vyama vingine kupitia kichaka cha urais.
Yaani rais anataka kuekeleza vyama vingine ama wanasiasa wengine mahali pakwenda? Lini waende na nani wa kuona?
Lakini msajili yuko kimya. Hajakemea kauli za aina hii zinazoashiria kupasua nchi. Hajamueleza bosi wake – rais – kuwa katazo lake linakwenda kinyume na sheria za nchi na linamega nchi vipandevipande.
Kama amemueleza, hajaeleza umma kuwa rais hashauliki au hataki kufuata ushauri wake juu ya kauli yake.
Ameishia kunakiri kuwa Chadema imetukana, lakini hataki kutaja anachoita “matusi.”
Rais Magufuli anasema, wanaoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara ni wawakilishi wa wananchi. Lakini yeye anazunguka nchi mzima kwa kisingizio cha kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa rais.
Kwamba mwenyekiti wa chama, mbunge au mjumbe wa Kamati Kuu (CC), hawana mamlaka ya kwenda kwa wananchi wa maeneo mengine, kueleza sera za chama chao na udhaifu wa serikali.
Siyo hivyo tu: Aliyekuwa mshindani wake mkuu, Edward Lowassa, haruhusiwi kwenda kuwashukuru waliompigia kura.
Haruhusiwi kuwaeleza kilichotokea hadi “kura walizompigia kutotosha”katika majumuisho ya mwisho yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva.
Haruhusiwi kwenda kuwaeleza kwa nini kura zilionekana vituo vya kupigia kura na katika majumuisho majimboni, lakini hazikuonekana kwenye karatasi ya mwisho iliyosomwa na Jaji Luvuba.
Haruhusiwi kukutana na wafuasi wake na kuwaeleza kililichosababisha yeye – Edward Ngoyai Lowassa – kukubali matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na NEC, wakati vyombo vya dola vimevamia ofisi zake za majumuisho ya kura.
Naye Fredrick Sumaye, mjumbe wa CC ya Chadema na waziri mkuu mstaafu, haruhisiwi kukutana na wananchi kufafanua madhara ya kauli tata za rais.
Kwa mfano, haruhusiwi kukutana na wananchi na kuwaeleza maana ya hatua ya rais ya kupunguza kima cha chini cha kodi kutoka asilimia 11 hadi asilimia tisa (9).
Haruhusiwi kueleza kuwa kiwango hicho kilichotangazwa na rais kwa mbwembwe, ni sawa na Sh. 3, 800 kwa mwezi; na sawa na Sh. 126.7 kwa siku.
Rais Magufuli alitangaza punguzo la kodi za mishahara ya wafanyakazi mkoani Mbeya, tarehe 1 Mei 2016.
Ukiacha hilo kuna hili pia: Ni vema msajili akafahamu kuwa kabla ya kukoromea Chadema, akemee matusi na dhihaka zilizofanywa na CCM katika mkutano wao mkuu maalum uliofanyika wiki iliyopita, mjini Dodoma.
Katika mkutano huo, CCM wametoa kauli nyingi za matusi, dhihaka na kejeli dhidi ya upinzani na viongozi wao wakuu, akiwamo Sumaye na Lowassa.
Msajili wa vyama anayejitapa kulinda vyama, hakupaswa kuwa moto kwa Chadema na kuwa baridi kwa CCM. Kuamua kuchukua mkondo huo ni kujivunjia hadhi binafsi na ofisi ya msajili.
Tatu, ni muhimu rais akaelezwa kuwa anaweza kuzima wananchi na vyama vyao na kujitangaza mshindi; lakini hawezi kupambana na historia. Hatashinda.
Wala kuzuia vyama vya upinzani au wanasiasa kutoka upinzani kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kunadi sera, hakuzuii chama tawala kuondolewa madarakani kwa utashi wa wananchi.
Kwa miaka mitano mfululizo – 1995 hadi 2000 – Chama cha Wananchi (CUF) hakikuweza kufanya mikutano ya hadhara katika mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mkoa wa Kaskazini Unguja ndiko anakotoka aliyekuwa rais wa wakati huo, Dk. Salmin Amour Juma na Ali Juma Shamhuna, aliyekuwa waziri wa uwekezaji. Shamhuna alikuwa kipenzi na nguzo kuu ya Dk. Salimin.
Kilizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, warsha, makongamano hadi kufungua tawi. Hakikuruhusiwa  kupeleka huko viongozi wowote wa kitaifa ili kuimarisha chama na kukutana na wafuasi wa chama na wananchi kwa ujumla.
Kila walipojaribu kutaka kufanya hivyo, walizuiwa na vyombo vya dola kwa amri ya Ikulu.
Lakini uchaguzi mkuu ulipowadia – Oktoba 2000 – miongoni mwa majimbo yaliyotangazwa mapema kutwaliwa na CUF, Unguja ni pamoja na jimbo la Bubwini, mkoa wa Kaskazini.
Hivyo basi, kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani ni kujenga chuki bila sababu ya maana miongoni mwa wananchi.
Rafiki yangu ananiambia kuwa katika mazingira ya sasa na uelewa mpana wa mambo ya siasa, kibano cha Magufuli chaweza kuwa njia ya kuua CCM kwa vitendo na kutoka ndani kabisa ya chama hicho.
Makala hii ilitoka kwenye Gazeti la MwanaHALISI Toleo No. 350 la tarehe 1-7 Agosti mwaka huu.

No comments:

Powered by Blogger.