HABARI ZA YANGA ZAIFIKIA FIFA,MANJI AWEKWA KIKAANGONI

Dar es Salaam.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema hatima ya usajili wa Yanga na Coastal Union inasubiri huruma ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Awali, muda uliopangwa na TFF kwa usajili huo ulikuwa ni kati  ya Juni 15 hadi Agosti 6, saa 6.00 usiku. Hata hivyo, Yanga na Coastal Union zimeshindwa kuwasilisha usajili wao  kwa muda, kati ya klabu 64 za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.

“Yanga wamewasilisha utetezi wao na sababu za kuchelewesha usajili, kama shirikisho tumeshautuma Fifa, hivyo tunawasikilizia kuona watatoa majibu gani,” alisema ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas.

Katibu mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa upo uwezekano wa Yanga kuadhibiwa na Fifa kwa kosa hilo kulingana na kanuni. Kanuni zimeainisha usajili wa wachezaji wa ndani kuwa utafanyika  wiki mbili kabla ya kuanza ligi ya nchi husika.

Amesema TFF ilizijulisha klabu mapema zikamilishe usajili wao kwani mfumo huo wa usajili unasimamiwa na Fifa na si chombo kingine.

“Tumetaka maelezo ili tuzisaidie klabu  zikubali kesi zao Fifa.  Dirisha hilo  linasimamiwa na Fifa, siyo  sisi, unaweza kuomba Fifa, wanaoweza kuamua ni wao, Fifa siyo. 

“Kila mwaka adhabu zimekuwa zikitolewa kwa vyama vya mpira kwa sababu unapokosea wanaamini kila kitu kinafahamika na haina utetezi.

“Baadhi ya klabu zimewahi kupata moja kwa moja adhabu kutoka Fifa kutokana na kutofanya usajili vizuri, nakumbuka Yanga waliadhibiwa kwa usajili wa Mbuyu Twite.

“Hivyo, kuna uwezekano wa kupigwa faini kutokana na ucheleweshaji huo,” amesema Mwesigwa.

Kalenda ya matukio iliyotolewa na TFF Juni mwaka huu ilionyesha kuwa baada ya  usajili kwa wachezaji wazawa kufungwa Agosti 6, kipindi kinachobakia hadi Septemba 6 ni usajili wa wachezaji wanaotoka nje.

Barua pepe iliyoandikwa na mmoja wa maofisa wa idara (nakala tunayo) inayosimamia mfumo huo, Agosti 4  iliikumbusha Yanga ikamilishe zoezi hilo ndani ya muda uliopangwa.

No comments:

Powered by Blogger.